Chelsea kuendeleza ubabe Conference Ligi

Muktasari:
- Chelsea imeondoka na wachezaji wengi chipukizi huku ikiwaacha wachezaji wazoefu kama Christopher Nkunku, João Félix, Benoît Badiashile, na Mykhaylo Mudryk huku Maresca akitaja kuwapa nafasi wachezaji chipukizi kwenye mchezo wa leo.
Chelsea itashuka dimbani kwenye uwanja wa ugenini leo dhidi ya Astana kwenye mchezo wa Europa Conference Ligi ambapo imekuwa na mwendelezo mzuri wa matokeo kwenye michuano hii.
Kocha Enzo Maresca ameiongoza Chelsea kupata ushindi kwenye michezo minne iliyocheza ambapo inaongoza kwenye msimamo wa Conference Ligi ikiwa na pointi 12 sawa na Legia Warszawa ambayo nayo haijapoteza mchezo kwenye mashindano hayo.
Kikosi cha Enzo Maresca kilifanikiwa kushinda dhidi ya Gent mabao 4-2, Panathinaikos 4-1, na FC Noah 8-0 kabla ya kuwashinda Heidenheim kutoka Ujerumani kwa mabao 2-0 ambayo yalifungwa na Christopher Nkunku dakika ya 51 na bao la dakika za mwisho lililofungwa na Mykhaylo Mudryk.
Chelsea imeondoka na wachezaji wengi chipukizi huku ikiwaacha wachezaji wazoefu kama Christopher Nkunku, João Félix, Benoît Badiashile, na Mykhaylo Mudryk huku Maresca akitaja kuwapa nafasi wachezaji chipukizi kwenye mchezo wa leo.
Tofauti na Ligi ya Mabingwa Ulaya na ile ya Europa ambapo timu zinacheza mechi nane kwa mfumo wa nyumbani na ugenini, timu za Conference League zina mechi sita pekee kwenye ratiba zao ambapo Chelsea ipo kileleni mwa Conference Ligi yenye timu 36.
Chelsea itaingia kwenye mchezo wa leo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kucheza mechi nane bila kupoteza kwenye mashindano yote tangu ilipofungwa mabao 2-0 dhidi ya Newcastle United kwenye EFL Cup Oktoba 30, 2024.
Chelsea pia wameshinda mechi zao nne za ugenini mfululizo, ikiwemo ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Tottenham Hotspur kwenye Ligi Kuu mwishoni mwa wiki iliyopita. Ushindi huo umewapandisha hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi kuu England wakiwa pointi nne nyuma ya vinara Liverpool wenye pointi 35 ambao wana mechi moja mkononi.
Astana imeonekana kuwa na hali mbaya kwenye mashindano haya baada ya kupata ushindi mara moja wa bao 1-0 dhidi ya Backa Topola huku ikitoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Vitoria Guimaraes ikiwa imepoteza mechi mbili ambapo ilifungwa mabao 2-0 dhidi ya The New Saints kabla ya kufungwa tena bao 1-0 dhidi ya Pafos.
Mechi nyingine za leo
Astana vs Chelsea
Fiorentina vs LASK
Copenhagen vs Hearts
Dinamo-Minsk vs Larne
Noah vs APOEL
Petrocub vs Real Betis
HJK Helsinki vs Molde
İstanbul Başakşehir vs Heidenheim
Legia Warszawa vs Lugano
Olimpija Ljubljana vs Cercle Brugge
St. Gallen vs Vitória SC
Mladá Boleslav vs Jagiellonia Białystok
Gent vs TSC
Omonoia vs Rapid Wien
Pafos vs Celje
Shamrock Rovers vs Borac
The New Saints vs Panathinaikos
Víkingur Reykjavík vs Djurgården