Chancel Mbemba aisogeza DR Congo mlangoni Kombe la Dunia
Chancel Mbemba ndio jina linaloimbwa zaidi kwa sasa miongoni mwa mashabiki wa soka nchini DR Congo na Afrika kwa ujumla. Mbemba, ambaye ni nahodha wa kikosi hicho maarufu The Leopards, ameisogeza nchi yake mlangoni kuungana na wababe watakaokipiga kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026.
Fainali hizo zitafanyika kwa ushirikiano wa mataifa ya Marekani, Canada na Mexico, baada ya kufunga penati muhimu kwenye mchezo wa mtoano dhidi ya Nigeria.
Nigeria na DR Congo walikuwa uwanjani usiku wa Jumapili, Novemba 16, 2025 kusaka tiketi ya kucheza hatua ya mtoano na wababe kutoka mabara kati ya Asia au Amerika kusaka nafasi ya kufuzu kucheza Kombe la Dunia 2026.
Katika mchezo huo, Nigeria ilitangulia kwa bao la mapema, dakika 3 ya mchezo kupitia kwa Frank Onyeka ambalo lilidumu hadi dakika ya 30 ya mchezo kabla ya Meschack Elia kusawazisha.
Mchezo huo ambao ulikuwa 100 kwa Mbemba akiwa na jezi ya DR Congo, ulilazimika kuamuliwa kwa mikwaju ya penati baada ya sare ya bao 1-1. Katika hatua hiyo Nigeria ikakubali kupoteza kwa penati 4-3 mbele ya DR Congo.
Itakumbwa kuwa kabla ya kukutana na Nigeria ambayo iliichapa Gabon mabao 4-1, DR Congo ilitoka kuizamisha Cameroon kwa bao 1-0 huku Mbemba akiibuka shujaa kwenye mchezo huo kwa kufunga bao la jioni, dakika 91 ambalo lilikatisha ndoto za Nigeria kushiriki fainali hizo.
Endapo itafanikiwa kushinda mchezo unaofuata unaotarajiwa kupigwa mapema mwakani, DR Congo itarejea kwenye fainali hizo baada ya kuzikosa kwa muda mrefu. Mara ya mwisho ilishiriki Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1974 wakati huo ikijulikana kama Zaire.
Mbemba (37) anayekipiga klabu ya Lille ya Ufaransa, amewahi kuzichezea Newcastle United ya England, FC Porto ya Ureno, Anderlecht na Marseille.