Chama aanza kutupia Yanga, Bacca anyimwa penati

Muktasari:
- Mabao 4-0 yametosha kuipa Yanga ushindi katika mchezo wa kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vital’O mchezo wa raundi ya kwanza.
Dar es Salaam. Yanga imeanza vyema kuchanga karata ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF) hatua za awali kwa kuichapa Vital'O ya Burundi mabao 4-0.
Mabao hayo yalifungwa na mshambuliaji, Prince Dube dakika ya tano akipokea pasi ya Clatous Chama ambaye aliifungia timu hiyo bao la pili dakika ya 68 na Clement Mzize aliyeweka nyavuni dakika ya 73 na Aziz KI aliyefunga dakika ya 90.
Kwenye mchezo huo Yanga ilikuwa ugenini Uwanja wa Azam Complex, Chamazi dhidi ya Vital'O ambayo ilichagua uwanja huo kuwa wa nyumbani kutokana na viwanja vyao huko Burundi kutokidhi vigezo vya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Dube na Chama wanakuwa wachezaji wa kwanza wapya kwenye klabu hiyo kuweka historia ya kufunga mabao kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa.
Wachezaji hao wawili walijiunga na Yanga msimu huu, Dube akitokea Azam FC alikodumu kwa misimu mitatu tangu alipojiunga 2020 huku Chama akitokea Simba.
BACCA AOMBA PENATI
Wakati mwamuzi wa mchezo huo mwamuzi alipotoa penalti katika dakika ya 90 baada ya Aziz KI kuchezewa rafu, beki wa Yanga, Ibrahim Bacca alionekana kuomba kupiga.
Iko hivi baada ya mwamuzi kutoa penati Bacca alimuomba kocha Miguel Gamondi apige penati ile huku akiashiria ishara ya kujifuta kama kutoa mkosi wa kukosa penati.
Hata hivyo baada ya kuiomba Gamondi alimkatalia beki huyo wakati huo huo jukwaa walilokaa viongozi wa Yanga wakiomba Bacca apewe.
Baada ya filimbi ya mwisho ya mwamuzi, Aziz KI ambaye ndio alipiga penati hiyo alimfuata Bacca na kuzungumza nae.
Yanga itarudiana tena Jumamosi ijayo dhidi ya Vital'O kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya mtoano wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika, mchezo utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.