Bayern ilivyoituliza Madrid Bernabeu, Arsenal ikitamba ugenini
Muktasari:
- Bayern Munich sasa wanajiandaa na mchezo wa marudiano utakaopigwa katika dimba la Alianz Arena nchini Ujeruman.
Madrid, Hispania. Mabingwa wa Ulaya mara 15, Real Madrid, wamejikuta wakipoteza baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Bayern Munich katika mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya uliopigwa katika dimba la Santiago Bernabeu.
Kocha wa timu ya taifa ya England, Thomas Tuchel, alikuwa miongoni mwa waliokuwepo uwanjani hapo kushuhudia pambano hilo kali, akiwafuatilia kwa karibu nyota wake Harry Kane, Jude Bellingham na Trent Alexander-Arnold.
Bayern walionekana kuwa bora katika sehemu kubwa ya mchezo huo, wakipata mabao yao kupitia Luis Díaz na Harry Kane, kabla ya Kylian Mbappé kufunga bao kwa Real Madrid kipindi cha pili.
Mshambuliaji wa Bayern Munich, Harry Kane wakati akishangilia baada ya kufunga bao la pili katika mechi ya Ligi ya ,Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid. Picha na Mtandao
Bao la Kane alifunga ndani ya sekunde 22 tu baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, kufuatia shambulizi lililoanzishwa na Aleksandar Pavlović aliyemnyang’anya mpira Álvaro Carreras kabla ya kumpasia Michael Olise, ambaye alimuwekea Kane pasi ya kufunga.
Kwa upande wa Real Madrid, walijaribu kusawazisha lakini walikwama mbele ya kipa mkongwe Manuel Neuer ambaye alionyesha kiwango cha juu na kuokoa michomo kadhaa hatari.
Mchezo huo pia ulimwonesha Alexander-Arnold akiwa na sura mbili tofauti akionekana dhaifu upande wa ulinzi lakini hatari sana anaposhambulia. Ni yeye aliyetoa pasi ya mwisho kwa Mbappé kufunga bao la Madrid dakika ya 74, baada ya kupokea mpira kutoka kwa Federico Valverde.
Beki wa kulia wa Real Madrid, Trent Alexander-Arnold akijaribu kuondoa mpira katika eneo la hatari kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich. Picha na Mtandao
Wakati huo huo, Bellingham alianza mchezo akiwa benchi na kuingia baadaye katika dakika ya 60 kujaribu kuisaidia Madrid kurejea mchezoni, lakini juhudi zao hazikutosha kubadili matokeo.
Kwa ushindi huo, Bayern Munich sasa wanajiandaa na mchezo wa marudiano utakaopigwa katika dimba la Alianz Arena nchini Ujeruman huku wakiwa na faida ya bao moja, wakitafuta kuvunja mwiko wa miaka 12 ya kutotawala dhidi ya Real Madrid katika michuano ya Ulaya.
Mshambuliaji wa Arsenal, Kai Havertz wakati akifunga bao la ushindi katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Sporting CP. Picha na Mtandao
Katika mechi nyingine ilishuhudiwa Arsenal ikiichapa Sporting CP bao 1-0 ambalo lilifungwa na mshambuliaji Kai Havertz ambaye aliingia kutokea benchi.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Chelsea, alifunga bao hilo katika dakika za majeruhi na kufufua matumaini ya Arsenal kutinga hatua ya nusu fainali huku wakisubiri mechi ya marudiano itakayopigwa kwenye dimba la Emirates.
Tangu ianze kushiriki mashindano hayo msimu huu, Arsenal hadi sasa haijapoteza mchezo wowote katika Ligi ya Mabingwa Ulaya ikishinda mechi 10 na kutoka sare mara moja tu.