Azam yaendeleza mkosi wa Singida BS nyumbani
Beki wa Azam FC, Lusajo Mwaikenda akishangilia baada ya kufunga bao la kuongoza katika ushindi wa 2-1 kwenye mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Singida Black Stars. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Fei Toto pia amebakisha bao moja kumfikia kinara wa kufumania nyavu kwenye Ligi Kuu, Fabrice Ngoy wa Namungo FC ambaye hadi sasa amepachika mabao nane.
Mabao ya kipindi cha pili ya Lusajo Mwaikenda na Feisal Salum 'Fei Toto' yameihakikishia Azam FC ushindi wa ugenini na kuiwezesha kupunguza pengo la pointi baina yake na vinara Yanga kubakia sita.
Ushindi huo wa mabao 2-1 dhidi ya Singida Black Stars kwenye Uwanja wa Airtel, Singida, umeifanya Azam FC kufikisha pointi 32 na kupanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikitoka ya tatu.
Mwaikenda ndiye ametangulia kuifungia bao Azam FC katika dakika ya 50 akimalizia krosi ya Idd Selemani 'Nado na dakika ya 64, Fei Toto akaongeza bao la pili akimalizia pia pasi ya Nado.
Dakika ya 71, Singida Black Stars ilipata bao la kufutia machozi lililofungwa na Ayoub Lyanga ambaye amefunga kwa kichwa akimalizia mpira wa faulo wa Ande Koffi.
Kwa kufunga bao leo, Fei Toto amezidi kujikita kileleni katika chati ya wachezaji wanaoongoza kwa kuhusika na mabao mengi kwenye Ligi Kuu hadi sasa ambapo amefikisha mabao 12, akifunga saba na kutoa pasi za mwisho tano.
Fei Toto pia amebakisha bao moja kumfikia kinara wa kufumania nyavu kwenye Ligi Kuu, Fabrice Ngoy wa Namungo FC ambaye hadi sasa amepachika mabao nane.
Kichapo cha leo kimekuwa ni cha tatu mfululizo kwa Singida Black Stars kupata nyumbani kwenye Uwanja wa Airtel katika Ligi Kuu baada ya kupoteza dhidi ya Yanga na Simba.
Hapana shaka Azam FC sasa inaiombea Simba ipoteze mechi ya kesho dhidi ya Coastal Union ili yenyewe ibakie katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.
Singida Black Stars imeendelea kubakia katika nafasi yake ya sita ikiwa na pointi 25.