Arsenal yatinga 16 bora Ulaya kwa rekodi ikiichapa Inter
Muktasari:
- Arsenal imejihakikishia kuongoza msimamo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya huku ikiwa na mechi mkononi baada ya kufikisha pointi 21.
Arsenal imekuwa timu ya kwanza kujihakikishia hatua ya 16 bora ya Liginya Mabingwa Ulaya baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 ugenini dhidi ya Inter Milan, Jumanne, Januari 21, 2026.
Ushindi huo umeifanya Arsenal kufikisha pointi 21 ambazo zimeifanya ijihakikishie kumaliza katika nafasi nane za juu ambazo timu za hapo zinafuzu moja kwa moja hatua inayofuata.
Mabao ya Arsenal katika mchezo huo yalipachikwa na Gabriel Jesus aliyefunga mawili huku lingine moja likiwa la Viktor Gyokeres wakati bao la Inter lilipachikwa na Petar Sucic.
Ni ushindi wa saba mfululizo kwa Arsenal kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu na ndio timu pekee ambayo imepata ushindi wa asilimia mia moja na hakuna nyingine ambayo imeweza au itaweza kufanya hivyo.
Katika Uwanja wa Santiago Bernabeu, Hispania, Kylian Mbappe aliiongoza Real Madrid kuiteketeza timu yake ya zamani, Monaco kwa mabao 6-1.
Mbappe alifunga mabao mawili huku mengine yakifungwa na Franco Mastantuono, Vinicius Junior, Jude Bellingham na moja la kujifunga la Thilo Kehler huku bao moja la Monaco likipachikwa na Jordan Teze.
Manchester City ilikutana na mshituko nchini Norway ambako ilijikuta ikichapwa mabao 3-1 na Bodo/Glimt na Kairat ilichapwa mabao 4-1 na Club Brugge.
PSG ilichapwa mabao 2-1 na Sporting Lisbon na FC Copenhagen ililazimishwa sara ya bao 1-1 na Napoli.
Tottenham Hotspur ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Borussia Dortmund na Olympiacos ikashinda mabao 2-0 dhidi ya Bayer Leverkusen.
Kwingineko, Villarreal ilichapwa mabao 2-1 nyumbani na Ajax.