Arsenal yaichapa West Ham ikibakiza mechi mbili itwae EPL
Baadhi ya wachezaji wa Arsenal wakishangilia bao la ushindi ailofunga Leandro Trossard dhidi ya West Ham. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Arsenal imebakiza mechi dhidi ya Burnley na Crystal Palace huku ikiitaji ushindi kwenye michezo hiyo ili iwe bingwa wa EPL msimu huu.
London, England. Bao la dakika za jioni alilofunga Leandro Trossard limetosha kuipa pointi tatu Arsenal ‘Washika Bunduki’ ambayo sasa inahitaji ushindi katika mechi mbili za mwisho kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England (EPL) 2025-2026.
Trossard amefunga bao hilo katika dakika ya 83 ambapo alimalizia kwa ustadi pasi aliyopewa na nahodha wake Martin Odegaard ambaye aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Eberechi Eze.
Kiungo wa Arsenal, Leandro Trossard wakati akifunga bao pekee la ushindi kwa upande wa Arsenal dhidi ya West Ham. Picha na Mtandao
Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa London ilishuhudiwa dakika za mwishoni wenyeji West Ham wakifanya mashambulizi kusawazisha matokeo ambapo walipachika bao ambalo baadaye lilikataliwa na VAR baada ya kuonekana kipa wa Arsenal, David Raya alifanyiwa madhambi wakati alipokuwa kwenye harakati za kutaka kuokoa shambulizi hilo.
Hadi sasa Arsenal inayoongozwa na Meneja Mikel Arteta imeendelea kujikita kileleni mwa Ligi Kuu ya England ikifikisha idadi ya pointi 79 huku ikitengeneza tofauti ya pointi tano dhidi ya wapinzani wao wa karibu Manchester City wenye pointi 74.
Kipa wa Arsenal, David Raya wakati akifanyiwa faulo alipokuwa akijaribu kuokoa shambulizi la kona dhidi ya West Ham. Picha na Mtandao
Hata hivyo, Man City wana faida ya mchezo mmoja mkononi utakaochezwa Jumatano, Mei 13 mwaka huu dhidi ya Crystal Palace.
Ushindi wa leo umeipa Arsenal matumaini ya kuukaribia ubingwa wa Ligi Kuu England ambao imekuwa ikiusaka kwa miaka 22 bila mafanikio tangu iliposhinda mara ya mwisho msimu wa 2002/2003 ilipokuwa chini ya Meneja Arsene Wenger.
Baada ya kuacha kipigo hicho kwa Wagonga Nyundo wa London, sasa vijana wa Arteta watakuwa na kibarua kingine Mei 18, 2026 watakaposhuka kwenye dimba la Emirates kuivaa Burnley kisha Mei 24 watakuwa ugenini kukamilisha ratiba ya ligi hiyo watakapokutana na Crystal Palace.