Arsenal yatangulia fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya
Muktasari:
- Washika Mitutu hao wa London wametinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya miaka 20 tangu walipofanya hivyo mwaka 2006.
London, England. Arsenal imekuwa timu ya kwanza kutinga katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu ambayo imepangwa kufanyika Mei 30, 2026 kwenye Uwanja wa Puskás Aréna huko Budapest, Hungary.
Arsenal imefanikiwa kuingia katika fainali hiyo baada ya kupata ushindi wa jumla wa mabao 2-1 dhidi ya Atletico Madrid ikiwa ni baada ya kutoka sare ya 1-1 katika mechi ya ugenini iliyopigwa wiki iliyopita kule Madrid, Hispania huku jana Mei 5, 2026 ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Emirates, jijini London.
Bao pekee la Arsenal ‘The Gunners’ katika mchezo huo limefungwa na Bukayo Saka katika dakika ya 44 ambaye alimalizia mpira uliotemwa na kipa wa Atletico Madrid, Jan Oblak baada ya kushindwa kudaka shuti kali la Leandro Trossard.
Kipindi cha pili, Atletico walionekana kufanya mashambulizi kadhaa ili kurejea mchezoni lakini hayakuzaa matunda baada ya kazi nzuri iliyofanywa na safu ya ulinzi ya Arsenal ikiongozwa na Gabriel Magalhães ambaye dakika ya 50 aliokoa shambulizi la hatari dhidi ya mshambuliaji Giuliano Simeone ambaye alionekana kuwa karibu kuisawazishia Atletico baada ya kumzidi maarifa kipa wa Arsenal, David Raya aliyekuwa ameliacha lango wazi.
Arsenal nao walitengeneza nafasi kadhaa ikiwemo ile ambayo aliikosa mshambuliaji wao Victor Gyokeres dakika ya 65 ambapo alipiga mpira uliopita juu ya lango baada ya kupokea pasi kutoka pembeni iliyopigwa na Pierro Hincapie.
Hata hivyo, vijana wa Meneja Mikel Arteta waliweza kulinda vizuri lango lao na kuhakikisha wanakata tiketi ya kutinga fainali ikiwa ni baada ya miaka 20 kupita tangu walipofanya hivyo Mei 17, 2006.
Katika fainali hiyo ambayo ilipigwa Paris, Ufaransa, Arsenal ilipoteza kwa kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Barcelona ambayo ilitoka nyuma kwa bao moja na kuibuka mshindi.
Katika mashindano hayo makubwa ya klabu Ulaya, Arsenal imeweka historia ya kipekee msimu huu ikiwa ndio timu pekee inayokwenda fainali bila kupoteza mchezo wowote huku ikiruhusu pia mabao machache ambapo imefungwa mabao sita tu.
‘The Gunners’ iliruhusu mabao manne katika hatua ya ligi na mawili ikifungwa katika hatua ya mtoano kwenye mechi iliyoisha kwa sare ya 1-1 dhidi ya Bayer Leverkusen katika hatua ya 16 bora huku bao lingine iliruhusu kwenye sare ya 1-1 dhidi ya Atletico Madrid yote ikifungwa ugenini.
Arsenal imeibuka na ushindi katika michezo 11 na kutoka sare mara tatu huku ikifumania nyavu za wapinzani mara 29 na kufanikiwa kuondoka bila kuruhusu bao ‘Cleen sheets’ katika michezo tisa ambayo lango la David Raya lilibaki salama.
Washika Mitutu hao wa London sasa wanamsubili mshindi watakaecheza naye fainali kati ya Bayern Munich au Paris Saint-Germain (PSG) ambao watavaana usiku wa leo huko jijini Munich, Ujerumani.