Watano Simba kula panga

VIGOGO wa Simba kama watafanikiwa kupata mashine mpya nne za kigeni wanazozihitaji ili kuongeza makali ya kikosi hicho, kuna wachezaji wasiopungua watano huenda wakaonyeshwa mlango wa kutokea kwenye dirisha dogo la usajili litakalofunguliwa Desemba 15.

Nyota wanaoweza kupigwa panga yupo, Nelson Okwa aliyerejea nchini jana akitokea kwao Nigeria kwa ajili ya matibabu ya nyama za nyuma ya paja alizoumia mazoezini siku moja kabla ya mechi dhidi ya Azam ambayo Simba ilipoteza.

Okwa ambaye alikuwa staa mkubwa nchini Nigeria, tangu amejiunga na Simba mzunguko wa kwanza unamalizika amecheza mechi chache akitokea benchini na hajapata nafasi ya kuanza kwenye mchezo wowote, huku kiwango chake kinaonekana kuwa tofauti na alipokuwa Rivers United msimu uliopita hadi kuwavutia vigogo wa Simba na kumsajili.

Victor Akpan chini ya kocha, Zoran Maki alikuwa hapati nafasi ya kucheza katikati ya mzunguko wa kwanza alikutana na majeraha na hata aliporejea chini ya kocha, Juma Mgunda bado amekuwa na wakati mgumu wa kucheza kwenye nafasi ya kiungo.

Kuna taarifa za uhakika uongozi wa Dodoma Jiji imeonyesha nia ya kuhitaji huduma Akpan hata kwa mkopo huku taarifa nyingine zikisema Coastal Union wanataka kumrudisha.

Kwenye eneo la kiungo Simba wanaocheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza ni Mzamiru Yassin na Sadio Kanoute na akikosekana mmoja wao chaguo la pili anakuwa, Jonas Mkude huku Akpan akiwa chaguo la nne.

Beki wa kati, Mohamed Ouattara mwanzoni mwa msimu wakati kocha, Zoran yupo alikuwa akipewa nafasi kikosi cha kwanza huku Joash Onyango akikaa benchi ila tangu kuondoka amekuwa mchezaji wa kuishia benchi muda mwingine anaingia dakika chache kabla ya mechi kuisha, huku Onyango akirudi kikosini. Ouattara amekuwa beki chaguo la nne kwani chaguo la kwanza Onyango na Hennock Inonga na Kennedy Juma.

Ukiachana na nyota hao wa kigeni kuna wazawa watatu hawapo kwenye wakati mzuri na si suala la kushangaza kusikia panga la kuwakata limewapitia nahodha, John Bocco anayesomea ukocha kwa sasa, Erasto Nyoni na Jimsony Mwanuke.

Bocco kuna vigogo wenye nguvu ndani ya Simba wamegawanyika kuna wanahitaji waachane naye sasa hivi ila kuna wengine wanataka abaki hadi mwisho wa msimu kutokana na kuitumikia timu hiyo vizuri na moyo wote tangu ilipomsajili kutokea Azam pamoja na kasi ya kufunga aliyokuwa nayo sasa ambapo kwenye ligi tayari ana mabao manne. Nyoni kushindwa kucheza mara kwa mara na kuishia benchi au kuingia dakika chache kwenye michezo michache huenda panga likampitia kama ilivyo Mwanuke anayesumbuliwa na majeraha.