Unataka pointi cheza Jang’ombe Boys

Muktasari:
- Ligi Kuu Zanzibar Kanda ya Unguja imezidi kushika kasi katika viwanja mbalimbali
Jang’ombe Boys imeendelea kugawa pointi baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Kilimani City katika muendelezo wa Ligi Kuu Zanzibar Kanda ya Unguja.
Katika mchezo huo wa mzunguko wa nne wa ligi hiyo ulipigwa kwenye Uwanja wa Amaan Mjini hapa, mshambuliaji wa Kilimani City, Baraka Mashango alifunga bao pekee dakika 19 na kuwaacha mashabiki Jang’ombe Boys wakiondoka uwanjani hapo kama wamewagiwa maji ya baridi.
Baada ya bao hilo Kilimani City ilijipanga vema katika safu ya ulinzi kwa kutoruhusu hata mpira wa bahati mbaya kuwapenya, huku wakishambulia kwa kushtukizia tu.
Hali hiyo iliwafanya Jang’ombe kushindwa kulikabili lango la wapinzani wao hadi kipenyenga cha mwisho kinapulizwa cha kukamilika kwa mtanange huo.
Matokeo hayo yanaifanya Jang’ombe Boys kushikilia nafasi yake ya tatu kutoka mwisho ikiwa na poiti mbili kwa kutoka sare michezo miwili na kufungwa miwili ikizipita timu ya Miembeni City yenye pointi moja pamoja na timu ya Charawe inayoshikilia mkia wa ligi hiyo.