Polisi yamshikilia Ally Kamwe kisa kauli chafu kwa viongozi

Jeshi la Polisi mkoani Tabora linamshikilia Ofisa Habari wa Klabu ya Yanga, Ali Kamwe.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Aprili 3,2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amethibitisha jeshi hilo kumshikilia Kamwe huku akitaja sababu kuwa ni kauli chafu kwa viongozi wa Serikali.
“Ndio tunamshikilia Ally Kamwe na tunaendelea na mahojiano na taratibu nyingine zitaendelea kwa mujibu wa sheria,"amesema Abwao.
Kamwe anashikiliwa ikiwa ni siku mbili zipite tangu arushe dongo kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha katika hamasa kuelekea mchezo wao dhidi ya Tabora United uliomalizika jana Aprili 2, 2025 kwa Yanga kushinda bao 3-0.
Katika video inayosambaa mitandaoni inamuonyesha Kamwe akiwa mkoani Tabora akifanya hamasa ya mchezo huo huku akisema: “Kuna watu wanatafuta kiki..mkuu wa mkoa nani huyu, Chacha eenh? Atachacha kweli baada ya mechi,”
Chanzo cha Kamwe kusema hivyo ni kutokana na mkuu wa mkoa kuahidi Tabora United endapo itamfunga Yanga itapewa bonansi ya Sh60 milioni huku pia akishutumu watu wa Yanga kuwatumia meseji za rushwa wachezaji wa Tabora.