Wiki ya Maji ilete ahueni kwa wananchi

Maji yakitiririka katika kilele cha Kihansi
Muktasari:
Ni wiki ambayo taasisi mbalimbali za sekta za maji zinafanya maonyesho ya kujivunia mafanikio yao. Lakini wananchi ambao ndiyo walengwa wa huduma hiyo wana maswali mengi hasa kuhusu wiki yenyewe.
Jumatatu ni mwanzo wa Wiki ya Maji, ambayo kwa mwaka huu ujumbe wake ni ‘Maji na Maendeleo Endelevu’. Ni wiki ya kusikia mafanikio na changamoto za sekta ya maji nchini.
Ni wiki ambayo taasisi mbalimbali za sekta za maji zinafanya maonyesho ya kujivunia mafanikio yao. Lakini wananchi ambao ndiyo walengwa wa huduma hiyo wana maswali mengi hasa kuhusu wiki yenyewe.
Kuna wanaouliza Wiki ya Maji inamnufaisha nini mwananchi? Sote ni mashahidi maadhimisho ya Wiki ya Maji yamekuwa yakiambatana na maonyesho ya vifaa vilevile na maelezo yaleyale, kuhusu huduma hiyo. Hakuna jipya.
Wiki iliyopita lilitokea tukio kwenye mkutano wa hadhara huko Mpwapwa mkoani Dodoma, ambapo mkurugenzi wa mamlaka ya maji katika mji huo alimkabidhi Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, nyaraka za wadaiwa sugu wa maji, zikiwamo taasisi za serikali, kampuni binafsi na benki.
Kinana alikabidhiwa nyaraka hizo baada ya kutokea malalamiko ya wananchi katika mkutano huo wakimueleza kuwa maji hayatoki, lakini kila mwezi wanadaiwa bili ya maji jambo ambalo limekuwa kero kubwa kwao.
Suala la Mpwapwa ni ushahidi wa maeneo mengi ya nchi ambako wananchi hawapati huduma ya maji, lakini wananchi wamekuwa wakipelekewa ankara za madai kila mwezi.
Sisi sote ni mashahidi kwamba kila mwaka kwenye maadhimisho ya Wiki ya Maji, wananchi wanaofika kwenye maadhimisho hayo hutoa kilio chao cha uhaba wa maji na kudaiwa malipo kwa huduma ambayo hawakuipata, lakini suluhisho la tatizo hilo limekuwa gumu kupatikana.
Pia imekuwa ni ada kwa watoa huduma wa sekta ya maji, hasa wizara ya maji, nao kulia kwamba wizi wa maji na uharibifu wa miundombinu vimekithiri.
Maadhimisho ya Wiki ya Maji yamekuwa ni kipindi cha kila mtu kutoa kilio chake, wananchi wanalia maji hakuna, huku wadau wa sekta ya maji nao wakilia kukithiri kwa wizi.
Kwa mfano Jiji la Dar es Salaam, Dawasco wamekijita zaidi katika biashara ya maji kwa wauzaji wa kwenye magari kuliko wananchi wa kawaida.
Dawasco wanauza maji zaidi kwa wenye magari ambao huwa na madumu yenye uwezo wa kubeba lita 1,000 kila moja. Pia bei ya dumu moja la lita 1,000 ni Sh17,000, wakati kuna taarifa kwamba Dawasco dumu hilo huliuza kwa wenye magari kwa bei nafuu sana, isiyofika hata Sh5,000.
Pia, ushahidi wa kero ya maji ni wakati muswada wa makadirio ya matumizi ya Wizara ya Maji wa Mwaka wa Fedha wa 1013/14 ulipokwama bungeni, baada ya wabunge kuchachamaa wakitaka majibu sahihi kuhusiana na kero ya uhaba wa maji nchini.
Pamoja na ukweli kwamba Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) ndilo lililopitisha Azimio Namba 47/193, mwaka 1992, likipendekeza kuwa Machi 22 ya kila mwaka iwe Siku ya Maji Duniani, sisi tunaona kuna haja siku hii ikawa na inakuja na majibu ya namna walivyoshughulikia hoja za wananchi, na hoja kuu ni upatikanaji wa uhakika majisafi na salama.
Tunaamini kuadhimisha siku hii huku wananchi wakiendelea kutaabika kwa kukosa maji ni kama kejeli kwao. Tunaziomba mamlaka husika kulishughulikia kwa dhati tatizo la maji kwa sababu maji ni uhai.