Siku ya wanawake duniani iendane na mikakati

Muktasari:
Siku ya Wanawake duniani ina historia ndefu ambayo kimsingi lengo lake ni kuonyesha mapambano ya wanawake dhidi ya hali ngumu sehemu za kazi na dhidi ya mifumo kandamizi.
Siku ya Wanawake duniani ina historia ndefu ambayo kimsingi lengo lake ni kuonyesha mapambano ya wanawake dhidi ya hali ngumu sehemu za kazi na dhidi ya mifumo kandamizi.
Ni siku ambayo wanawake duniani huangalia changamoto zinazowakabili katika nyanja za kijamii, kiuchumi na kisiasa na kujaribu kuziwekea mikakati ya kukabiliana nazo. Kwa upande mwingine ni siku ya kuangalia mafanikio na michango ya wanawake mbalimbali duniani.
Kwa mara ya kwanza siku hiyo iliadhimishwa Machi 19 nchini Australia, Denmark, Ujerumani na Uswisi ambako wanawake na wanaume zaidi ya milioni moja walishiriki katika maandamano wakidai haki ya kufanya kazi bila ubaguzi na haki ya kupiga kura. Mwaka 1913-1914 siku ya wanawake duniani ilitumika kama jukwaa la kupinga Vita ya Kwanza ya Dunia kwa sababu pamoja na kuwa wanaoingia katika medani ya vita aghlabu ni wanaume, lakini wanaoathirika na vita ni wanawake na watoto.
Kuanzia wakati huo siku ya wanawake duniani imekuwa ikiadhimishwa kwa dhamira maalumu, aidha kupinga kitu au kushajiisha mabadiliko katika nyanja za uongozi, uchumi na kijamiii.
Mwaka huu shajiisho liko katika kuwapa wanawake nafasi katika ngazi ya uamuzi, ‘50 kwa 50 ifikapo 2030, jitihada ziongezwe.’ Hiyo ni kaulimbiu endelevu kwa maana ya kuwa haiishii mwaka huu ila jitihada zinatakiwa ziongezwe katika kila nyanja ili ifikapo mwaka 2030, azimio hilo liwe limeingizwa katika utekelezaji kwa maana ya kuwa mwanamke aonekane katika nafasi zote za uongozi kuanzia ngazi za chini tena kwa asilimia hamsini.
Miaka 20 imepita tangu nchi 189 wanachama wa Umoja wa Mataifa zilipopitisha azimio la Beijing katika mkutano wa nne wa wanawake uliofanyika 1995, azimio ambalo lilisisitiza usawa wa kijinsia, kuwaongezea wanawake uwezo na kuzingatia haki za binadamu.
Licha ya hatua kubwa zilizopigwa kuhusu usawa na kuwaongezea uwezo wanawake, Afrika bado ina safari ndefu, hivyo inabidi Serikali za nchi za Afrika zifanye jitihada ya nyongeza kuhakikisha kuwa uwiano wa usawa wa kijinsia unapatikana. Bila shaka hilo halihitaji nguvu kubwa bali utashi tu wa kisiasa.
Ili kulifikia lengo hilo ni lazima mikakati ianzie ngazi za chini katika jamii, ambako watoto wa kike watapewa nafasi ya kujifunza na kushiriki katika masuala mbalimbali ya kijamii sawa na wanaume.
Vilevile lipo tatizo la mila na desturi zinazomweka mwanamke katika nafasi ya pili na pia kutoshirikishwa katika ngazi ya kutoa uamuzi, huu ni mkakati unaopaswa ufanyiwe kazi taratibu, tena kwa muda mrefu kwani kubadili mila na desturi hakutahitaji sera tu bali utashi wa jamii husika.
Ingawa Tanzania ilishafikia asilimia 30 ya wanawake katika ngazi za uamuzi katika Serikali na Bunge, baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 idadi ya wanawake katika ngazi hizo ilishuka kidogo. Hata hivyo kwa mara ya kwanza Tanzania imepata Makamu wa Rais mwanamke, hilo ni jambo la kupongezwa.
Tungependa kuona idadi ya wanawake katika ngazi ya uamuzi inaongezeka si kwa ajili ya kupendelewa bali kwa sababu ya uwezo wao, hivyo suala la kujengewa uwezo nalo linapaswa kuingizwa katika mikakati inayopangwa kuhakikisha kuwa azimio la 50 kwa 50 linafikiwa.