Makosa katika magazeti
Muktasari:
“ Mfungaji bora msimu huu ni majanga.” Ni aibu kuandika kama ilivyoandikwa kama kichwa cha habari kwani ni muundo unaotokana na mazungumzo lakini haukubaliki katika kutumika katika uandishi
Katika magazeti ya Kiswahili ya hapa nchini, makosa ninayopambana nayo ni mawili. Kwanza ni katika uandishi wa vichwa vya habari. Pili, ni katika taarifa au maelezo yanayofuatia vichwa hivyo cha habari. Kwa hakika kosa katika vichwa vya habari ni kubwa zaidi kuliko maelezo yanayotolewa kwenye taarifa inayozumnumzia. Nitatoa mifano miwili. Mfano wa kwanza ni sentensi unaofuata:
“ Mfungaji bora msimu huu ni majanga.” Ni aibu kuandika kama ilivyoandikwa kama kichwa cha habari kwani ni muundo unaotokana na mazungumzo lakini haukubaliki katika kutumika katika uandishi. Ingekuwa bora kama angeandika, “Mfungaji bora msimu huu ni kasheshe kwa maana ya hali ya kutoelewana. Kama mwandishi angekuwa makini, tatizo hili halingetokea.
Mfano wa pili ni:
“Sumaye abeza mfumo uliopo” Taarifa hii ni tata kwa sababu hatujui ni mfumo gani unaoongelewa. Maelezo kamili yanapatikkana baada ya kusoma maelezo. Kwa ufafanuzi angeandika kwa kuweka maneno ‘elimu nchini’. Kwa hiyo kichwa cha habari kisomeke,
“Sumaye abeza mfumo wa elimu uliopo.”
Mifano iko mingi lakini hii miwili inatosha udhaifu uliopo kwa waandishi wetu.
Katika kuchambua makosa katika taarifa zinazotolewa baada ya kichwa cha habari kuandikwa, yafuatayo yamegundulika:
“ Walizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wanachama waliomba majina yao yasitajwe.” Hapa suala lililopo ni matumizi ya vituo katika uandishi. Vituo hivi ni kama nukta, alama ya mkato, ya kuuliza, nukta pacha, nukta na mkato, alama ya kushangaa, alama za mnukuo, n.k. Katika sentensi iliyoandikwa hapo juu, kituo cha mkato kimeachwa. Alama ya mkato ilitakiwa kuwekwa baada ya neno tofauti. Kituo cha mkato kinafanya maana ya sentensi ifahamike vizuri. Hii ni dhahiri kuwa mafunzo wanayopata wanachuo katika vyuo vya uandishi wa habari kuhusu uandishi bora una walakini. Kwa kuwa haupo mwongozo kuhusu uandishi bora hali inayowafanya waandishi kubabaika wanapoandika. Hata hivyo mwongozo wa mbinu bora za uandishi uko mbioni kuchapishwa na utakuwa ni mkombozi kwa waandishi walio kazini na wale wanaosoma vyuoni. Inatarajiwa kuwa mwongozo huu utaondoa au kupunguza kabisa makosa yoyote ya kisarufi nay a kifasihi katika magazeti yetu.
Mwandishi anatakiwa aandike sentensi zinazoeleweka. Hivyo alitakiwa kuandika, “ Walizungumza kwa nyakati tofauti na baadhi ya wanachama waliomba majina yao yasitajwe.”
Suala jingine ni kuwataka waandishi kutumia sentensi fupi. Nimegundua kwa sentensi katika gazeti moja ina maneno mengi jambo ambalo linafanya sentensi iwe ndefu na isieleweke.
Mfano ufuatao uko wazi. Kwa mfano:
“ Pinda alitoa kauli hiyo juzi katika maadhimisho ya ‘Wiki ya Maji’ kitaifa yanayofanyika katika Mkoa wa Mara wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nyabehu wilayani Bunda mkoani hapa baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi huo ambao unatekelezwa na Serikali.”
Inashauriwa kuwa kituo cha nukta kingewekwa baada ya neno Mara. Ili kubadilisha muundo wa sentensi tunaondoa neno ‘wakati’ na kuanza na neno ‘Alikuwa’ akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nyabehu wilayani Bunda.
Suala jingine ni kuchanganya neno kupokelewa na kupokewa. Hili ni kosa. Kupokewa ni kulaki au kupata kitu kutoka kwa mtu mwingine. Kupokelewa ni kupokea kwa niaba ya mtu mwingine. Kwa mfano: Kaka alinipokelea cheti changu nilipokuwa naumwa. Kwa hiyo kwa usahihi ingekuwa ‘…walipokewa na wenyeji wao…’
Pia liko tatizo la kutumia neno ‘polisi.’ Neno hili liondolewe.
Kwa hiyo sentensi isomeke,
“Alisema wahamiaji hao haramu walipokewa na mwenyeji wao huyo ambaye ni mwinjilisti na kuwahifadhi jikoni …”
“ Kaimu Meneja wa Kampuni (Gasco) Kapulya Musomba alisema shirika limepanga kutoa motisha kwa wananchi katika maeneo yaliyopita mradi huu wa gesi.”
Siyo sahihi kutumia neno Gasco na kuliwekea mabano. Ilitakiwa kuandika kwa urefu jina la kampuni hiyo na baadaye kulitumia neno Gasco kwenye mabano.