Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kitafutwe kiini cha mauaji haya Zanzibar

IGP Said Mwema

Muktasari:

Makamu wa Askofu wa kanisa hilo Zanzibar, John Mfoi alisema watu waliompiga risasi padri huyo walikuwa kwenye pikipiki aina ya Vespa na walikuwa wakimfuatilia nyuma wakati akielekea kanisani

MATUKIO kadhaa ya kutisha ambayo yametokea visiwani Zanzibar katika siku za hivi karibuni hakika yameacha maswali mengi na kuibua mashaka kama kweli visiwa hivyo vinatawalika.

Pamoja na kutokea vurugu za kidini na kisiasa ambazo zilisababisha vifo, umwagaji damu na uharibifu mkubwa wa mali, sasa tunashuhudia mauaji yanayowalenga viongozi wa madhehebu ya dini.


Juzi asubuhi padri wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Minara Miwili iliyoko Mji Mkongwe, Evaristus Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana wakati alipokuwa akienda kuendesha ibada ya Jumapili katika Kanisa la Mtoni, Mkoa wa Mjini Magharibi, nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.


Makamu wa Askofu wa kanisa hilo Zanzibar, John Mfoi alisema watu waliompiga risasi padri huyo walikuwa kwenye pikipiki aina ya Vespa na walikuwa wakimfuatilia nyuma wakati akielekea kanisani. Alisema wakati padri huyo alipokuwa akitaka kuegesha gari lake baada ya kufika kanisani hapo, watu hao walimfyatulia risasi na kutokomea kusikojulikana.


Ikumbukwe kwamba hilo ni tukio la pili ndani ya miezi miwili visiwani humo, ambapo Desemba 26 mwaka jana, Padri Ambrose Mkenda wa Kanisa Katoliki mjini Zanzibar alipigwa risasi na kujeruhiwa vibaya na watu wasiojulikana nje ya nyumba yake wakati akitokea kanisani.

Mapadri hao wawili wanatokea Tanzania Bara, lakini wamekuwa visiwani humo kwa muda sasa kama kituo chao cha kazi, chini ya Kanisa Katoliki, Dayosisi ya Zanzibar.


Kama tulivyosema hapo juu, matukio hayo ya kutisha yameacha maswali mengi yasiyokuwa na majibu. Wengi wamehusisha matukio hayo na sababu za kidini na kisiasa, huku wengine wakiyahusisha moja kwa moja na kikundi kinachopinga Muungano kati ya Zanzibar na Tanzania Bara.


Ni vigumu kwa sasa kusema kwa uhakika sababu za matukio hayo ya kutisha ambayo bila shaka pia yanaibua maswali kuhusu usalama wa wananchi wenye asili ya Tanzania Bara wanaoishi visiwani humo, wakiwamo viongozi wa dini.

Tunasema hivyo kutokana na ushuhuda uliotolewa jana mjini Zanzibar na kiongozi wa kanisa hilo visiwani humo, Askofu Augustino Shao, kwamba marehemu padri huyo alikuwa akipokea vitisho vingi kutoka kwa watu wasiojulikana, wakimtishia maisha iwapo asingeondoka Zanzibar na kurudi Bara.


Kiongozi huyo alisema mara kadhaa kanisa lake lilipeleka taarifa za vitisho hivyo kwa Jeshi la Polisi, Ikulu za Zanzibar na Dar es Salaam, kwa maana ya Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete na kwamba taarifa hizo hazikufanyiwa kazi.

Ndugu wa marehemu walioko mkoani Kilimanjaro pia walithibitisha katika mahojiano maalumu na gazeti hili jana kwamba walikuwa na taarifa za vitisho kwa ndugu yao huyo kutoka kwa watu waliomtaka aondoke visiwani humo, vinginevyo maisha yake yangekuwa hatarini.


Baada ya mauaji ya padri huyo sasa ghafla tunaona pilikapilika za Serikali na Jeshi la Polisi zikianza kufanyika na tunaambiwa Rais Kikwete mwenyewe ameagiza waliohusika katika mauaji hayo wasakwe kwa gharama yoyote na kupelekwa mbele ya sheria.


Sisi tumefadhaishwa na hatua hiyo ya zimamoto ya Serikali, kwani iwapo taarifa za vitisho kwa padri huyo zingefanyiwa kazi mapema, maisha yake yasingeangamia.

Pamoja na kuzitaka serikali zote mbili ziwajibike kwa tukio hilo, tunazitaka pia zichukue hatua kuhakikisha usalama wa wananchi wote wenye asili ya Tanzania Bara wanaoishi visiwani humo, kwani wengi wao wamekuwa hawana uhakika na usalama wao na mali zao.