Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanachama NHIF tumieni kadi kwa usahihi

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kupitia mifumo yake ya ndani umekamata kadi 1,346 ambazo zimekuwa zikitumiwa na wasio wanachama wala wanufaika wa mfuko huo.

NHIF ilibaini hilo baada ya kufanya uhakiki kuanzia Juni 1 mwaka huu katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Arusha, Kilimanjaro na Dodoma.

Mfuko huo unapaswa kupongezwa kwa jitihada hizo zilizowezesha kulibaini hilo, ambalo bila shaka lilikuwa linachangia kwa kiasi fulani kusuasua kwa utendaji wa mfuko huo.

Kadi 1,346 kutumiwa na watu wasiokuwa wanachama ni zaidi ya hasara, kwani haijulikani walifanya hivyo kwa muda gani, inawezekana walianza zamani lakini wamebainika sasa, hivyo kuwa sehemu ya kuuingizia hasara mfuko huo.

Inawezekana hata kilichobainishwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kikionyesha hofu ya mfuko huo kufilisika ni kutokana na ujanjaujanja huu unaofanywa na watumiaji wasiokuwa waaminifu, wakisaidiwa na baadhi ya watendaji ama wa mfuko au wa vituo vya kutolea huduma.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya CAG, NHIF ilivilipa vituo vya afya madai yasiyo ya kweli kiasi cha Sh14.46 bilioni kwa kipindi cha mwaka 2019/20 hadi 2021/22. Hizi si fedha ndogo, zote hizi kutumika nje ya utaratibu ni hasara kubwa inayoweza kuuyumbisha mfuko huo.

Mbali na kubaini hilo, NHIF haina budi kuwachukulia hatua kali watumishi hao, wakiwemo waliobainishwa na CAG wakidaiwa kujihusisha na vitendo vya udanganyifu.

Miongoni mwa hatua za kuchukua ukiachilia mbali za kinidhamu, ni kuubaini mtandao wao pia, ili kuumaliza kabisa.
Kupitia wao, hatuna shaka watabainika hata ambao walifanikiwa kujificha wakati wa ukaguzi.

Pamoja na hatua zilizoanza kufanyika, NHIF inapaswa kudhibiti hali hii. Inaweza kuja na utaratibu unaofanywa na mifuko mingine ya afya ya kuweka kiwango maalumu cha fedha kwa kila mwanachama, kikiisha analazimika kufuata utaratibu maalumu kuongezewa fedha ili aendelee kupata matibabu.

Faida ya kufanya hivyo ni kuwa kila mwanachama atatumia kadi yake kwa uangalifu kwa kujua akizidisha matumizi itafikia mahali fedha zitakwisha.

Hivyo ataitumia vizuri na peke yake, ikitokea imekwisha kwa matumizi yake halali, hilo litakuwa jambo lingine, lakini haitakuwa rahisi kuigawa ovyo kwa watu wasiohusika.

Wananchi pia wana jukumu la kuulinda mfuko huu kwa sababu ni mahali ambapo wanapata unafuu wa matibabu.

Kila mmoja anayejua faida na thamani ya mfuko awe mlinzi wa mwenzake kwa kuhakikisha kadi moja inatumiwa na mtu mmoja, tena anayetambulika kisheria.

Inajulikana jinsi gharama za matibabu bila bima zilivyo ghali na baadhi ya mifuko ya huduma ya afya ilivyo na gharama kubwa ukilinganisha na NHIF, hivyo kuuhujumu ni kuuchimbia shimo, hilo likitokea anayeathirika ni mwanachama mwenyewe na nduguze.

Wahenga walisema usipoziba ufa, utajenga ukuta, badala ya kusubiri madhara yatokee kwa mfuko kufilisika ni bora kuchukua tahadhari, kwa kuzingatia sheria za matumizi ya kadi hizo na wanachama husika kuchukuliwa hatua kwa vitendo hivyo.

Vilevile elimu zaidi itolewe ili wananchi waulinde mfuko wao kwa kudhibitiana wao kwa wao dhidi ya matumizi yasiyo sahihi ya kadi za bima ya afya.