Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ushiriki wa wabunge kutunga sheria uimarishwe

Muktasari:

  • Katika kufanikisha shughuli hiyo kwa kufuatia utaratibu uliowekwa na sheria, vipo vikwazo kadhaa vya ushiriki wao na kuleta ugumu kwa baadhi ya wabunge kutokana na kuwapo masuala ya kitaalamu zaidi ambayo si wote wenye ujuzi nayo.

Kazi kubwa ya Bunge mbali na kuisimamia na kuishauri Serikali ni kutunga sheria za nchi kwa niaba ya wananchi.

Katika kufanikisha shughuli hiyo kwa kufuatia utaratibu uliowekwa na sheria, vipo vikwazo kadhaa vya ushiriki wao na kuleta ugumu kwa baadhi ya wabunge kutokana na kuwapo masuala ya kitaalamu zaidi ambayo si wote wenye ujuzi nayo.

Kwa miaka kadhaa tunaofuatilia mijadala ya Bunge tumeshuhudia ushiriki wa wabunge wachache hasa wenye ujuzi wa sheria katika kufanya marekebisho ya sheria na miswada mbalimbali inayowasilishwa na Serikali bungeni, hali inayowafanya wananchi kuuona upungufu katika uboreshaji huo.

Baadhi ya wabunge ambao hujitokeza mara nyingi katika miswada ya sheria na kuibua mapendekezo mazito ni Andrew Chenge (Bariadi), William Ngeleja (Sengerema), George Simbachawene (Kibakwe), Tundu Lissu (Iramba Mashariki) na Ali Salehe (Mji Mkongwe).

Hali hii imekuwa inafanya michango ya miswada ya sheria inapowasilishwa bungeni mara nyingi huwa na wachangiaji walewale ambao wamezoeleka hasa wale wenye ubobezi wao huko katika sheria.

Wabunge hawa wamekuwa wakiona upungufu mwingi na kupendekeza mabadiliko, na jinsi vifungu hivyo vinavyotakiwa kuandikwa ili kuwezesha sheria kuwa bora zaidi.

Pengini ili kuwa na wabunge wengi wanaoshiriki kwa ufanisi kimichango katika uboreshaji wa miswada mbalimbali ya kisheria, ungeweza kuongeza ubora wa sheria zetu kwa kiasi kikubwa.

Ipo haja sasa Bunge kufikiria namna ya kuwasaidia wabunge katika kutimiza majukumu yao hayo ya kutunga sheria ili kuongeza ushiriki wao kwa kiasi kikubwa katika utungaji wa sheria mbalimbali kwa manufaa ya Taifa.

Mara nyingi Spika au viongozi wengine wanaoongoza Bunge wamekuwa wakiwataka wabunge pia kutumia fursa ya kikanuni ambayo inawapa mwanya kuwasilisha miswada ya marekebisho ya sheria mbalimbali ambazo wanaziona zina upungufu.

Kanuni ya 81 ya Bunge inasema bila ya kuathiri masharti ya Ibara ya 99 ya Katiba, kamati yoyote ya kudumu ya Bunge au mbunge yeyote anaweza kuwasilisha bungeni muswada binafsi wa sheria.

Kanuni hiyo inasema taarifa ya kuwasilisha muswada binafsi wa sheria na muswada wa sheria wa kamati itapelekwa kwa katibu na taarifa hiyo itaeleza jina la muswada unaopendekezwa pamoja na madhumuni na sababu zake.

Kanuni hiyo inasema mara baada ya muswada huo kupita katika taratibu zote za kikanuni, masharti ya kujadili hoja hii yatakuwa kama yalivyo kwa upande wa miswada ya sheria ya Serikali.

Pamoja na kuwapo fursa hiyo, wabunge hawajaitumia ipasavyo, hivyo wamebaki wakibariki miswada ya Serikali.

Hata hivyo, wapo wabunge akiwemo John Mnyika (Kibamba), Zitto Kabwe (Kigoma Mjini), Juma Nkamia (Chemba) na John Heche (Tarime Vijiji) ambao waliwahi kuonyesha nia ya kupeleka miswada binafsi ya sheria bungeni, lakini haijawahi kufikia hatua ya kujadiliwa na Bunge

Kutokana na hali hiyo mara zote marekebisho ya sheria yamebaki kuwasilishwa tu na Serikali huku wabunge wakihusika katika uboreshaji wake wa vifungu wanavyoona vina upungufu kabla ya kupitisha kwa wingi wa kura.

Hali hii ya kushindwa kuwasilisha miswada binafsi bungeni imewafanya wabunge wengi kutotimiza yale wanayoyapigania ndani ya Bunge kwa miaka mingi kwa sababu ya kutegemea upande mwingine uwasilishe miswada bungeni.

Mfano ni Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ambayo imekuwa ikilalamikiwa kwa miaka mingi bungeni na nje ya Bunge kuwa inapingana na Sheria ya Mtoto. Upo uwezekano kuwa muda wa kuchangia pia unaweza kuwa ni kikwazo kwa wabunge wengi kupata fursa hiyo ya kuchangia katika uboreshaji wa miswada hiyo ya sheria.

Hapo ndipo umuhimu wa kutatua changamoto hizo unapohitajika ili kusaidia katika kuwawezesha wabunge kuongeza ushiriki katika kutunga au kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali.

Njia mojawapo ni kuwapa mafunzo maalumu ambayo yatawaongeza uelewa katika kutambua upungufu uliopo katika utungaji wa sheria ikiwemo kufanya marekebisho katika sheria.

Pia kuwepo kwa namna ya kuwapata wanasheria kwa ajili ya kuwasaidia katika kuboresha michango yao katika utunzi wa sheria, jambo ambalo litasaidia kupanua wigo wa idadi ya wabunge wanaoshiriki kikamilifu katika kazi hiyo muhimu.

Hayo yote ni vyema yafanyike ili kuwasaidia wabunge katika kuhakikisha ushiriki wao kwenye utekelezaji wa majukumu kuwa bora zaidi, hasa katika utunzi wa sheria.