Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UCHAMBUZI WA MJEMA: Kama ni mgombea, usizidishe idadi hii ya timu ya kampeni

Naamini wengi wetu tunafahamu kampeni za Uchaguzi Mkuu 2025 kwa Tanzania Bara zitaanza Agosti 28 na kufikia tamati Oktoba 28, 2025, lakini unafahamu kuwa kuna idadi mahususi iliyowekwa na sheria ya timu za kampeni za wagombea?

Ninafahamu unaanza kujiuliza, mbona katika kampeni iwe kwa kiti cha Rais, ubunge na udiwani tunashuhudia misafara mirefu ya magari na watu kama kweli kuna udhibiti, basi ni muhimu sana ukapitia makala hii kujua idadi ya kisheria.

Tafsiri ya timu ya kampeni ni kwamba ni kikundi cha watu wanaofanya kazi pamoja ili kuunga mkono kampeni ya mgombea au chama cha siasa, kinachoshiriki uchaguzi kama ilivyo sasa vyama 18 vya siasa vinashiriki uchaguzi mkuu.

Jukumu lao kuu ni kumsaidia mgombea kushinda uchaguzi kwa kuimarisha jukwaa lake, kushirikiana na wapiga kura na kutekeleza mkakati wa kampeni ikiwamo kuhakikisha hotuba zake na sera zinasaidia wapiga kura kufanya maamuzi sahihi.

Sasa Tanzania tuna Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 toleo la 2015 na Kanuni zake za mwaka 2010 kama zilivyofanyiwa marejeo Julai mwaka 2025 ambazo zimeweka ukomo wa idadi kwa mgombea urais, ubunge na udiwani.

Kulingana na kifungu cha 17(1) (a) hadi (c), idadi ya timu ya kampeni kwa mgombea urais haipaswi kuzidi watu 50, kwa mgombea ubunge haipaswi kuzidi watu 20 wakati kwa mgombea udiwani, timu hiyo haipaswi kuzidi watu 10.

Kifungu kidogo cha (2) kinataka mgombea awasilishe ombi kwa Msajili wa Vyama vya Siasa akiainisha majina ya timu yake ya kampeni siku mbili kabla ya kuanza kwa mchakato wa uteuzi au siku saba baada ya siku ya uteuzi wa wagombea.

Kumbuka uteuzi wa wagombea sio ule unaofanywa na chama cha siasa, la hasha, bali ni ule utakaofanywa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Kulingana na sheria hii, iwapo mgombea urais anataka kubadili timu yake ya kampeni atamjulisha Msajili wa vyama vya siasa, na kwa ubunge atamjulisha mkurugenzi wa halmashauri na kwa diwani, atamjulisha ofisa mtendaji wa kata.

Ni muhimu sana tukatofautisha kati ya timu ya kampeni ya mgombea na wanachama, wapambe, mashabiki na wafuasi ambao wanaamua kuandamana naye wakitumia muda wao, gharama zao na bila kulipwa hata senti tano.

Katika timu ya kampeni kunakuwa na meneja wa kampeni anayekuwa mkuu wa operesheni zote za kampeni, kufanya maamuzi ya mikakati na kusimamia rasilimali zinazotumika katika kampeni za mgombea ikiwamo helikopta, magari na pikipiki.

Mbali na meneja kampeni, lakini katika timu hiyo anaweza kuwapo mkurugenzi wa mawasiliano anayesimamia habari na mahusiano ya vyombo vya habari na kunakuwepo na mshauri wa sera anayesimamia sera ya mgombea wake.

Kunaweza kuwa na mratibu wa kutafuta watu wa kujitolea, kunakuwepo na timu ya harambee kwa ajili ya kutafuta fedha za kampeni, kunakuwa na timu ya kidigitali (digital team), mwandishi wa hotuba na anayesimamia shughuli za za matukio na mikutano yote.

Katika timu hiyo ya kampeni, inaweza kujumuisha pia watafiti ambao jukumu lao ni kutafuta data na kufanya tafiti ili mgombea azitumie kuhabarisha umma na pia timu ya mitandao (social media) kusimamia maudhui na kuibua mijadala.

Timu ya kampeni hugharamiwa na chama au mgombea kuanzia chakula, vinywaji, usafiri na posho zao za siku na gharama hizi zitahesabika kama gharama za uchaguzi kulingana na kifungu cha 7(2) cha sheria ya uchaguzi 2010 toleo la 2015.

Nchi yetu inaongozwa kwa utawala wa sheria na kila mmoja anawajibika kuwa chini ya sheria hivyo ni wajibu wa kila mgombea kutenganisha kati ya timu ya kampeni ambayo inasimamiwa na sheria na wapambe ambao hujitolea.

Utawala wa sheria ni nini? Kwa lugha ya kawaida kabisa, utawala wa sheria ni kwamba hakuna mtu aliye juu ya sheria, kuanzia Rais wa nchi, Dola ya nchi, kaya, kila taasisi na kila mtu anawajibika kwa sheria, hivyo wagombea wafungue macho.

Ni muhimu sana orodha ya timu ya kampeni ikawa wazi kwa mamlaka ili pale itakapohitajika kutoa mchanganuo wa matumizi, wawe wanajulikana.

Hii inasaidia pia kumuepusha mgombea na kuonekana anagawa rushwa au hongo pale ambapo atakuwa anailipa timu yake malipo stahiki kwa sababu endapo mgombea atabainika kuvunja kanuni hizi, anaweza kuondolewa kugombea.

Kwa hiyo katika kampeni hizo zinazotarajia kuanza Agosti 28,2025 ni wazi tunaweza kushuhudia misafara mirefu ya magari hasa kwa mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu, lakini tusichukulie wote hao wapo kwenye timu ya kampeni.

Ninasema hivyo kwa sababu, kwa mazingira ya kukua kwa Tekinolojia ya Habari (ICT) na ujio wa mitandao ya Kijamii, mtu anaweza kurekodi picha au video na kurusha mitandaoni akihoji ukubwa wa timu ya kampeni kumbe ni wapambe tu.

Ieleweke kuwa mashabiki na wapambe sio sehemu ya timu ya kampeni bali hao wanafanya hayo kwa mapenzi waliyonayo kwa mgombea au chama hivyo sio kila gari litakalokuwa kwenye msafara, basi lihesabiwe ni rasilimali ya kampeni.

Timu ya kampeni ni lazima itolewe na ijulikane na mamlaka, ndio sheria inavyotaka na tusifanye mambo kimazoea, tuheshimu Sheria ya Gharama za Uchaguzi 2010 toleo la 2015 na kanuni zake, tuepuke kufanya mambo kiholela.

0656600900