Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UCHAMBUZI WA MJEMA: Bodi ya Ithibati iiheshimishe Taaluma ya Habari

Kesho Machi 3, tutashuhudia tukio muhimu la kuzinduliwa kwa Bodi ya Ithibati ya Wanahabari, lakini kuzinduliwa ni jambo moja, na kutekeleza majukumu yake na kufanya uandishi wa habari kuwa taaluma inayoheshimika ni jambo lingine.

Bodi hii ambayo iko chini ya mwenyekiti wake Tido Mhando, na wajumbe Tobias Makoba,Kingoba Bakari, Dk Rose Mchomvu, Dk Egbert Mkoko na Ladislaus Komanya, inazinduliwa na Waziri mwenye dhamana, Profesa Palamagamba Kabudi.

Uteuzi wa bodi hii unafanywa na Waziri kupitia kifungu cha 12 cha sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 na kuanzia vifungu vidogo vya (a) hadi (g) vimetaja nani watakuwa na sifa ya kuteuliwa kuwa wajumbe wa Bodi.


Bodi hii inaanzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 11 cha Sheria ya Huduma za Habari (Media Services Act) ya mwaka 2016 na imepewa majukumu manane, likiwamo la kutoa vitambulisho (press cards) kwa mujibu wa sheria hii.

Kazi nyingine za Bodi hii ni kutekeleza kanuni za maadili kwa wanahabari ambao ni wana taaluma, kuzingatia viwango vya maadili ya kitaaluma na kukuza viwango bora vya maadili na nidhamu miongoni mwa wanahabari nchini.

Pia imepewa jukumu la kuishauri Serikali juu ya masuala yanayohusu elimu na mafunzo kwa wanahabari na kwa kushauriana na taasisi za elimu, Bodi itaweka vigezo na masharti ya mafunzo ya taaluma ya Habari.

Halikadhalika, kuandaa mafunzo kwa wanahabari kwa kushirikiana na Baraza la Habari na kutunza orodha ya wanahabari waliothibitishwa na bodi kuwa wana sifa ya kuitwa wanataaluma ya Habari.

Taaluma ni nini, taaluma ni kazi inayohitaji maarifa maalum (specialized training), ujuzi na mafunzo na kwa kawaida hutawaliwa na maadili na kanuni za maadili na ni lazima kuwepo na bodi ya ithibati ya kutambua nani ni mwanahabari.

Ni lazima ieleweke uandishi wa habari si kipaji ambacho mtu anazaliwa nacho, ili kuwa mwanahabari kwa mujibu wa sheria ya Huduma za Habari ya 2016 na Kanuni zake za 2017 na marekebisho yake ni lazima mtu aingie darasani kusomea.

Ukisoma kanuni ya 17(2)(a) ya Kanuni za Huduma za Habari ya 2017 inasema ili mtu awe na sifa ya kutambuliwa kama mwanahabari ni lazima awe na kiwango cha elimu ya Stashahada au shahada ya habari kutoka chuo kinachotambuliwa.

Lakini ukisoma kifungu kidogo cha (b) inasema anaweza pia kuwa na shahada au stashahada yoyote inayohusiana na masuala ya habari kutoka chuo kinachotambulika na mamlaka, kwa hiyo sheria inasisitiza suala la elimu.

Kifungu kile cha 17(1) kinasema mtu yeyote anaweza kutambuliwa kama mwanataaluma akiwa ni mhariri au mwanahabari, mwanafunzi anayesomea taaluma ya habari na wananchi wenye utumishi bora kwa taaluma ya habari.

Lakini ukirudi nyuma ukasoma kifungu cha 13(a), (b) na (c) cha majukumu ya bodi ni pamoja na kumsimamisha au kumfukuza mwandishi wa habari kutoka orodha ya wanahabari walioidhinishwa na kutoza faini kwa anayekiuka kanuni hizo.

Nimetangulia kueleza kwa kirefu majukumu ya bodi na kuisimamia taaluma ya habari ili atakayepewa kitambulisho awe kweli amekidhi sifa za kitaaluma ili kuonyesha umuhimu mkubwa na majukumu mazito ya Bodi.

Hali tuliyonayo sasa ambapo kila anayeshika kalamu na 'note book' au 'mic' anakuwa mwanahabari kumeshusha heshima ya taaluma hii na utashangaa huko mitaani, ilifika mahali hata wapiga picha za harusi nao kujiita ni wanahabari.

Hili la kila mwenye 'notebook' na kalamu kujiita mwandishi wa habari lilizungumzwa pia na Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, akisema aliporuhusu uanzishaji vyombo binafsi vya habari, hapakuwa na tahadhari.

Alisema nia ilikuwa njema, lakini walipofungua milango, walisahau kufunga madirisha kwa hiyo taaluma ikavamiwa na watu ambao hawakuwa na sifa ya kuitwa waandishi wa habari na tatizo hili limedumu zaidi ya miaka 30.

Ni kutokana na kukosekana kwa usimamizi wa taaluma, leo hii kuna mambo ya hovyo yanaendelea radio na televisheni za mtandaoni, zinazosimamiwa na watu wasio na taaluma ya habari na kufanya waandishi wote tuonekane wa hovyo.

Unakuta huyo anayejiita mwandishi wa habari hana ABC zozote za taaluma ya habari, anauliza maswali kwa 'source' (mtoa habari) mpaka unataka kuingia chini ya meza na baadhi hawavai nadhifu, wanavaa kihuni jambo linalotia aibu.

Ndio maana ninasema uzinduzi wa Bodi ya Ithibati kesho ni jambo moja, na kusimamia uandishi wa habari uwe ni taaluma inayoheshimika ni jambo jingine. Hilo jambo jingine ndilo tunataka tuone wana taaluma ndio wanatambuliwa.

Tunataka taaluma ya habari iheshimike kama mhimili wa nne usio rasmi (Fourth Estate) na iheshimike kama taaluma nyingine zenye bodi za kitaaluma kama mawakili, wahandisi, wahasibu na wakaguzi wa Hesabu, madaktari na wauguzi.

Haiwezekani ambaye hajasomea sheria akawa wakili, ambaye hajasomea udaktari akawa daktari au ambaye hajasomea uhandisi akafanya kazi ya uhandisi na hivyo hivyo tunataka aliyesomea uandishi wa habari ndiye aitwe mwandishi wa habari.

Kama muuguzi tu anayefunga vidonda hospitalini ni lazima asomee taaluma hiyo sembuse mwandishi wa habari ambaye akikosea tu kupeleka ujumbe kwa umma, madhara yake ni makubwa na si kwa mtu mmoja, bali inaweza kuwa taifa zima.

Ni muhimu sana Bodi ikafanya uhakiki wa taaluma kwa kila atakayeomba kutambuliwa kama mwanahabari na mifumo ya uhakiki wa elimu isomane ili itakapomtambua muombaji ni mwana taaluma basi awe mwana taaluma kweli.

Mifumo ninayoizungumzia ni ile ya Bodi ya Ithibati ya wanahabari isomane na ile ya Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Baraza la Taifa na Elimu ya ufundi (Nactevet) na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kabla ya kumthibitisha.

Uzuri kifungu kile cha 17 cha Kanuni za sheria za huduma za Habari 2017 na marekebisho yake ya 2024 kimeweka wazi kiwango cha chini cha elimu, tusiruhusu visingizio vyovyote, waandishi waliopo kazini walipewa muda kutosha wa kusoma.

Tukiamua kuiondoa taaluma hii kutoka kwenye uholela ambapo hata baadhi ya wapiga picha mitaani au washereheshaji (MC) nao kujiita wanahabari, au washika Mic (vipaza sauti) huko kwenye televisheni za mitandaoni, tutaiheshimisha.

Mwandishi wa vitabu, Issac Asimov alipata kusema “anyone who writes about science must know about science”, kwamba yeyote anayeandika Habari za sayansi ni lazima aijue sayansi, na kwenye habari inapaswa kuwa hivyo hivyo.

Kwamba anayeandika habari lazima awe amesomea taaluma ya Habari, anajua ABC zake, anaijua misingi yake, anajua maadili na miiko yake na ni Bodi ya Ithibati itasaidia kuiheshimisha taaluma hii, kama itasimamia sheria kikamilifu.

Sina mashaka na weledi wa wanataaluma wanaunda bodi hii, wanaifahamu vizuri taaluma, changamoto zake, mahali tulipotoka, tulipo na tunapotaka kwenda. Bodi hii ikishirikiana na taasisi za kihabari na kitaaluma, tutafika tunapotaka kwenda.

0656600900