Prime
UCHAMBUZI WA MALOTO: Wanaotetea maandamano hawakemei uhalifu, waliochukizwa na uhalifu hawalalamikii mauaji
Mali za umma na watu binafsi ziliharibiwa, na zaidi kuteketezwa. Watu wamepoteza maisha, tena vijana. Taifa la Tanzania limegawanyika makundi mawili.
Wapo wanaosema uharibifu ule wa mali ni uhalifu, wengine wanatetea kwamba yalikuwa maandamano ya amani.
Wengine wanahoji, maandamano gani ya amani, watu walikusanyika wakiwa wamebeba madumu ya petroli na viberiti kwa ajili ya kuchoma mali za umma na watu binafsi?
Kundi lingine linalalamikia matumizi ya risasi za moto ambazo zimekuwa chanzo cha vifo.
Angalau Dk Samia Suluhu Hassan, wakati wa hotuba yake ya uapisho kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muhula wa pili, alitambua uwepo wa vifo, akasikitikia na kutoa wosia kwa umma, hasa kwa wazazi kuhusu nafasi yao katika malezi.
Na nini cha kushika kipindi cha njia panda za kimaisha. “Niwasihi Watanzania, tuchague hekima badala ya ghadhabu, busara badala ya mihemko, upendo badala ya chuki, uvumilivu badala ya vinyongo, umoja badala ya mgawanyiko, na amani badala ya vurugu. Lakini vilevile ni wajibu wetu kuchagua unyenyekevu badala ya kiburi, na huruma badala ya hasira. Taifa letu ni moja na lenye nguvu kuliko mtu yeyote yule.” Mwisho wa kumnukuu Rais Samia.
Nyakati zilizopo kama nchi, zinahitaji tafakuri nzito. Kuchambua madhara ya kila upande. Kutoka vifo vilivyotokea hadi mali zilizoharibiwa.
Mateso ya watu kukosa chakula baada ya huduma nyingi za kijamii kukosekana. Ajira zimepotea, baada ya maeneo ambayo walikuwa wanafanyia kazi kuharibiwa, kuibiwa au kuteketezwa kwa moto.
Tutafakari taharuki na wasiwasi wa watu ambao waliwindwa na kukaguliwa vidole vyao ili waonekane kama kweli walipiga kura.
Nimesikia sauti ikihoji je, ni aina gani ya maandamano ya kudai haki kwa kuwashughulikia ambao walikinzana misimamo?
Ukikataa kupiga kura kwa utashi wako, ndiyo umzuie mwingine naye kufuata upande alioona unafaa?
Hakuna haki inayoingilia haki ya wengine. Kipindi hiki cha tafakuri kwa nchi, inabidi kusemezana kuanzia ngazi ya familia, maofisini, vijiweni na majukwaa ya mitandao ya kijamii kuwa njia sahihi ya kudai haki yako ni ile ambayo unaitumia pasipo kuingilia, kubughudhi, kunyang’anya au kudhulumu haki ya mwingine.
Kama nchi, kuna mambo yanapaswa kuwaweka pamoja Watanzania kipindi hiki cha tafakuri ili kuiendea kesho iliyo bora. Lazima kukubaliana kwenye mambo mabaya yaliyotokea, halafu kuwe na ushirikiano wa kuyalaani.
Kwanza, mali ziliharibiwa, pili vifo vimetokea. Suluhu ianze kwa kutambua madhara hayo.
Jambo ambalo inabidi litambuliwe kwa nafasi ya kwanza ni kuwa chuki ndiyo chanzo cha kila kitu. Hamasa iliyotoka mitandaoni, iliwajenga vijana kuamini kwamba kuna watu wananeemeka zaidi na nchi.
Kwamba wapo watu wachache ndiyo wanaonufaika na keki ya Taifa. Wanaila wao peke yao, hawaachii na wengine wale.
Kijana asiye na ajira, anaposikia taarifa kama hiyo, lazima apatwe na chuki. Haishangazi kuona watu wakiingia barabarani wakiwa wamejawa hasira kali, na kuanza kushughulika na mali za umma pamoja na za watu binafsi, badala ya kubeba mabango yenye ujumbe, ili kuwasilisha kile ambacho walikihitaji kama raia.
Ni chuki kubwa ndani ya jamii, ndiyo maana mali za watu zimeteketezwa kwa kudhaniwa ni za walengwa fulani. Mathalani, mabasi ya Esther Luxury Coach, watu waliyafuata kwenye yadi na kuyachoma moto. Ujumbe ulitembea Oktoba 29, 2025, kwamba “Mabasi ya Mwigulu Nchemba yamechomwa moto.”
Taifa limekuwa na upandikizwaji mkubwa wa chuki za kijamii.
Mtu mmoja anavumishwa kwamba ana utajiri mkubwa na anamiliki mali nyingi. Yanatajwa mabasi, vituo vya mafuta na gesi, majengo makubwa (maghorofa), vituo vya manunuzi na kadhalika. Wamiliki halisi wapo, lakini wanatajwa wengine ili kuwajengea uhasama wa kijamii.
Ona sasa, mabasi ya Esther yakachomwa moto. Wachomaji waliaminishwa na wakaamini kwamba mmiliki ni mwanasiasa mwandamizi Tanzania.
Hasara moja kwa moja inakwenda kwa wamiliki halisi ambao ni wawili. Watanzania waliopambana na kufanikiwa kusimama kibiashara, wanashambuliwa na wenzao kisa chuki za kijamii.
Kampuni ya mabasi ya Esther, inamilikiwa na wazawa Joseph Didas Ngeleuya na Neema Peter Thomas, kama inavyoainishwa kwenye nyaraka za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra). Waliochoma moto mabasi ya kampuni hiyo, walitamba kwamba wanamkomoa Mwigulu.
Vituo vya mafuta na gesi vya Lake Oil, ambavyo vinamilikiwa na kampuni ya Lake Oil Limited, navyo vikakumbana na shambulio. Vijana walivichoma moto, wakapora mitungi ya gesi na mali nyingine. Walisema wanafanya hivyo ili kumkomoa mwanasiasa Ridhiwani Kikwete, ambaye ni mtoto wa Rais wa awamu ya nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Mmiliki wa kampuni ya Lake Oil Limited, kwa mujibu wa nyaraka za Brela ni mfanyabiashara Ally Edha Awadh. Zaidi, ukipitia wasifu wa Lake Oil Limited, kama ulivyochapishwa kwenye tovuti yao rasmi, inaonesha kuwa Awadh alianzisha kampuni hiyo mwaka 2006, akiwa na umri wa miaka 27.
Mtazame Awadh, ambaye ameadhibiwa kwa sababu ya chuki ya kijamii. Siyo chuki dhidi yake, bali kwa mali zake kutajwa kwamba zinamilikiwa na mtu ambaye jamii imetengenezwa kuamini kuwa ni tajiri kupita kiasi, na utajiri wake umetokana na kujimegea keki kubwa ya Taifa, huku wengine wakitaabika na maisha mitaani.
Namtazama kijana wa Magomeni, Dar es Salaam, ambaye duka lake la kuuza kamera, lilivamiwa, wakapora kila kitu, kisha wakaliharibu. Hiyo ni sawa na wajasiriamali wengine ambao walijikomboa kwa kuanzisha ofisi za kibiashara, wapo wauza simu, nguo na thamani nyingine. Waliporwa na maduka yao kuharibiwa!
Tukio la Oktoba 29, 2025, uharibifu wa mali na vifo vilivyotokea, ni shule yenye mtihani mgumu.
Ufaulu wake utawezesha kuiendea Tanzania ya kesho ikiwa yenye neema, upendo, umoja na mshikamo. Kufeli kwake ni kuendelea kuunda bomu litakalolipuka na kuiangamiza nchi nyakati zijazo.
Nini mwarobaini wa chuki zinazopandikizwa? Nani anapandikiza chuki na kwa masilahi gani? Tunataka kujenga taifa la aina gani, ikiwa wananchi wanajengwa kuchukiana wao kwa wao?
Ni hatari kubwa kwa taifa ambalo limelea na linaendelea kulea wakimbizi waliokimbia machafuko nchini kwao yaliyotokana na chuki za kiraia, nalo linaruhusu chuki kustawi.
Wajibu wa wenye umri mkubwa ni upi? Hawawasimulii vijana kuhusu Rwanda na Burundi yenye vita ya Wahutu na Watutsi. Hawawapi hadithi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Sudan, kisha Sudan Kusini ya mapambano ya Dinka na Nuer.
Hakuna faida yoyote katikati ya machafuko, zaidi ya uharibifu wa mali na vifo vya watu wasio na hatia.
Yupo mtu aliniambia kwa kuhoji, kwamba tangu lini Dar es Salaam watu wakavaa makoti na mizula kichwani, tena mchana wa jua kali?
Alikuwa anajaribu kunielewesha kwamba kuna watu ambao ni zaidi ya Watanzania walishiriki ghasia zilizosababisha madhara makubwa.
Alijaribu kujenga picha kutokana na uvaaji wa wahusika kutoendana na utamaduni wa wakazi wa Dar es Salaam.
Hili limesemwa sana. Kuna watu maeneo kadhaa ya Dar es Salaam, walisema kuwa wapo wahusika wa ghasia hawakuwa wakizungumza Kiswahili cha Kitanzania. Rais Samia pia alisema waliokamatwa kutokana na kadhia hiyo, baadhi siyo raia wa Tanzania.
Hiyo ya wageni kushiriki ghasia za Oktoba 29, 2025, nalo linahitaji tafakuri. Kwa nini wageni waingie na kushiriki matukio ya fujo? Waliwezaje? Vyombo vipo wapi? Je, Tanzania ina uadui na mataifa jirani? Wakati tukitafuta majibu ya maswali yote, muhimu ni kutambua madhara ya kila upande na kusaka suluhu ya pamoja, vifo na uharibifu wa mali za umma na watu binafsi. Vyote vimetokea na matendo yote ni mabaya.