Tuipe elimu ya watu wazima sura mpya
Katika historia ya elimu ya Tanzania, dhana ya elimu ya watu wazima imekuwa ikihusishwa zaidi na kampeni za kufundisha watu kusoma na kuandika.
Hata hivyo, leo tunapozungumzia elimu hii, tunapaswa kuipa tafsiri pana na ya kisasa zaidi.
Sisi Mwananchi tunaungana na wadau waliotoa ushauri kwa Serikali kuhusu haja ya kufanya maboresho, ili elimu ya watu wazima iwe na maana pana, ya kuvutia na yenye kuleta matokeo chanya kwa Taifa.
Moja ya mapendekezo hayo ni kuhakikisha kila kata nchini inakuwa na kituo cha elimu jumuishi. Hatua hii ni muhimu kwa sababu inawapa watu wazima nafasi ya karibu zaidi ya kupata maarifa bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.
Katika jamii zetu za vijijini, upatikanaji wa elimu bado ni changamoto kubwa. Kuwa na kituo cha elimu katika kila kata si tu kunarahisisha upatikanaji, bali pia kunatoa ujumbe wa wazi kwamba Serikali inathamini haki ya kila mtu kupata fursa ya kujifunza katika umri wowote.
Pendekezo jingine lililotolewa ni kuifanya elimu ya watu wazima iendane na mazingira ya dunia ya sasa. Hii ni hoja ya msingi sana.
Dunia ya leo imebadilika; ajira, biashara, na maisha ya kila siku vinategemea teknolojia, maarifa ya kidijitali, stadi za ujasiriamali na uelewa wa masuala ya kimataifa.
Hivyo basi, elimu ya watu wazima haitakiwi kuishia kwenye kujua kusoma na kuandika pekee, bali iende mbali zaidi kuwapa wananchi ujuzi wa kompyuta, stadi za biashara, ufugaji na kilimo cha kisasa, elimu ya fedha, na hata ujuzi wa lugha za kigeni.
Haya ndiyo mambo yatakayowawezesha watu wazima kushindana katika soko la ajira la sasa na kesho.
Mara nyingi tumeshuhudia miradi mizuri ikianza kwa kishindo, lakini baada ya muda hupoteza nguvu kwa sababu ya ukosefu wa mipango endelevu. Hatupaswi kurudia makosa hayo.
Elimu ya watu wazima inahitaji mkakati thabiti wa muda mrefu, unaoungwa mkono na bajeti, sera, na rasilimali watu.
Kuna ushauri wa kuhakikisha kuwa elimu ya watu wazima inakuwa rafiki na inazingatia mazingira ya kijamii na kiuchumi ya wanaoihitaji.
Hii inamaanisha kwamba ratiba za masomo, aina ya mitalaa na mbinu za ufundishaji ziwe zenye kubadilika ili kuwavutia watu wazima ambao mara nyingi wana majukumu ya kifamilia na kikazi.
Mwananchi tunasisitiza kwamba mapendekezo haya mazuri yasibaki tu kwenye nyaraka za kiofisi.
Mara nyingi tumeshuhudia mijadala mizuri kwenye semina na makongamano, lakini matokeo yake hayafikii wananchi wanaolengwa.
Wadau wamefanya kazi yao ya kutoa mawazo, sasa jukumu kubwa lipo kwa mamlaka husika kuhakikisha haya yanageuka vitendo vinavyoleta mabadiliko halisi.
Tunapozungumzia mabadiliko, hatuzungumzii tu maboresho ya mitalaa au kujenga majengo. Tunamaanisha mabadiliko katika mtazamo wa taifa zima kuhusu elimu ya watu wazima.
Tunahitaji jamii iondokane na fikra kwamba elimu hii ni kwa ajili ya wale waliokosa nafasi shuleni pekee. Badala yake, ieleweke kuwa kila mtu, bila kujali umri, anahitaji kujifunza mara kwa mara ili kuendana na dunia inayobadilika kila siku.
Ikiwa Serikali itachukua hatua thabiti kutekeleza mapendekezo haya, basi Tanzania inaweza kuibua kizazi kipya cha watu wazima wenye maarifa mapana na stadi ya kuchangia maendeleo kwa kiwango kikubwa.