TLS tutumie fursa hii kumweleza ukweli Rais Samia

Sehemu ya bandari ya Dar es Salaam. Picha na Maktaba
Mwaka huu, Chama cha Mawakili cha Tanganyika (TLS), kinaadhimisha miaka 70 tangu kuasisiwa kwake mwaka 1954. Katika maadhimisho yatakayofanyika jijini Dodoma, mgeni rasmi ni Rais Samia Suluhu Hassan.
Nikiwa mmoja wa wanachama hai wa chama hiki, hii ni makala ya kufikiri kwa sauti, je, TLS imweleze ukweli Rais Samia kuhusu ubatili wa Katiba yetu na sheria zetu au iendelee kuunyamazia kwa sababu ubatili huo umefanywa na Serikali na kubarikiwa na Bunge huku Mahakama ikinawa mikono?
TLS ni moja ya vyama vikongwe kabisa vilivyoanzishwa hata kabla ya Tanganyika kupata uhuru. Majukumu yake ya msingi, kwa mujibu wa tovuti yake; kwanza, nilichokutana nacho, ni lugha ya kimombo.
Naomba na mimi niende nao hivyo hivyo, lakini kiukweli wakoloni wametufanya vibaya kwenye eneo “indoctrination”, Tanzania lugha yetu ya taifa ni Kiswahili ambayo ni lugha adhimu, lakini TLS wao ni kimombo tu, wale wenzangu na mimi wa St Kayumba, mtanisamehe.
Ukiingia tovuti ya TLS (www.tls.or.tz), unapokelewa na makaribisho ya utambulisho wa TLS ni nini na kina nani, kisha inakuja idadi ya wanachama wao, ambao na mimi nimo. Tanzania tuna mawakili 8,514 wanaofanya uwakili, mawakili 1,007 wasiofanya uwakili na mawakili 387
waliotangulia mbele ya haki.
Kisha wanakuja na tamko la dira (vision) na malengo (mission) yao. Ndipo tunapata makaribisho ya rais wa TLS, Wakili Harold Sungusia.
Kwenye Majukumu ya TLS, naomba kujikita kwenye jukumu moja tu, “to support the State Organs in legislation and administration of rule of law” ikiwa na maana “kuisaidia serikali kwenye utungaji wa sheria na utawala wa sheria”.
Kabla sheria yoyote haijatungwa, TLS kama wadau wa sheria, wanaipitia, wanatupa wanachama wao wote fursa ya kutoa maoni, kisha TLS inapeleka maoni yake ya kisheria, ndipo sheria inatungwa.
Tangu nimejiunga TLS, nimekuwa nahudhuria vikao vya kukusanya maoni kuhusu ule mkataba wa makubaliano kati ya Serikali (IGA) ya kampuni ya DP World na bandari ya Dar es Salaam, nikaipongeza TLS kwa maoni yake, kiukweli kabisa yalikuwa magumu.
Serikali na Bunge ilipigwa na kitu kizito. Hoja za kisheria za TLS, zilipuuzwa, hazikujibiwa na TLS ikanyamaza.
Hivyo ujio wa Rais Samia kwenye AGM yetu, hii sasa ni fursa adimu na adhimu ya kulizungumza hili, kwa Rais Samia na yeye kulisikia kwa masikio yake mwenyewe, maana wasaidizi wake wa sheria, hawawezi kumweleza kwa sababu ni wao, japo sio waliouanza ubatili huo, bali ndio wanaouendeleza ubatili huo.
Hili la ubatili wa Katiba ni jambo kubwa sana ambalo TLS ilibidi washughulike nalo tangu pale Mahakama Kuu ilipotamka ubatili huo wa Katiba na sheria hiyo.
Siku TLS wametuita wadau wao kututaka tuchangie maoni yetu kwenye mkataba wa DPW na bandari zetu, mimi niliwapongeza TLS. Nimelizungumza sana kwenye awamu hii ya sita ya Rais Samia na kuandika makala zaidi ya 20.
Sasa kwa kuwa imejitokeza fursa ya TLS kuhutubiwa na Rais Samia, hii ni fursa adimu na adhimu kwa TLS, tumweleze Rais Samia kuhusu ubatili wa Katiba yetu unaonyima haki ya Watanzania kuchagua na kuchaguliwa ambao wasaidizi wake hawamwambii.
Serikali yake imetutungia muswada batili wa sheria ya uchaguzi, Bunge likapitisha muswada huo, hivyo kukutungia tena sheria batili na yeye akaisaini ianze kutumika na ubatili wake, hivyo hivyo.
Sisi hatumlaumu Rais Samia kwa kusaini sheria batili, kwa sababu yeye si mwanasheria kuujua ubatili huo, lakini wasaidizi wake ni wanasheria wanaujua fika ubatili wa Katiba yetu na sheria zetu, lakini hawamwambii.
Hivyo, hii ni fursa, kwa TLS kutimiza wajibu wake kikamilifu kwa kumweleza ukweli Rais Samia kuwa ni lazima tufanye kwanza mabadiliko madogo ya Katiba (minimum reforms), ndipo twende kwenye uchaguzi.
Tumshauri Rais Samia kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa uahirishwe kwanza, tuondoe kwanza ubatili wa Katiba, tufanye marekebisho ya sheria, ndipo twende kwenye uchaguzi na uchaguzi huo wa serikali za mtaa ufanyike siku moja na uchaguzi mkuu na kusimamiwa na Tume moja huru na shirikishi ya uchaguzi.