Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vyama, vyaishtukia Serikali Katiba mpya

Muktasari:

  • Zikiwa zimepita wiki mbili tangu Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro kutangaza kuanza mchakato wa Katiba kwa kutoa elimu kwa wananchi, baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani na asasi za kiraia, wamekosoa na kutaka muswada wa Sheria ya mabadiliko ya Katiba upelekwe kwanza bungeni.

Dar es Salaam. Zikiwa zimepita wiki mbili tangu Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro kutangaza kuanza mchakato wa Katiba kwa kutoa elimu kwa wananchi, baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani na asasi za kiraia, wamekosoa na kutaka muswada wa Sheria ya mabadiliko ya Katiba upelekwe kwanza bungeni.

Julai 27 mwaka huu, Waziri Ndumbaro akiwa Songea mkoani Ruvuma, aliwaambia waandishi wa habari mchakato wa Katiba utaanza Septemba mwaka huu kwa kutoa elimu ya Katiba iiyopo sasa.

Jana alipoulizwa kwa simu, Waziri Ndumbaro alisema:"Kama wamesema hivyo, waulize wao, mimi ya kwangu nimeshayasema, sitayarudia. Walioongea wao wewe yaandike, ya kwangu si mliandika? Wewe yaandike, ndio uhuru wa kutoa maoni.’’

Akizungumza jana katika mjadala wa mabadiliko ya Katiba ulioandaliwa na Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema kauli hiyo ni mtego wa kuchelewesha mchakato wa Katiba.

"Maoni yetu, wadau na asasi za kiraia wasiingie kwenye mtego huu wa kuchelewesha Katiba mpya, badala yake Serikali ipeleke muswada bungeni Septemba," alisema.

Alisema katika mkutano wa Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wa vyama vya siasa uliofanyika Ikulu ya Dar es Salaam Januari 3, mwaka huu, aliahidi kuanzisha kamati kuhusu Katiba.

"Sisi tunaamini hiyo ni kamati ya mwafaka wa Katiba na hapaswi kuiunda yeye mwenyewe bali iwe ndani ya sheria.

"Rais aharakishe kuundwa muswada utakaopelekwa bungeni Septemba ili kuweka utaratibu na ratiba nzima ya mchakato wa Katiba," alisema.

Alisema kwa kuwa muda unazidi kwenda, mchakato wa Katiba unapaswa kujikita katika mambo muhimu zikiwemo sheria za uchaguzi.

Kwa upande wake. msemaji wa Katiba na Sheria wa ACT- Wazalendo, Mbarara Maharagande aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu alisema wakati wakitarajia mchakato wa Katiba kuanza, Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa imewataka kutoa maoni ya mabadiliko ya sheria za uchaguzi. "Tukashtuka maana mabadiliko ya Katiba bado hayajafanyika. Kwa hiyo tuliona haina nia nzuri," alisema.

Alisema chama hicho kilishiriki kwenye kikosi kazi kikamilifu cha wadau wa siasa ambapo walishauri mambo manne likiwamo kuendelezwa kwa mchakato wa Katiba.

"Sisi tunaamini mamlaka ya kutafsiri maoni ya wananchi yalikuwa chini ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Bunge halikutakiwa kubomoa misingi.

"Tunashauri kufanyika kwa mabadiliko ya sheria ya Katiba ili kukIdhi matakwa ya sasa na kuna haja ya kuwa na mkutano wa kitaifa wa maridhiano utakaoshirikisha wadau mbalimbali," aisema.

Aligusia pia mambo waliyotaka yaangaliwe katika mchakato huo kuwa ni pamoja na kujenga mwafaka wa kitaifa, Muungano na muundo wake, madaraka ya rais, mgawanyo wa madaraka wa mihimili yetu na mfumo wa uchaguzi.

Naye Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe alisema lengo la kudai mabadiliko ya Katiba ni kuondokana na ubaguzi wa kisiasa.

"Watanzania tunaona hii Katiba ya sasa inatuletea kichefuchefu, ina maneno ya upendeleo wa nani awe kiongozi, wengine ni wasindikizaji tu. Tunataka Katiba itakayozungumzia haki za wananchi," alisema.

Awali, akitoa mada katika mkutano huo, mjumbe wa Jukata, Deus Kibamba alisema baada ya Rais Samia kuingia madarakani Machi 19, 2021, mchakato wa Katiba ulifufuliwa baada ya kukwama katika awamu ya tano.

"Mchakato uliopo ni kama gari limenasa kwenye matope, sasa lazima lishtuliwe. Habari njema! Gari limeanza kunasuka. Juni 2022 CCM ilitoa tamko kuwa mchakato uendelee. Wakaiagiza Serikali yao kwamba mchakato huo uanze ili kuukamilisha," alisema.

Hata hivyo, alisema tangu wakati huo utekelezaji wake umekuwa kitendawili.

"Mimi nilitegemea kwamba Waziri wa Katiba na Sheria angepokea agizo na kuanza utekelezaji, lakini mwaka ukapita bila utekelezaji wake," alisema.

Alisema ili mchakato huo uanze, ilitarajiwa kuwe na mabadiliko ya sheria yatakayounda sheria ya mabadiliko ya Katiba.

"Nilimwelewa kuwa Rais alikubali kuandaa kamati ya watalaamu. Hata hivyo maswali mengine hayajajibiwa: Kamati itafanyaje kazi? Wajumbe watakuwaje? Sheria ya mchakato?" alihoji.

Kuhusu bajeti ya Sh9 bilioni iliyotengwa na Serikali kwa ajili ya mchakato wa Katiba, alisema.

"Bajeti ya mchakato ni Sh9 bilioni imepitishwa, hakuna andiko wala maelezo, je amezipataje? Undani wake uko wapi?

Waziri alitakiwa kutoa ramani, Sheria ya mabadiliko ya Katiba, sheria ya kura ya maoni, bajeti, kamati," alisema.

Naye Askofu wa kanisa Menonite Tanzania, Nelson Kisare aliwataka wadau wa mabadiliko ya Katiba kuwa na nia moja na kuwa makini.

"Tujiulize tumekwama wapi? Neno la Mungu linasema wana Israel walizunguka jangwani miaka 40, kwa hiyo tutazungushwa kamati moja baada ya nyingine lakini mko pale pale huku tukitumia fedha," alisema.