Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TAHARIRI: Litafutwe suluhisho la ngedere, bundi SGR

Ikiwa ni siku sita tangu usafiri wa abiria wa treni ya reli ya kiwango cha kimataifa (SGR) uanze rasmi kati ya Dar es Salaam na Dodoma, limejitokeza jambo ambalo halipaswi kupita bila kulizungunzia.

Pamoja na mafanikio hayo ya treni kukatiza umbali wa kilomita 541 kwa muda wa saa 3 na dakika 25, jana Shirika la Reli Tanzania (TRC) liliomba radhi baada ya treni hiyo ya umeme kusimama kwa saa mbili kutokana na hitilafu ya umeme.

Safari za treni ya SGR kwanza kati ya Dar es Salaam na Morogoro na baadaye Dodoma zimeleta matumaini kwa Watanzania wengi kwamba wamepata mkombozi wa kusafiri haraka, nafuu na salama.

Kwanza tunaipongeza Serikali kwa kufanikisha usafiri huu uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu na wengi, kwa muda mrefu.

Hata hivyo, kukatika kwa umeme katika kituo cha kupozea umeme namba saba (Godegode) saa 4:20 usiku na kusababisha abiria kukwama porini, hakuleti taswira nzuri ya mradi huo wa mabilioni ya shilingi.

Licha ya TRC kuomba radhi na kutoa sababu kwamba hitilafu hiyo ilisababishwa na bundi na ngedere waliogusa nyaya, bado suala hilo lingeweza kuepukika mapema, kwa kuwa reli inapita porini na kuna namna ya kujikinga na madhara ya wanyama hao.

Tunajua muungwana huomba radhi, lakini TRC ilipaswa kutoa hakikisho la kutojirudia kwa hali hiyo kwa kuchukua tahadhari mapema.

Pia, TRC ilipaswa kueleza suluhisho ya madhara ya wanyama na ndege ni nini, au tutaendelea kusimamisha huduma kila linapotokea tatizo kama hilo?

Madhara ya wanyamapori na ndege yanajulikana, TRC kwa nini hawakuweka vifuniko kwenye nyaya hizo au kuzifunika na plastiki zitakazozuia msuguano unaoweza kuleta hitilafu.

Hatuna nia ya kusema kilichotokea ni inaweza kuwa hujuma, lakini kulingana na taarifa kadhaa za TRC kuhusu kuwepo vitendo vya hujuma, ni vema pia wakajipanga kwa hilo.

Mfano, TRC iliwahi kutoa taarifa kuhusu hujuma kwenye njia ya reli ya kwenda Moshi mkoani Kilimanjaro kwamba kumekuwa na matukio ya hujuma kwa kutega vyuma relini.

Tunatambua kuwa suala hilo ni la dharura, lakini linaibua maswali mengi kwa kuwa TRC iliwahi kusema inatarajia kuagiza vichwa vya ‘hybrid’ vyenye mifumo miwili, kwamba ikitokea dharura wanatumia vichwa vyenye mifumo ya umeme, mafuta na betri kwa ajili ya dharura.

Katika ufafanuzi huo ilielezwa vichwa hivyo vingekuwa na betri ambayo ina uwezo wa kujichaji kadri treni inavyofanya kazi na baadaye nishati hiyo inaweza kutumika kwa dharura pindi kunapokuwa na tatizo.

Ufafanuzi huo ulitokana na maswali ya wananchi ya kutilia shaka treni hiyo ya umeme itakavyofanya kazi wakati kuna katikakatika ya umeme.

Tunajiuliza kama kuna vichwa vinavyotumia betri au vyenye mfumo wa kutumia mafuta, kwa nini havikuletwa kuokoa jahazi?

Uongozi huo uliwahi kuzungumzia hujuma kwa kuondolewa kipande cha reli na kurudishwa kwa kuegeshwa kulikosababisha ajali ya treni ya abiria mkoani Tabora.

Si hivyo tu, baada ya kuzinduliwa SGR kwenda mkoani Morogoro, TRC ilitoa taarifa ikikiri kutokea changamoto kadhaa, ukiwemo uhujumu wa sehemu ya miundombinu ya reli hiyo.

Kutokana na hayo tungependa kushauri viashiria hivyo vya kiusalama vipewe kipaumbele na kufanyiwa kazi badala ya kusubiri kutolea taarifa na kuomba radhi.