Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ONGEA NA AUNT BETTIE: Nachukiwa na mama mkwe akidhani najizuia kuzaa

Swali: Nimeolewa miaka mitatu iliyopita, kimsingi mama mkwe ndiye aliyeniona na kunipenda na kuniambia atahakikisha ninaolewa na kijana wake.

Baada ya mwaka kweli niliolewa na kijana wake, ingawa tulikutana mjini tukapendana, lakini hata tukikaa tunakumbuka kauli ya mama mkwe ambayo aliwahi kumwambia na kijana wake pia.

Mwaka mmoja wa mwanzo mambo yalikuwa mazuri ninawasiliana na mama mkwe, nampa zawadi na ninakwenda likizo. Kwa kweli alikuwa ananipenda sana na anapotaka kupumzika akija mjini anafikia kwangu, kwa watoto wake wengine anakwenda kusalimia tu. Lakini tangu umeanza mwaka wa pili katikati alibadilika ghafla, hanipigii simu na nikimpigia akipokea anazungumza kama amelazimishwa.

Nilipopata likizo nikaenda kijijini kumsalimia na kujua labda ana changamoto anashindwa kuniambia kwenye simu.

Kwanza hakunipokea vizuri kama kawaida yake. Siku iliyofuata akaniita ndani kwake na kunieleza kuwa anachukizwa na tabia yangu ya kujizuia kuzaa. Nilistuka kwanza na nikamueleza sijizuii ila Mungu hajanipa. Niliishia hapohapo, mama alizungumza kwa kujiamini kuwa ninajizuia ujana umenitawala na ninaona nikizaa sitofanya anasa. Kifupi Anti huyu mama ananichukia sana tena waziwazi na siku hizi ananinanga hata mbele za watu. Naapa sijajizuia kupata mimba ila hanielewi, hata sijui nifanyeje?

Jibu: Pole. Hali kama hiyo ni ngumu sana kwa sababu inahusisha hisia za familia na matarajio ya kina mama walio wengi kwamba vijana wao wakioa au kuolewa kinachofuata ni kuanzisha familia, kwa maana ya kupata watoto.

Hujasema mumeo anasema nini katika hilo. Ila jambo la muhimu ni kuzungumza na mama mkwe wako kwa heshima na uwazi ukiwa na mumeo. Mweleze kuhusu jitihada zako na mtazamo wa mume wako.

Kama mmewahi kwenda hospitali kushughulikia suala hilo, mweleze taarifa za daktari, ikiwamo sababu za kuchelewa kupata mtoto na mlichoshauriwa kufanya na daktari ili kufanikisha hitaji hilo la familia. Anaweza kukushauri kutumia dawa za kienyeji mwambie sawa, nipe nitazitumia. Zikiwa zimeandaliwa kitaalamu unaweza kuzitumia, ukiwa na mashaka nazo ziache ila bila yeye kujua. Akishiriki kutatua tatizo atapunguza jazba na kukuchukia. Hakikisha mumeo anakuunga mkono kumuelewesha mama hali halisi na hatua mnazochukua. Miaka mitatu siyo mingi sana na si michache kutokuwa na mtoto, kama hamjawaza kuhusu hilo anzeni kufikiria. Ingawa inategemea na mipango yenu. Hakikisha mapenzi yako kwake hayapungui na heshima yake pia, kwani hana nia mbaya, ni kutokuwa na uelewa wa masuala ya uzazi, mkimuelewesha naamini atawaelewa.


Mmh! Mwenzangu anazungumza kama kasuku, nakosa utulivu

Swali: Anti kwa kawaida ninapenda kusoma vitabu. Shida yangu huwa napenda kusoma kwenye utulivu, nimekuwa nikifanya hivyo tangu nikiwa chuo ila nahisi ninakoelekea nitashindwa kwa sababu sipati utulivu kwa sababu mpenzi niliyenaye hawezi kukaa kimya.

Kweli nilimpendea ucheshi wake kiasi cha kufikiria kufunga naye ndoa siku za usoni, nikimaliza jambo ambalo ni la kisheria na yeye analijua. Ila hapana, mwanamke anaongeza huyu kama redio iliyochajiwa. Hajali umerudi umechoka, unataka utulivu ufanye kazi, usome ilimradi anazungumza tu kila wakati.

Akianza kuimba sasa! Kila wimbo anaujua mwanzo mwisho. Shida nyingine ninayoiona ni kuokoteza kesi kwa kuwa anapenda kuongea ongea akiokoteza kesi zake si kunakuwa na majibizano, nahisi ndiyo anachokipenda. Ninajieleza mpaka nimefikia mahali ninamtazama tu. Nauliza, nikikomaa naye atabadilika na kuacha tabia hizi zinazonikera au nitafute jambo la kufanya?

Jibu: Atabadilika kabisa, lakini akiwa anakupenda kwa dhati na anataka kufanya safari ya maisha na wewe.

Kila mara ninasema hapa kuwa tiba ya kwanza ya kutibu chochote kinachosumbua uhusiano wenu ni kuzungumza. Zungumza naye kwa upole na heshima umueleze hisia zako. Mwambie unahitaji muda wa utulivu na haimaanishi humpendi au huna hisia naye, bali ndivyo ulivyo kuna wakati unahitaji kutulia ufanye mambo yako, ikiwamo kusoma vitabu.

Katika mazungumzo yenu unaweza kumwambia kwamba baada ya kula kabla ya kulala unahitaji utulivu, unaweza pia kumshauri na yeye muda huo afanye nini, baada ya hapo muendelee na taratibu zenu.

Muhimu na litakalokusaidia ni kumshirikisha katika hayo mambo unayofanya ukihitaji utulivu, pengine hapendi kusoma vitabu, hivyo unaweza kumwambia kuna movie nzuri unataka kutazama pamoja naye, lakini kwa utulivu, au mkafanya matembezi ya jioni au asubuhi kwa utulivu, yaani kila mmoja akiwa kimya mpaka mmalize. Hamuwezi kuwa kimya kabisa, ila ukiweka utaratibu utampunguzia kuzungumzazungumza ovyo.

Pia mueleze awe msikilizaji zaidi, hivyo unapomweleza kitu mwambie akusikilize hadi umalize, ndiyo achangie, hii itamsaidia kupunguza hiyo tabia inayokukera. Ila usisahau kutenga muda wa kusikiliza mazungumzo yake, hata kama wakati mwingine anazungumza pumba, mrekebishe kwa heshima, lakini mpe sikio, usimpuuze.

Kumbuka mawasiliano ni muhimu katika uhusiano. Hakikisha mnakuwa na nafasi ya kuzungumza. Utulivu sawa, mazungumzo pia yana nafasi yake.