ONGEA NA AUNT BETTIE: Hanipi ushirikiano faragha, nataka kuoa mke mwingine anikate kiu

Swali: Nimeoa miaka kadhaa nyuma, nimejitahidi kuvumilia hili huba la mke wangu lisilokuwa na chembe ya ubunifu, nimechoka Anti.
Nafikiria kuoa mke mwingine kwa sababu siwezi kuzini. Nimejitahidi kwa kila hali kumueleza jinsi alivyo mzembe faragha, lakini akibadilika siku moja anarudia tena yaleyale. Anaweza kubadilika kweli au nitimize azma yangu ya kuoa maana naona najipunja sana.
Jibu: Wazo lako la kuoa siyo baya kulingana na mwongozo wa imani yako japo hujaitaja. Kama inaruhusu sawa. Lakini unaona ni busara kuoa mke kwa ajili ya kukuridhisha faragha? Siamini kama huyu uliyenaye ameshindwa kabisa au kuna namna humuelekezi vizuri.
Kama ulivyonishirikisha mimi, mshirikishe shangazi au bibi yake wakae naye wamwelekeze tena inaonekana hakuelekezwa vizuri. Ingawa hawa watamwambia kwa ujumla tu, lakini hawatajua wewe unataka aina gani ya mapenzi ili kiu yako ikatike.
Nakushauri usizungumze naye kuhusu hili ukiwa wa moto yaani unahitaji hilo suala kwa wakati huo. Zungumza naye mkiwa mmekaa rasmi kwa ajili ya majadiliano hayo. Mpe sifa zake kwa mambo mazuri anayoyafanya kama mke, kisha mwambie jambo moja linalokusononesha na kukukatisha tamaa ni uhondo anaokunyima faraghani.
Pia mweleze unataka akufanyie nini na nini, wanawake wote siyo wajanja wa kujua uguswe, ushikwe au ukaliwe mkao gani ili ufurahie tendo, hivyo mwambie. Na umesema ukimsema anabadilika siku moja kisha anarudia ina maana anafanya makusudi, hivyo mwambie ukweli kuwa pamoja na mambo mazuri anayofanya kama mke, hilo la kutokonga moyo wako faraghani linakufikirisha kuoa mke mwingine. Usimfiche, mweleze ili ajue ukubwa wa tatizo. Ila sikushauri kukurupuka kuoa, naamini bado kuna nafasi ya kuliweka hili sawa. Najua faraghani ndiyo ndoa yenyewe.
Ila na nyinyi wanawake mnaniangusha sana, suala la faragha nalo ni la kuweka ndoa yako hatarini, mnafeli wapi? Unayehusika na hili jitume, kuwa mbunifu kila jambo linahitaji kunogeshwa unashirikije kama unacheza gwaride!
Swali: Anti naomba kujua maana ni kama ninachanganyikiwa, hivi wanaume wenye mapenzi ya kweli bado wapo?
Nimechoka sana, nimeshaingia kwenye uhusiano na zaidi ya wanaume wanane, huku umri wangu ukiwa miaka 29. Kibaya zaidi kati ya wote sijapata mwenye mapenzi ya kweli, nimeishia kuumizwa tu.
Siyo kwamba ninachagua sana, hapana, napigwa matukio ya kweli ambayo hakuna namna, lazima uamue moja, kuachika au kuendelea kuteseka.
Nikikupa mifano yote hata wenzangu watakosa nafasi ya kujibiwa maswali yao, nakupa mfano mmoja. Nilikuwa nina mpenzi ambaye sikuwa na wasiwasi na uaminifu wake kwangu, hadi siku nilipokuja kubaini yupo na mimi kwa sababu nyingine na wala si mapenzi.
Alikuwa ananihudumia kama wengine wanavyofanya, ananitoa out, kwa kweli nilidhani angalau nimepata mtu anayejali hisia zangu, ila sikuwa namuelewa, nikipata hedhi, anakuwa hana raha kabisa. Siku moja bila kujua kama nimerudi alikuwa anazungumza na mtu ambaye mpaka leo simjui ni nani anamuambia anaomba Mungu nibebe mimba.
Sijui aliulizwa nini kwenye simu ila nikasikia anajibu ‘...Mbona hata home wanajua nipo naye kwa sababu nataka mbegu yake, ana akili, mrefu, sura nzuri na rangi ya kuvutia’. Sikusikia alichoulizwa tena, ila akacheka sana na kusema aagh, akizaa mbona fasta nampiga chini, najua mtoto atabaki kuwa wangu, tutalumbana lakini nitampata. Sikuamini nilichokisikia na sikuaga, niliondoka, baadhi ya vitu alivyotaka kunipa vilinifuata nilipo.
Alinibembeleza sana, ila sikuwa na mapenzi naye tena, hao wengine kuwafumania siyo jambo la kushitua. Nafanyaje nimpate mwenye mapenzi ya kweli asiyekuwa na sababu kama za huyu mwehu niliyekusimulia.
Nisaidie Anti, nimechoka kubadili wanaume.
Pole sana. Kabla sijakushauri kwanza nikupe tu ninachokifahamu ni kuwa kila mtu huwa na mtu kwa sababu. Hata wanaopendana hupendana kwa sababu ingawa si ya kuachana.
Huyu uliyenaye kwanza anahitaji kupatiwa ushauri, inaonekana wazi ana shida ya afya ya akili, kabla hujaamua chochote washirikishe rafiki zake apatiwe mtaalamu wa ushauri nasaha, hayupo sawa.
Kwa akili ya kawaida upange kuzaa na mtu kisha umuache kwa sababu ulikuwa unataka mbegu yake tu, akizaliwa mtoto hajafanana na hiyo mbegu anayoitaka ina maana atawaacha wote mama na mtoto? Ndiyo maana inakuambia ana shida kichwani.
Pia labda kuna vitu unafanya hujavisema ambavyo vimesababisha awaze hivyo, ingawa napo haiingii akilini, hakuna mtu anayepanga kuzaa na mwenza wake kisha waachane.
Nakushauri lifanyie kwanza kazi hili la kumuweka sawa kiakili, kifikra na kimtazamo, mwanamke siyo chombo cha kutotoa watoto, anazaa kwa uchungu, anastahili heshima na siyo kila mmoja amebahatika kuzaa, anapaswa kulijua hilo pia. Hivyo mapenzi hayabebwi na mambo ya watoto, mnapendana kwanza hayo yanakuja baadaye, ndiyo maana kuna watu wanaasili watoto, kwani walipendana wakaja kubaini baadaye hawawezi kuwapata.
Muhimu pia wakati unamtafutia mshauri uishi naye kwa maarifa na weledi wa hali ya juu, ukiona anajazibika punguza kujibizana naye hasa wakati ukiwa na hedhi, kwani ni kitu asichotaka kukisikia anataka kusikia ukiwa na ujauzito.
Asipobadili msimamo wake wa kutaka mbegu yako tu atakupa shida baadaye ukija kupata mtoto, kwani kama hajafanana na wewe hatompenda.
Ananisumbua turudiane, nimeshapata mwingine
Swali: Niliachwa kwa karaha na fedheha na mwenza wangu kiasi kwamba, ilikuwa ngumu hata kujadili malumbano yaliyosababisha tuachane.
Kwa kipindi cha miaka saba tuliyokuwa kwenye mahusiano, ukiachilia miwili ambayo kila mmoja alikuwa akiishi kwake nilikuwa nusu mume, nusu mke, kwani kazi zote za nyumbani nilifanya mimi na lilikuwa ni jukumu langu, kwani zisipofanyika nitaulizwa au kununiwa.
Nakiri nilianza kumsaidia kazi baada ya kumuona yupo bize sana, kazi yake haimpi muda mwingi wa kupumzika kama ilivyo kwangu. Lakini alizidisha na kuona ni jukumu langu. Mambo yalizidi akazidi kujikweza, kunibeza, kunipandishia sauti kwa jambo dogo, mwisho akasema tuachane.
Niliomba msamaha, nilipiga magoti, nililia, niliandika ujumbe mfupi kwenye simu, ingekuwa ni kalamu ingeisha wino maana niliandika mara nyingi huku machozi yananitoka, sikuwaza kama ninaweza kupata mwanamke nikampenda na kuwa huru nikiwa naye kama huyu.
Alininyanyasa sana mpaka nikakubali yaishe, sitaki kukuambia nilipitia hali gani katika miaka miwili ya kusonga mbele bila yeye, ila jua niliumia sana.
Nikaomba kuhama kituo cha kazi kutoka hapa Dar kwenda Dodoma ilimradi nisione vitu, mahali tulipokuwa pamoja.
Nashukuru nikapata mtu mwenye sifa na tabia nizitakazo zaidi ya alivyokuwa yeye tunafanya maisha na sasa tuna mtoto.
Shetani ameanza kujitutumua, kwani mwanamke niliyeachana naye zaidi ya miaka mitano sasa ananisumbua na kutaka turudiane, kawatumia ndugu zangu, marafiki na akaja Dodoma kazini kwangu bila aibu.
Anajiliza na kujikondesha huku akiahidi hatorudia tabia zake mbaya, amejifunza na mimi ni mumewe wengine ni mahawara.
Nisaidie nifanyeje, amepata likizo kazini yupo huku Dodoma anaishi hotelini, kisa amenifuata mimi.
Dah! Umejiingiza mtegoni. Mwanamke uliyempenda na kuchukua miaka miwili kumsahau umemrudisha tena kwenye maisha yako ilhali una familia? Hili tatizo.
Kama unasema umeshasonga mbele na una familia yako nyingine huyu mpotezee kabisa, kwani alionyesha wazi hana nia na wewe. Kibaya zaidi mwanamke uliyempenda sana ni rahisi kuingia kwenye mtego wake, kwani anaujua udhaifu wako asije akautumia vibaya.
Pia unaweza kuingia kwenye migogoro na mwanamke uliyenaye sasa ambaye ni mama wa mtoto wako. Kaa mbali na huyu mtu, amejifunza ina maana miaka mitano yote alikuwa anaponda maisha alitaka ukae unamsubiri, huyu ni mbinafsi, achana naye kabisa.
Pia jifunze kuheshimu hisia za wengine, usiziumize kama zilivyoumizwa za kwako, mwenza wako akibaini haya ataumia sana na anaweza kukuchukia maisha yake yote, pengine aliamua kuacha mambo yake mengi kuwa na wewe.
Achana na mgeni kutoka Dar, akija kazini salimiana naye kisha mwambie una kazi akuache, pia unaweza usionane naye ukiamua. Kuachana si uhasama wala ugomvi, ila kwa maelezo yako alikuacha vibaya na hakujali hisia zako, kwa nini wewe ujipe shughuli ya kujali za kwake tena baada ya miaka mitano.
Hapana. Mpunguze kwenye maisha yako atakuletea shida. Nakushauri endelea na maisha yako, huyu muache na dunia yake.