Nasisitiza tasnia ya habari inahitaji Baraza Huru la Habari

Moja ya nguzo muhimu katika demokrasia ya nchi yoyote duniani ni uhuru wa vyombo vya habari, ambavyo vinatengeneza jukwaa la watu kuzungumzia mambo yao na kujua viongozi wanaowataka au waliowachagua kuwahudumia.

Siyo tu katika siasa, inakuza hata uchumi wa nchi hasa kupitia makala zinazochochea shughuli za namna hiyo kama vile kilimo na ujasiriamali ili mradi wananchi wapate taarifa sahihi.

Kutokana na umuhimu wake katika jamii, vyombo vya habari vinahitaji mazingira bora ya kuvisimamia ambayo hayataathiri uendeshaji wake wala kuzuia uhuru au uwekezaji wake katika Taifa lolote.

Hapa Tanzania tuna Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ambayo inalalamikiwa na wadau kwa sababu baadhi ya vifungu vyake vinavyokandamiza uhuru wa vyombo vya habari kwa namna tofauti.

Wadau wamechambua sheria hiyo na kubainisha vikwazo ambavyo siyo tu vinakwamisha utendaji wa vyombo vya habari, bali pia kufifisha ukuaji wa demokrasia hapa nchini hasa katika kipindi hiki cha vyama vingi.

Mfano wa vifungu hivyo ni kifungu cha tisa ambacho kinampa mamlaka Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) kufungia chombo cha habari pale anapodhani chombo husika kitakuwa kimekiuka sheria na kanuni zilizopo.

Huko nyuma, mamlaka hayo alikuwa amepewa waziri mwenye dhamana na sekta ya habari, hata hivyo baada ya sheria hii kupitishwa na Bunge mwaka 2016, mamlaka hayo yalihamishiwa kwa Mkurugenzi wa Maelezo.

Ukifanya tathmini kuhusu athari zinazojitokeza kwa kufungia gazeti, utabaini kwamba sheria hiyo ni hatarishi na inaathiri uchumi wa nchi. Ajira za watu zinapotea, serikali inapoteza mapato kutokana na kodi kwa wafanyakazi na chombo cha habari husika.

Jambo hili linapaswa kurekebishwa katika sheria kwa sababu hatutakuwa tukisubiri kauli ya Rais ili aamue tunavyotaka. Inapaswa sheria kupinga utaratibu wa vyombo vya habari kufungiwa hata kama kuna makosa yamefanyika.

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), pamoja na wadau wengine wanapendekeza kwamba mamlaka ya kuviadhibu vyombo vya habari pale vinapokiuka maadili, yakabidhiwe kwa Baraza Huru la Vyombo vya Habari.

Baraza hilo halitafanya kazi ya kufungia vyombo vya habari bali litakuwa likisikiliza mashauri kama kuna makosa ya kimaadili yamefanywa na wanahabari. Watu husika ndiyo watakuwa wakiadhibiwa huku shughuli nyingine za kihabari zikiendelea.

Utaratibu huo unafanyika pia katika mataifa mengi ambapo hakuna chombo cha habari kinafungiwa eti kwa sababu kiongozi fulani kaandikwa vibaya. Wahusika wanaadhibiwa kwa namna ambayo haihusishi kampuni husika ya habari.

Ghana ni mfano bora wa nchi zenye utaratibu huo ambapo wana Baraza la Habari ambalo limepewa jukumu la kusimamia maadili ya vyombo vya habari katika Taifa hilo. Tunapaswa kuiga kwa wenzetu.

Serikali isifanye tu kazi ya kuvidhibiti vyombo vya habari, bali pia ivilee ili vikue na ikiwezekana viwe na uwezo wa kuvuka mipaka ya nchi kama ilivyo kwa vituo vya televisheni vya Citizen (Kenya), SABC (Afrika Kusini) na The EastAfrican (Kenya).

Taifa hili linahitaji kupiga hatua kubwa katika kuongeza uhuru wa vyombo vya habari. Uhuru huo unaanzia kwenye vifungu vya sheria ambavyo ndiyo vinatoa maelekezo kwa wawekezaji, waandishi wa habari na wadau wengine.

Kama sheria haitajengwa katika misingi ya kuvutia uwekezaji au utendaji bora wa vyumba vya habari, basi hatutapata uhuru wa habari ambao Watanzania wanauhitaji katika maisha yao ya kila siku.

Serikali ambayo ni mdau namba moja katika jambo hili, ni vizuri ikasikiliza maoni ya wadau na kuyafanyia kazi kwa kina ili kuondoa mkanganyiko ambao unaleta mkwamo na kurudisha nyuma maendeleo ya tasnia ya habari.

Kitu kikubwa tunachokiona sasa ni kwamba kuna utashi wa kisiasa ambao Rais Samia aliuonyesha tangu mwanzo alipoingia madarakani. Mambo mengi yamefanyika na sasa wako kwenye hatua ya kukusanya maoni ya wadau.

Ni wajibu wetu sasa kuhakikisha kwamba tunazungumzia mambo haya ili Serikali isikie moja kwa moja kutoka kwa wadau. Maoni yetu ni muhimu kwa sababu yataiongoza Serikali katika kuyafanyia kazi mabadiliko hayo.