Namna ya kuongeza matumizi huduma za kifedha kidijitali

Utoaji huduma za kifedha kwa njia ya teknolojia au kidijitali, ni njia rahisi na haraka ya kufikisha huduma hizo kwa wateja kukidhi mahitaji yao mbalimbali. Mfano, teknolojia za pesa mtandao, benki intaneti, benki wakala, malipo kielektroniki, ili kufanikisha malipo, utoaji mikopo, taarifa za mteja, na mengineyo.
Hapa nchini, teknolojia ya pesa mtandao ambayo ni huduma za fedha zinazotolewa na makampuni ya mitandao ya simu za mkononi imekuwa chachu ya kuongezeka kasi ya matumizi ya huduma rasmi za kifedha nchini.
Kufikia Juni mwaka huu 2024, idadi ya akaunti milioni 55.7 za pesa mtandao zimesajiliwa, na jumla ya idadi ya miamala milioni 295.9 imefanyika, kwa mujibu wa Taarifa ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA.
Hata hivyo, uelewa kuhusu teknolojia ya masuala ya kifedha unahitaji kuongezwa, ili watumiaji waweze kufaidika zaidi na huduma mbalimbali kupitia majukwaa hayo, kwa mfano kuweka akiba, kupata mikopo, kupata taarifa za akaunti, huduma za bima, kulipia bili, badala ya kutumia kufanya miamala ya kutuma na kupokea pesa tu, sambamba na kuepuka visa vya watuamiaji teknolojia hizo kuingia katika mikono ya matapeli wa kimtandao, na mengine.
Serikali, taasisi za kifedha na mashirika yasiyo ya kiserikali wanaweza kushirikiana kubuni na kutekeleza mipango kuelimisha watumiaji kuhusu huduma za kifedha za kidijitali katika namna mbalimbali;
Kwanza, kuifanya elimu ya teknolojia ya fedha kuwa mtambuka na itolewe sambamba katika maudhui mbalimbali yanayolenga utoaji elimu huduma za kifedha, maudhui hayo yanaweza kujumuishwa katika mitaala ya kielimu, sambamba na kuandaa programu za mafunzo ya walimu kuwapa ujuzi unaohitajika kufundisha dhana za kifedha.
Pili, mashirika yasiyo ya kiserikali na asasi za kiraia zinaweza kubeba ajenda hiyo kwa kuendesha warsha za kielimu na kusaidia kuyafikia makundi ya kijamii, mfano watu wazima, vikundi vya ushirika, wakulima na wengineo, hususan kwa wakazi wa vijijini ambao uelewa wao kuhusu teknolojia ya fedha kidijitali unaweza kuwa mdogo zaidi.
Warsha hizo zinaweza kujumuisha mafunzo kuhusu matumizi ya simu janja, kuvinjari programu na aplikesheni za huduma za fedha, kufanya miamala, kusoma taarifa ya miamala, kulinda taarifa binafsi, na masuala mengine sambamba na hayo yanaweza kutolewa.
Tatu, teknolojia za kifedha ziongezewe lugha ya Kiswahili kurahisisha uelewa, kwa mfano katika uandaaji wa aplikesheni za benki, bima, mitandao ya simu, ikizingatiwa Watanzania wengi wanajua kusoma na kuandika zaidi kwa Kiswahili tu, na asilimia 79 ya watu nchini wanatumia Kiswahili kama lugha kuu ya kuwasiliana katika kupata huduma za kifedha, (Finscope,2023).
Mbinu kama hizo zinaweza pia kutumika kufikia makundi ya wanawake, ikilenga mahitaji yao maalumu ya kifedha na changamoto wanazokutana nazo. Kukuza ujasiriamali wa wanawake kupitia elimu ya kifedha na upatikanaji wa mikopo.
Nne, mabenki, benki na watoa huduma za pesa kwa simu, waongeze mkazo kutoa elimu ambayo ni rahisi kueleweka kuhusu mazingira salama mtandaoni, mafunzo hayo yasaidie watumiaji kuelewa jinsi ya kulinda akaunti zao, kuhifadhi taarifa binafsi na namna mbalimbali ya kutambua udanganyifu.
Hivi sasa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), inaendesha Programu ya elimu ya fedha (Financial literacy) kwa lengo ya kuongeza uelewa wa kifedha kwa jamii ya Watanzania, ni mwanzo mzuri wa kufikia tunapotaka.
Hata hivyo, kuna umuhimu wa kuongeza ushirikiano wa kitaasisi, wadau, na kuongeza mbinu za ubunifu wa kufikisha elimu hiyo kwa namna mbalimbali ili kuwafikia vizuri walengwa na kutimiza malengo yaliyokusudiwa.