Mkataba wa jezi Simba uwe na uhalisia

Jumatano iliyopita Simba iliingia mkataba mnono wa miaka mitano na kampuni ya JayRutty Investment wenye thamani ya Sh38 bilioni.
Mkataba huo unaipa haki kampuni hiyo ya kubuni, kuzalisha na kusambaza jezi na bidhaa nyingine zenye nembo ya klabu hiyo kwa kipindi hicho cha miaka mitano huku klabu hiyo kwa upande wake ikinufaika kwa kuingiza kiasi cha takribani Sh6.5 bilioni kwa mwaka.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa siku ya kuutambulisha mkataba huo, manufaa kwa Simba hayatoishia kwa kupata Sh38 bilioni pekee bali kuna ahadi nyingine za kimkataba ambazo kampuni hiyo imeahidi itazitekeleza kuanzia pale mkataba huo utakapoanza kufanya kazi.
Ahadi hizo ni kujenga uwanja wa kisasa wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 10,000 hadi 12,000, kununua basi la kisasa, kujenga ofisi za kudumu za klabu, kutengeneza studio ya kisasa kwa ajili ya kurusha maudhui ya habari.
Nyingine ambazo zimeahidiwa kutekelezwa ni kutoa kiasi cha Sh100 milioni kwa ajili ya kukuza soka la vijana, kutoa Sh100 milioni kwa maandalizi ya msimu (Pre Season) na pia watatoa kiasi cha Sh470 milioni kwa ajili ya kuongeza motisha kwa wachezaji na hiyo itakuwa kila mwaka katika kipindi cha miaka mitano.
Mashabiki wa Simba pia wameahidiwa kwamba watapata jezi na bidhaa za kisasa na za daraja la juu zenye nembo ya klabu hiyo ambazo zitabuniwa, kuzalishwa na kusambazwa na miongoni mwa kampuni kubwa ya biashara ya vifaa vya michezo duniani.
Ni jambo linalotia matumaini kuona klabu zetu zikisaini mikataba kama hiyo ya kiasi kikubwa cha fedha kinachoendana na mahitaji ya wakati uliopo na unaokuja baada ya kutofanya hivyo miaka mingi hapo nyuma.
Mpira wa kisasa unahitaji uwekezaji mkubwa wa fedha ambazo zinapatikana kupitia mikataba ya namna hiyo na ndizo zinawezesha timu kusajili wachezaji wa daraja la juu, kufanya vizuri kwenye mashindano ya ndani na nje na pia kujiendesha katika shughuli nyingine kama za utawala.
Maisha ya kutegemea fedha za kuchangishana kama ilivyokuwa zamani yameshapitwa na wakati na kwa hapa nyumbani Tanzania ni uhalisia kwamba ni vigumu kwa klabu zetu kujiendesha kwa kutegemea ada za michango za mashabiki na wanachama kwa vile viwango wanavyotozwa ni vidogo sana kuendana na uhalisia wa mahitaji ya timu zetu lakini pia hata muitikio wa kuzichangia timu umekuwa ni mdogo na klabu zimejikuta zikitumia ngumu na rasilimali nyingi kuhamasisha watu wazichangie.
Kwa sasa Simba ni miongoni mwa timu kubwa barani Afrika hivyo inapaswa kuishi maisha ya kikubwa na hilo haliwezi kutimia kama klabu haina fedha za kutosha hivyo kupitia mikataba ya namna hii, angalau wanachama na mashabiki wake wanapata ujasiri na kujitambulisha kama wao ni klabu kubwa.
Hata hivyo kusainiwa mkataba ni jambo moja na kufanikiwa kwa mkataba ni jambo lingine hivyo ili mkataba huo ambao Simba iliutambulisha Jumatano iliyopita uwe wenye tija na halisi, ni lazima pande zote mbili zitimize vipengele ambavyo vimo ndani yake.
Simba inapaswa kumlinda vyema mzabuni wake aliyeshinda tenda ya kubuni, kuzalisha na kusambaza bidhaa zenye nembo ya klabu hiyo kwa kuhamasisha mashabiki na wanachama wake kununua kwa wingi bidhaa hizo pindi zitakapoanza kuzalishwa lakini pia kumuimba katika jukwaa ili kupandisha thamani na hadhi ya kampuni hiyo.
Mzabuni huyo naye anapaswa kubuni, kuzalisha na kuzalisha bidhaa bora na kutoa fedha za mkataba kwa wakati ili kuisaidia klabu kukamilisha mipango yake mapema na kwa wakati pasipo kuyumba.
Na hiyo haipaswi kuishia kwa kutoa fedha tu au kwenye bidhaa bali pia kutimiza kwa usahihi ahadi zile nyingine ambazo amewahakikishia Simba kuwa atazishughulikia katika muda wote wa mkataba baina yao.
Ahadi ya ujenzi wa uwanja, makao makuu ya klabu, ofisi za idara ya habari pamoja na kutoa fungu kwa ajili ya kuimarisha soka la vijana kila mwaka hizi ni muhimu sana kuanza kutekelezwa mapema na sio ziishie katika makaratasi.
Hayo yakifanyika kwa usahihi, thamani na maana halisi ya mkataba huo itaonekana na kila upande utavuna matunda yake na inaweza kuvutia wadhamini wengine kwa klabu hiyo na soka letu kiujumla.
Haitopendeza kuona baadaye kunaibuka malalamiko ya upande mmoja au zote kushindwa kutekeleza vipengele vilivyomo kwenye mkataba huo kwani utashusha thamani na hadhi kwa kila upande na itatia doa soka letu.
Mkataba huo unapaswa kuwa chachu ya kuvutia zaidi udhamini kwenye soka letu badala ya kuwa sababu ya kufanya kampuni na taasisi mbalimbali kuhofia kuweka fedha zao katika mpira wa miguu Tanzania.