Simba kuwasili Zanzibar kesho maandalizi ya kuivaa Stellenbosch

Muktasari:
- Simba imetinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuitoa Al Masry ya Misri kwenye robo fainali.
Unguja. Kikosi cha Timu ya Simba, kinatarajiwa kuwasili kesho Apili 16, 2025 visiwani Zanzibar kwa ajili ya kujiandaa na kukabiliana na timu ya Stellenbosch ya Afrika Kusini katika mechi ya kwanza ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Simba itaivaa timu hiyo Jumapili Aprili 20, 2025, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar baada ya Uwanja wa Benjamin Mkapa kufungiwa kupisha ukarabati.
Akizungumza na waandishi habari leo, Aprili 15, 2025, meneja habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema timu hiyo haitaishia hapo kwani watahakikisha wanakwenda fainali ili kutimiza lengo na ndoto za kulichukua kombe la Shirikisho.
Ahmed amesema, timu hiyo ina kila sababu ya kumaliza mechi hiyo katika uwanja wa nyumbani kwani mpinzani wao yupo vizuri na hawana sababu ya kuibeza timu hiyo.
Amesema mpinzani huyo hakufika nusu fainali kwa bahati mbaya bali wana ubora na wachezaji wa Simba wanapaswa kuju ugumu wa kazi hiyo.
"Tuna kazi ya kumdhibiti na kumfunga mpinzani wetu katika uwanja wa nyumbani kwa lengo la kuimaliza kazi yetu mapema tukiwa kwetu," amesema Ahmed
Akitangaza bei za mchezo huo, Ahmed amesema VIP A Sh40,000, VIP B Sh20,000 na mzunguko ni Sh10,000 na tiketi hizo zitauzwa kuanzia leo katika vituo vyote vya kuuzia tiketi hizo.
Amewataka mashabiki wa Simba kuzidisha maombi kwa njia yake katika kuipeleka timu hiyo fainali.
"Inawezekana Simba kucheza fainali kwani timu tunayo na tumejipanga vizuri kuandika historia hiyo mwaka huu ikiwa mikononi mwetu,” amesema Ahmed.
Amewataka mashabiki kutunza amani na nidhamu katika mchezo huo ili wasilete taswira mbaya katika michuano ya CAF.