Makipa, washambuliaji Taifa Stars wanaangukia hapa

Timu yetu ya taifa ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kwa sasa ipo Morocco ambako itacheza mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya wenyeji, usiku wa kuamkia Jumatano keshokutwa.
Ni mchezo muhimu kwa Taifa Stars ambayo inashika nafasi ya tatu kwenye kundi lake E la mashindano ya kufuzu kwani inahitaji ushindi ili kuweka hai matumaini yake ya kwenda Marekani, Canada na Mexico ambako fainali za Kombe la Dunia mwakani zitafanyika.
Kumekuwa na mjadala mkubwa juu ya kikosi ambacho benchi la ufundi la Taifa Stars limekiita hasa katika nafasi ya golikipa ambayo inaonekana wameitwa wachezaji watatu ambao kundi kubwa la wadau wa mpira wa miguu lina wasiwasi nao kutokana na sababu tofauti.
Kipa Ally Salim ambaye angalau anaonekana kuwa mzoefu katika kikosi cha Taifa Stars kilichoitwa, amekuwa hapati nafasi ya kucheza katika timu yake ya klabu, Simba lakini makipa wengine wawili ambao nao wameitwa hawana uzoefu wowote na jezi ya timu ya taifa na hii ni mara ya kwanza kwao kuitwa kikosini.
Walinda mlango hao wawili ni Hussein Masalanga wa Singida Black Stars na Yakoub Suleiman wa JKT Tanzania.
Wasiwasi wa wadau haumaanishi kwamba kipa atakayepewa nafasi kikosini atafanya vibaya lakini unamaanisha kuwa timu ya taifa inahitaji kuwa na kipa chaguo la kwanza ambaye amekuwa na muendelezo wa ubora na ana nafasi ya kutosha ya kucheza katika klabu yake tena akiwa anapata ushindani wa kutosha nani na nje ya nchi.
Lakini hilo kwa sasa limekuwa gumu na linaonekana kuliumiza kichwa benchi la ufundi la Taifa Stars chini ya Hemed Morocco.
Na changamoto hiyo haionekani kwa wachezaji wa nafasi ya kipa tu bali hata ile ya mshambuliaji wa kati, hivi sasa hakuna wachezaji wazawa kwenye ligi yetu ambao wanaweza kulipa uhakika benchi la ufundi la Taifa Stars katika kuipatia mabao.
Udhaifu huu kwa namna moja au nyingine unachangiwa na klabu nyingi zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kukosa wachezaji wazuri na mahiri wa nafasi hizo.
Mchezaji bora anatengenezwa katika viwanja vya mazoezi na katika mechi ni vigumu hilo kufanyika, zaidi inakuwa ni jukwaa la mchezaji kuonyesha ubora wake na kile alichokivuna mazoezini.
Hivyo tusitegemee kuona tutakuwa na makipa au washambuliaji wazuri katika mechi wakati huo hakuna walichokifanya kwenye programu ya mazoezi.
Kipa ili awe na kiwango bora na chenye muendelezo anapaswa kukutana mara kwa mara na wachezaji bora wa nafasi za ushambuliaji na hilo linapaswa kufanyika kwa washambulizi ambao nao wanapaswa kukutana na mabeki na makipa mahiri.
Changamoto za washambuliaji wazuri mazoezini zitampa fursa kipa ya kuonyesha udhaifu wake na kisha kuufanyia kazi hivyo kumuweka katika mazingira mazuri ya kufanya vyema katika mechi lakini kama hakutani nao huko, atategemea maajabu na bahati tu ili kutamba katika mechi.
Kwa mshambuliaji kucheza mara kwa mara mazoezini na safu ngumu ya ulinzi, zitamuimarisha na kumfanya awe na urafiki na nyavu na maana yake ubora huo atauhamishia katika mechi.
Tutazame mfano wa makipa Moussa Camara wa Simba na Djigui Diarra wa Yanga ambao kwa hivi sasa hapana shaka yoyote ndio makipa bora zaidi waliopo katika ligi yetu.
Camara ambaye anaongoza kwa kucheza idadi kubwa ya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa, katika mazoezi ya Simba anakutana na Leonel Ateba, Charles Ahoua na Steven Mukwala ambao wote wana takwimu nzuri za ufungaji kwenye ligi.
Ahoua ni kinara wa ufungaji katika ligi akiwa na mabao 12, Steven Mukwala amepachika mabao tisa na Leonel Ateba amefumania nyavu mara nane.
Kwa upande wa Yanga, Diarra naye mara kwa mara katika mazoezi anakutana na wachezaji watatu tishio kwa kufunga mabao kwenye Ligi Kuu msimu huu ambao ni Clement Mzize, Prince Dube na Stephane Aziz Ki.
Dube na Mzize kila mmoja hadi sasa amefumania nyavu mara 10 kwenye ligi wakati huo Stephane Aziz Ki akifunga mabao saba.
Kama kina Diarra na Camara wanajiandaa kukabiliana na kina Aziz Ki, Ateba, Mukwala, Dube, Mzize na Ahoua mara kwa mara, haiwezi kuwa ngumu kwao kufanya hicho wanachokionyesha kwenye mechi za mashindano.
Ni kama ilivyo kwa viungo na washambuliaji hao ambao haiwezi kuwa ngumu kuwafunga makipa wa timu nyingine wakati tayari wameshakutana na ugumu mbele ya kina Camara na Diarra.