Majimbo yagawiwe kutokana na uhitaji

Jaji Jacobs Mwambegele
Mchakato wa kugawa na kubadili majimbo ya uchaguzi unaoendeshwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ni hatua muhimu, ikifanyika kwa mustakabali wa demokrasia nchini.
Kama ilivyotangazwa, INEC imeanza mchakato huo, huku wananchi wakipewa nafasi ya kutoa maoni yao kuhusu mpango huu.
Mchakato huu unahitaji umakini mkubwa kutoka kwa wadau wa siasa, wanasheria na wananchi ili kuhakikisha lengo lake la kuboresha uwakilishi linafanikiwa bila upendeleo wa kisiasa.
Kama ilivyoelezwa na Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele, mchakato huu ni utekelezaji wa kifungu cha 74(6)(c) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kinachoitaka Tume kuufanya angalau kila baada ya miaka 10.
Kwa kuwa suala hili limekuwa na malalamiko mengi, ni muhimu majimbo haya yakagawanywa kwa kuzingatia idadi ya watu na si kwa misingi ya kisiasa au kijiografia, ili kuyanufaisha makundi au wagombea fulani.
INEC inapaswa kuhakikisha mapendekezo yatakayowasilishwa ni yale yatakayosaidia kuboresha uwakilishi wa wananchi bila kutumika kwa masilahi ya kisiasa ya makundi fulani.
Huu ni wakati muhimu kwa Tanzania kuonyesha mabadiliko ya kimuundo katika uwakilishi wa kisiasa na kuhakikisha mchakato huu unafuata misingi ya sheria na Katiba. Kwa sasa, nchini kuwa majimbo 264, kati ya hayo 214 yapo Tanzania Bara na 50 Zanzibar.
Ingawa idadi ya majimbo haijabadilika kwa miaka mingi, kuna mjadala mkubwa kuhusu uwiano wa idadi ya watu katika majimbo mbalimbali, kwa kuwa mengine, hasa ya mijini, yana idadi kubwa ya watu ikilinganishwa na yale ya vijijini.
Hali hiyo, imekuwa ni changamoto kubwa kwa kuhakikisha kuwa kila raia anapata uwakilishi wa haki bungeni.
Hivyo, inapaswa kufanyika mabadiliko ya kimaendeleo kwa kuzingatia idadi ya watu, badala ya kuangalia tu ukubwa wa eneo au changamoto nyingine za kijiografia.
Licha ya kutolewa mwezi mmoja wa kutoa mapendekezo hayo, tunatambua mchakato wa kugawa na kubadili majina majimbo unahusisha hatua nyingi na nyeti kwa mustakabali wa uwakilishi wa wananchi bungeni, ikiwamo hali ya kiuchumi.
Hata mazingira ya mchakato wa ukusanyaji maoni yanaweza kuwa kikwazo kwa kuwa hayawezeshi wadau wengi kushiriki, badala yake ikawa rahisi kukuta upande mmoja wa kiitikadi ndio unaonufaika, achilia mbali suala la muda ambalo pia limeibuliwa na wadau.
INEC, kama ilivyoelezwa na wadau ilipaswa kufanya mabadiliko haya mapema ili kutoa fursa zaidi kwa wananchi kushiriki kikamilifu.
Maelezo hayo yanaakisi kwamba, baadhi ya mabadiliko ya kisiasa yanaweza kuwa na madhara kwa uchaguzi, hasa kama mchakato husika haukutekelezwa kwa ufanisi.
Ni wazi kuwa, mchakato wa kugawa majimbo unahitaji kuendeshwa kwa umakini ili kuhakikisha masilahi ya wananchi yanayopewa kipaumbele.
Hii ni fursa ya kipekee ya kuboresha demokrasia, lakini ni muhimu kuhakikisha kila hatua ya mchakato inazingatia kanuni za haki na uwazi.
Mchakato wa kugawa majimbo ni muhimu kwa demokrasia ya Tanzania, lakini ili ufanikiwe, unahitaji umakini, uwazi na ushirikishwaji wa wananchi.