Mahitaji ya msingi ya biashara changa
Chiraka Muhura
Muktasari:
Biashara inatakiwa kuwa sehemu ambayo kuna mzunguko mkubwa wa watu na sehemu ambayo inafikika kiurahisi. Biashara iliyojificha au ambayo iko mahali ambapo si rahisi kufikika itakosa wateja na matokeo yake inaweza kufa. Mjasiriamali anatakiwa kupata eneo la biashara lenye bei nafuu ili aweze kupata faida ya kutosha katika kukuza biashara yake.
Biashara inayoanza (biashara changa) ni tofauti kabisa na ile inayokua au iliyokua.Mahitaji ya msingi ya biashara hizi katika mchakato wa hatua za maendeleo yake, ndivyo vitu muhimu vinavyotofautisha biashara moja iliyo katika hatua ya mwanzo dhidi ya ile iliyo katika hatua ya pili au ya tatu.
Biashara changa ni aina ya biashara ambayo iko katika hatua za awali za uendeshaji wake. Hii ni hatua ngumu katika biashara, kwani haina tofauti sana na mtoto mchanga ambaye anahitaji matunzo ya hali ya juu ili aweze kukua au kukua vizuri.
Katika biashara changa, mjasirimali anatakiwa kufanya mambo muhimu yafuatayo: kwanza anatakiwa kutafuta wateja wa bidhaa au huduma husika ili kujua ukubwa wa soko la biashara zake ikiwa ni pamoja na kujua mahali ambako wateja wake wanapatikana.
Kutafuta wateja si jambo rahisi kwani ni sawa na kumshawishi mtu asiyekujua ili aweze kukupatia kile unachohitaji kutoka kwake.
Pamoja na ukweli kuwa mjasirimali anatakiwa kuwa na uwezo wa kujua wateja wake, anatakiwa kujua ukubwa wa soko la bidhaa au huduma zake na kubaini mbinu mbalimbali anazoweza kuzitumia katika kuingia sokoni kwa mafanikio. Kwa mfano anapaswa kuangalia bei atakayotoza wateja wake, namna atakavyofanya bidhaa zake zijulikane kwa kutangaza katika vyombo mbalimbali vya habari, kutumia vipeperushi na kwa kunadi bidhaa/huduma husika ana kwa ana.
Mjasiriamali anatakiwa kuwa na mtaji unaotosheleza mahitaji ya biashara yake. Mtaji wa biashara ni pamoja na mali isiyohamishika na gharama za moja kwa moja zinazotumika katika biashara kama vile kununua bidhaa, kulipia pango la nyumba ya biashara, kulipa wafanyakazi, kufanya matangazo ambayo ni muhimu sana katika biashara kwani biashara ni matangazo.
Mtaji wa biashara unaweza kupatikana kwa njia mbalimbali kama vile kukopa kutoka katika taasisi za fedha, kujiwekea akiba au kutoka kwa familia au marafiki.
Mjasirimali anatakiwa kuwa na eneo zuri la kufanyia biashara ili kuvutia wateja.
Biashara inatakiwa kuwa sehemu ambayo kuna mzunguko mkubwa wa watu na sehemu ambayo inafikika kiurahisi. Biashara iliyojificha au ambayo iko mahali ambapo si rahisi kufikika itakosa wateja na matokeo yake inaweza kufa. Mjasiriamali anatakiwa kupata eneo la biashara lenye bei nafuu ili aweze kupata faida ya kutosha katika kukuza biashara yake.
Kimsingi maeneo mazuri ya kufanyia biashara huwa ni ghali, hii haina maana kuwa mjasiriamali mdogo hawezi kupata eneo ambalo lina nafuu kidogo.
Kwa mfano, badala ya kupanga kwenye chumba kikubwa cha biashara, anaweza kuchagua chumba kidogo kama sehemu ya kuanzia na biashara itakavyozidi kukua ndivyo atakavyozidi kuwa na eneo pana la biashara yake.
Mjasiriamali anatakiwa kuwa na mpango wa biashara utakaomwongoza katika biashara hiyo ikiwa ni pamoja na kumsaidia katika kupata mtaji kutoka katika taasisi za kifedha kama itamlazimu kufanya hivyo. Mpango wa biashara unashauriwa uwe katika maandishi na wenye kuelezea hali halisi ya biashara husika.
Mjasirimali anatakiwa kuwa na vyeti na leseni za biashara kutoka katika mamlaka za biashara kama vile cheti cha jina la biashara, cheti cha mlipa kodi na leseni ya biashara kutoka manispaa au halmashauri za wilaya/mji/jiji ikiwa ni pamoja na mamlaka nyingine zinazohusiana na biashara husika.
Mwandishi wa makala haya ni mtaalamu wa ujasiriamali na mtunzi wa vitabu
0755 526 958 / 0714 631 110