Kwa nini sikukuu zimepungua utamu siku hizi?

Muktasari:

  • Jibu rahisi na la uhakika zaidi; ni kwa sababu huna hela. Jiulize hiyo zamani unayosema sikukuu zilikuwa tamu kuliko siku hizi ulikuwa ni nani kwenye familia? Ulikuwa baba au mtoto?

Jibu rahisi na la uhakika zaidi; ni kwa sababu huna hela. Jiulize hiyo zamani unayosema sikukuu zilikuwa tamu kuliko siku hizi ulikuwa ni nani kwenye familia? Ulikuwa baba au mtoto?

Kama ulikuwa baba na bado unasema sikukuu zilikuwa nzuri kuliko siku hizi, wewe sio mwenzetu na tatizo lako hatuliwezi, labda utafute daktari bingwa.

Lakini kama unasema ulikuwa mtoto, basi nina uhakika tayari jibu unalo, hiyo ndiyo sababu ya sikukuu kuwa tamu kuliko enzi hizi.

Sikukuu inahitaji pesa, wote tunakubaliana na hili. Kuanzia chakula nyumbani, mavazi ya watoto, mitoko ya sikukuu, kupokea wageni na mengine mengi na yote haya huwezi kuyafanya kama umefulia. Na katika familia, anayetegemewa zaidi kuleta pesa ya makorokoro yote haya ni nani? Ni baba.

Kwa hiyo zamani ulikuwa unakula pilau lenye nyama nyingi na kachumbari kwa jasho la mzee wako. Unavaa nguo nzuri mpya kwa pesa ya baba yako, unakwenda mtoko kwa juhudi za baba, mwenyewe hukuwa na presha kabisa.

Kinachotokea sasa hivi ni kwamba meza imepinduka, wewe ndiye baba unayetakiwa kuwanunulia watoto nguo za sikukuu na kuhakikisha nyumbani inapikwa pilau ya kuku.

Wewe ndiye unayetakiwa kuhakikisha watoto wana nguo za sikukuu, wameenda kutembea na kuwafanya watoto wasijisikie wanyonge msimu huu wa sikukuu.

Kama hiyo haitoishi, wakimaliza sikukuu tu zinabaki siku mbili tatu wanatakiwa kurudi shule, huko nako unatakiwa ulipe ada ununue na vifaa vya shule na hiyo yote ni pesa.

Hujakaa sawa, unakumbuka kuwa Januari hiyo hiyo unayolipa ada baada ya kumaliza kugharamika na sikukuu, pia unatakiwa ulipe kodi ya nyumba. Majukumu yote haya yanategemea mfuko wako, yote yanategemea pesa yako; sasa niambie kwa msururu wa majukumu namna hii unadhani utawezaje kuuona uzuri wa sikukuu?

Mwanamume ukishakuwa mkubwa msimu wa sikukuu kwako ni kama kiama, hasa usipokuwa umejipanga vizuri.

Kwa hiyo kaa ukijua sikukuu ni ileile kila mwaka. Inasherehekewa kwa sababu zile zile kila mwaka. Kinachobadilika ni mfuko wako na ndiyo kinachoamua kama uione sikukuu ni nzuri au mbaya, imepoa au imechangamka.

Na ndiyo maana tunasema kuwa mwanamume ni tabu. Kwanza unakosa hela ya kusherehekea sikukuu kwa namna unayotaka, pili unatakiwa utafute sababu za kuwaaminisha watu kwamba siku hizi sikukuu imepoa sio kwa sababu huna hela, bali ni kwa sababu zama zimebadilika.

Lakini sisi wenyewe tunaelewana. Tukisikia maelezo mengi tunajua hapa mwenzetu ndio vile tena.


Nawatakia Krismasi njema na Mwaka Mpya wenye heri tele.