Kutoyajali mabadiliko ya tabianchi kutatugharimu

Mabadiliko ya tabianchi ni suala linalozidi kuwa tishio kubwa kwa ulimwengu, na athari zake zinaonekana wazi katika maeneo mengi duniani. Hata hivyo, licha ya madhara yake, bado kuna mtindo wa kutokujali au kupuuza athari zake miongoni mwa Watanzania.
Sababu kubwa ya Watanzania kutokujali athari za mabadiliko ya tabianchi ni uelewa mdogo kuhusu suala hili.
Hii ni kutokana na kukosekana kwa elimu ya kutosha juu ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi na umuhimu wa kuchukua hatua mapema.
Katika maeneo mengi uzoefu unaonyesha watu wengi hawana ufahamu wa wazi kuhusu mabadiliko haya, hivyo wanadhani ni suala linalohusiana na siasa za kimataifa.
Hali hii inachangia kupuuza athari za tabianchi na kutochukua hatua za kupunguza madhara yanayoweza kutokea.
Nikionacho, kuna tatizo la ukosefu wa uongozi bora katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi. Viongozi wengi hawana mkakati madhubuti wa kupambana na changamoto hii.
Badala ya kuweka sera na mipango thabiti ya kulinda mazingira, mara nyingi tunashuhudia mipango inayolenga maslahi ya muda mfupi,
Mabadiliko ya tabianchi ni tishio kubwa kwa mazingira, lakini matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali za asili pia ni mojawapo ya vyanzo vikubwa vya mabadiliko haya.
Wakati mwingine, kwa kutokujali, wananchi hutumia rasilimali kama vile misitu na maji kwa njia isiyozingatia uhifadhi wa mazingira.
Uharibifu wa misitu, uchomaji moto wa magogo kwa ajili ya kilimo, na uchimbaji wa madini bila kuzingatia utunzaji wa mazingira, ni baadhi ya mifano ya matumizi mabaya ya rasilimali zinazochangia mabadiliko ya tabianchi.
Kwa wananchi wengi hasa wa vijijini, maisha ni magumu na changamoto za kiuchumi zinawafanya washughulike zaidi na kutatua matatizo ya kila siku kama vile chakula, makazi, na huduma za msingi.
Hali hii inawafanya wengi kuona masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi kama jambo la pili au la tatu, kuliko changamoto za kimsingi wanazokutana nazo kila siku.
Kwa mfano, wakulima wanapokutana na ukame au mvua zisizozalisha mazao bora, hawazingatii mabadiliko ya tabianchi kama sababu ya tatizo hili, bali wanachukulia kama mabadiliko ya kawaida ya hali ya hewa.
Ingawa baadhi ya Watanzania wenye uelewa, wanakubali kwamba mabadiliko ya tabianchi ni tatizo kubwa duniani, bado kuna mtazamo wa kuona kama ni changamoto inayowahusu zaidi nchi zilizoendelea.
Ushawishi wa baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii pia unachangia kuendeleza mtazamo huu.
Wapo wanaomini kwamba athari za mabadiliko ya tabianchi, kama vile joto kupanda na mabadiliko ya mvua, ni matokeo ya shughuli za viwanda katika nchi za dunia ya kwanza, na kwa hivyo wao hawahitaji kuchukua hatua yoyote.
Kiuhalisia kwamba mabadiliko ya tabianchi yanatokea katika maeneo yote ya dunia, ikiwamo nchi yetu na athari zake ni majinuni pekee anayeweza kuzikana.
Hivi nani kwa mfano leo hii hashuhudii matukio ya ukame wa mara kwa mara katika maeneo mengi nchini, au hata mafuriko yanayosababisha uharibifu mkubwa?
Tuendelee kutojali, lakini madhara yake hayatabagua mtu au kundi. Sote kama taifa tutakuwa waathirika wa hali hiyo.
Kwa kutokujali athari za mabadiliko ya tabianchi, tunajiweka katika hatari kubwa ya kupoteza rasilimali muhimu na uharibifu wa mazingira unaoweza kudhoofisha uchumi wetu na ustawi wa jamii.
Ili kujiepusha na madhara hayo, ni muhimu kubadilisha mtindo wa maisha, kuwekeza katika elimu ya mazingira, na kuchukua hatua madhubuti katika kutunza mazingira.
Hilo linajumuisha pia kupitia sera za kitaifa zinazolenga kupunguza uzalishaji wa gesi chafu, uhifadhi wa misitu, na matumizi bora ya ardhi.
Kila mmoja anapaswa kufahamu kwamba mabadiliko ya tabianchi si suala la nchi fulanifulani hasa zilizoendelea.
Ni wajibu wetu sote, Serikali, wananchi, na taasisi mbalimbali, kuchukua hatua za haraka za kupunguza athari za mabadiliko haya.
Hilo linaweza kufanyika kupitia elimu kwa umma, sera bora, na juhudi za pamoja zitakazotuwezesha kujenga taifa linaloweza kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha mustakabali mzuri kwa vizazi vijavyo.