Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kliniki ya kero za walimu ilitazame hili

Januari 15, 2019, aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli alitoa agizo kwa aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii wakati huo, Dk Hamisi Kigwangala kusitisha kuondolewa kwa baadhi ya vitongoji na vijiji vilivyokuwa ndani ya hifadhi.

Ni kutokana na agizo hilo, Rais aliwaagiza mawaziri nane wa kisekta kupitia maeneo yote nchini na kujiridhisha juu ya migogoro ya wananchi na hifadhi, yakiwamo mapori yaliyotengwa zamani ili ikibidi wamalize kwa njia ya staha.

Mikoa mingi ilipitiwa, vijiji vikapitiwa, wengi walipata nafasi ya kuhojiwa juu ya nini wangetaka kifanyike.

Baadhi yao walipata kile kilichoonekana kuwa ni ahueni, licha ya ukweli kuwa siyo wote walifanikiwa kama ilivyokuwa.

Hata hivyo, licha ya mafanikio mengi, kulikuwa changamoto ikiwemo ya kutokufika maeneo husika kwenye migogoro, kwani baadhi walikuwa wakiishia kwenye ofisi za wakuu wa mikoa na wilaya.

Maamuzi hayo na ziara hizo zinaweza kufanana na hiki kinachoendelea kwa sasa nchini kwenye mpango uliopewa jina la Samia Teachers Mobile Clinic ulioasisiwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na kupata baraka za Serikali.

Mpango huo ni wa viongozi wa CWT kuwatembelea walimu kwenye maeneo yao ya kazi wakishirikiana na Ofisi ya Rais Utumishi, Ofisi ya Rais Tamisemi, Tume ya Utumishi wa Walimu na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Madhumuni makubwa ya mpango huo ni kutafuta njia bora ya kuondoa na kumaliza changamoto zinazowakabili walimu ikiwemo madaraja, madai ya malimbikizo ya mishahara na manyanyaso wanayopata walimu kazini.

Natambua Samia Teachers Mobile Clinic ilishapita karibu mikoa 13 na kuzungumza na makundi makubwa ya walimu, lakini neema ni kama inawafikia walimu waliopo karibu na miji ambao hata ufuatiliaji wa haki zao huwa hawatumii gharama kubwa kuwafikia wakurugenzi.

Waliofikiwa na kampeni hiyo wanapongeza kuwa inasaidia kwani inawapa nafasi ya kusikilizwa na kupewa ushauri inapobidi au kuonyeshewa njia ya kupita ili kufikia malengo au kumaliza matatizo yao papo kwa hapo kama inawezakana.

Siku chache zilizopita timu hiyo ilikuwa mkoani Iringa ilikopokelewa na Katibu Tawala wa mkoa huo Doris Ntuli Kalasa ambaye aliisifu kampeni hiyo kwamba inakwenda kuongeza ari na motisha wa utekelezaji wa majukumu ya walimu na hatimaye kuongeza ufaulu katika masomo ya wanafunzi.

Kalasa alimwaga pongezi kwa ubunifu huo na kusisitiza jambo hilo lazima lipewe uzito unaotakiwa, ikiwemo kuwafikia walimu wengi zaidi hasa wanaofanya kazi maeneo ya vijijini ambako kunatajwa kuwa na kilio kikubwa.

Mambo manne yanapaswa kutazamwa, nayo ni nani wanafikiwa? Je, wahusika halisi wanafikiwa, kwa njia ipi wanafikiwa? Je, hao ambao wamekosa nafasi ya kukutana na timu hiyo inakuwaje?

Mfano katika mkoa wa Kigoma kliniki hiyo ilikita kambi eneo moja la mkoani na kuwataka walimu kusafiri kwenda kuwafuata mahali pamoja bila kujali mazingira na umbali ambao walimu wanatoka na gharama wanazotumia kuifuata huduma hiyo.

Ni wazi kuwa, lengo ni jema lakini utekelezaji wake hauwezi kuwa na mantiki kama inavyokusudiwa kwani taarifa zitaandikwa kuwa kazi imefanyika, lakini kwenye uhalisia bado kunakuwa na kilio kwa maeneo ambayo wamepitia na hivyo baadhi ya walimu kuchelewa kupata haki zao.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari na Uhusiano wa CWT Juma Dedu, baadhi ya Wilaya wanashindwa kuzifikia kutokana na changamoto za kimazingira huku akitaja muda mfupi walionao kwenye kampeni hiyo.

Hilo ni tatizo linalozua swali, je kama wenye magari na posho za kulipwa kwenye kampeni wanashindwa kufika baadhi ya maeneo, itakuwaje kwa walimu ambao wengine wana zaidi ya miaka 10 kazini lakini hawajafika mkoani?

Ipo haja ya kuangalia kwenye jambo hili ili kuondoa mpango wa kuwagawa walimu kwa makundi kama ambavyo inaanza kutafsirika.

Kuna walimu wanaishi Mungu nihurumie. Mishahara wanayoipata sehemu kubwa inaishia kwenye mikopo ya benki na kausha damu.

Walimu wa aina hiyo kutoa nauli zaidi ya Sh15,000 ya kwenda na nyingine kama hiyo kurudi kituoni kwake mbali na chakula na malipo ya nyumba ya kulala wageni, ni kitu cha kawaida. Ndio hawa huishia kusema afadhali kukaa ili kusubiri neema nyingine.

Wenzetu wa CWT watumie njia nyingine kutafuta namna bora ya kuwafikia walimu wa vijijini ambao kwa sehemu kubwa wanatajwa kuwa na changamoto lakini nyingi zinatokana na waajiri ama viongozi wanaowasimamia ambao ni vigumu pia kuwapa ruhusa ya kwenda mijini kuonana na timu hiyo.