Kile apandacho mtu ndicho atakivuna

Bwana Yesu asifiwe,
Karibu katika tafakari ya ujumbe wa leo unaosema, “Kile apandacho mtu ndicho atakachovuna” Maombolezo 5:7 inasema Baba zetu walitenda dhambi hata hawako; na sisi tumeyachukua maovu yao”. Kuna mambo mengi tumefanya sirini na hakuna hata mmoja anayefahamu ni wewe peke yako unajua, hujawahi sema kwa yeyote na ukute huna hata mpango wa kesema.
Ndugu yangu hiyo ni mbegu ulipanda muda ukifika itachipua, itakua, itazaa na matunda yake utayaona! Tatizo ni kwamba madhara yake unaweza usiyapate wewe watakaoathilika ni vizazi vyako. Mungu atuhurumie sana.
Kuna watu wanadhani wanaweza kupanda mchicha na kuvuna ufuta, au kupanda mahindi halafu wakavuna matembele, kwa hakika jambo kama hilo haliwezekani kabisa. Galatia 6:7 neno la Mungu linasema “Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa chochote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.”
Mpendwa kila unalofanya lina pande mbili tu, laweza kuwa zuri au baya nikwambie tu mbegu unayopanda kwa kujua au kwa kutokujua ipo siku utavuna, na usipovuna wewe basi wanao au wajukuu au vitukuu watavuna matunda yake. Kutoka 20:5b anasema “Kwa kuwa mimi, Bwana Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukizao”.
Mwanzo 12:11-13 Ni habari za Ibrahimu, alidanganya kuwa Sarai si mkewe (mbegu ya uongo). Uongo huu Ibrahimu hakukumbuka kuutumbia ndio maana tunamuona mwanae pia Isaka akidanganya kuwa Rebeka si mkewe. Mwanzo 26:7. Sielewi ni mambo mangapi ndugu yangu umefanya na hujawahi kuyatubia yamkini umeokoka kabisa lakini hujawahi kuchukulia jambo hilo kama linaweza kuwa kikwazo kwako au kwa uzao wako Mungu akupe neema ya kutambua kuwa unalojambo la kufanya ili kufanya mambo yaende vizuri.
Tunayo mifano mingi sana kwenye jamii zetu, hebu jaribu kuchunguza watu watano waliooa au kuolewa wakiwa tayari na watoto, ukichunguza kwa makini utangundua kuwa watoto wao wamezalia nyumba kama ni mabinti na kama kijana hajaleta mtoto nyumbani basi fahamu kuwa sketi haikatizi.
Wazazi tumekimbilia kuwaadhibu na pengine kuwafukuza bila kujitathimini enzi za ujana wetu tulikuwaje, mpendwa mwanao hana shida, shida iko kwako, rudi magotini tubu dhambi hiyo ya uzinzi ili ujiokoe wewe na uzao wako na ujue haitoishia kwa mwanao hadi mjukuu. Kuna kajukuu ukikaangalia unajikuta unasema yaani huyu ni babu/baba yake mtupu! (vijitabia vyake). Ezekiel 16:14 inasema “Kama mama ya mtu alivyo ndivyo alivyo binti yake”.
Kwa upande mwingine tunaweza kusema kama baba ya mtu alivyo ndivyo alivyo kijana wake. Angalizo ni kwamba usijihesabie haki kwani mtoto anaweza rithi tabia ya baba au ya mama hivyo omba sana Mungu mithali hii isitumike kwako. Mpendwa wangu, haijarishi tumekosea kiasi gani, tunapotubu Mungu husamehe na kutusafisha kabisa, hujachelewa wakati wa wokovu wako na uzao wako ni sasa.
Zaburi 126:6. Ingawa mtu anakwenda zake akilia, azichukuapo mbegu za kupanda. Hakika atarudi kwa kelele za furaha,Aichukuapo miganda yake. Bwana Yesu asifiwe! Ukipanda wema utavuna wema, yale mambo mazuri yote unayotenda ni mbegu unapanda na jambo la kushangaza ni kwamba unaweza usifurahie matunda ya yale mazuri uliyotenda, huenda umesaidia watu wengi, umejitoa kuliko kawaidia lakini ukikaa na kutathmini wale uliowatendea wamenyamanza kana kwamba hujawahi fanya lolote kwao au kwa familia zao, wakati mwingine hakuna hata asante badala yake unaweza kutana na kashfa au masimango. Nikutie moyo kuwa usichoke kutenda mema kwani muda utazungumza, Mungu atakulipa kwa njia usiyotarajia.
2Samweli:9:1-7, Ni habari za Daudi na Yonathani, walipendana sana na kutendeana mema, Yonathani alikuwa tayari kwenda kinyume na baba yake ili tu kumuokoa rafiki yake Daudi na wacha nikwambie kitu wakati Yonathani anafanya yote haya hakufanya ili aje alipwe, lakini baada ya Sauli na yeye kufariki, Daudi anarudi na kuuliza “Je, Amesalia mtu mmoja katika nyumba ya Sauli nipate kumtendea mema kwa ajili ya Yonathani?”
Mefibosethi mwana wa Yonathani anapata kibali cha kula mezani pa mfalme, anakula matunda ya wema aliotenda baba yake. Ni nini umefanya wewe katika jamii yako ambacho ni alama hata wakati wewe umetwaliwa bado uzao wako utakumbukwa. Kuna wale tumetenda wema na sasa hatuoni faida bali tunahesabu hasara, nikutie moyo usichoke uwe na moyo mkuu Mungu hawezi kukusahau wewe na uzao wako. Ni maombi yangu siku ya leo kuwa huyu Mungu aliyekupa kibali cha kusoma ujumbe huu, akupe neema ya kutambua ni mbegu gani umekuwa ukipanda au ulipanda miaka ya nyuma huenda ni uzinzi, uongo, chuki, umbea, yamkini ulitamka maneno mabaya kwa wanao au mkeo/mumeo na hukuwahi kutubu, Roho Mtakatifu akukumbushe ili ufanye toba. Muda wa wokovu ni sasa, usiwe mkaidi. Okoa uzao wako.
Kwa maombi, semina na ushauri.
Mwalimu Peace Marino anapatikana KKKT Usharika wa Ebeneza Nyashimo, Busega mkoani Simiyu.
0783999044