Kiini cha lawama ajali ya Precision Bukoba

Muktasari:

  • Ajali ya ndege ya Shirika la Precision Air imeleta maumivu, lawama na mshangao. Ilizama asubuhi Novemba 6, 2022 katika Ziwa Victoria mjini Bukoba na watu 19 wakapoteza maisha, 24 wakaokolewa.

Ajali ya ndege ya Shirika la Precision Air imeleta maumivu, lawama na mshangao. Ilizama asubuhi Novemba 6, 2022 katika Ziwa Victoria mjini Bukoba na watu 19 wakapoteza maisha, 24 wakaokolewa.

Maumivu? Ndiyo, inaumiza sana kupoteza watu unaowapenda. Familia zimeagana jumla na ndugu zao ghafla. Taasisi mbalimbali zimepoteza wafanyakazi mahiri na tegemeo. Taifa limeondokewa na nguvu kazi. Nchi ipo msibani.

Kwa nini ajali na ikawaje watu 19 hawakuokolewa wakati ndege ilitumbukia ziwani takribani mita 100 kutoka nchi kavu? Maswali hayo ndiyo yanatuleta kwenye mshangao na lawama.

Mshangao? Bila shaka, mpaka sasa Watanzania kwa wingi wao kila mmoja anazungumza lake. Wanajiuliza kama ajali imetokea jirani na uwanja wa ndege wa Bukoba, kweli ndani ya uwanja hakuna wataalamu wala vifaa vya uokoaji?

Tanzania imeona na dunia imeshuhudia, watu wa kawaida wakiwemo wavuvi ndio walijitosa majini na kuokoa watu 22.

Hakukuwa na vikosi wala vifaa vya uokoaji vilivyonunuliwa kwa kodi za wananchi. Ni mshangao!

Lawama? Naam, lini kama Taifa itawezekana kujenga umahiri wa kukabili ajali hasa za majini? Ikiwa uokoaji umeshindikana ndege ikiwa karibu, hali ingekuwaje kama itakuwa umbali mrefu?

Utashangaa pia kuona nchi yenye vikosi vya uokoji lakini havionekani katika mazingira ya uokoaji badala yake wanaookoa watu ni wananchi wasio na elimu wala mafunzo ya kuokoa.

Kisha, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akaagiza wavuvi na wananchi walioshiriki kwa moyo mkubwa uokoaji, wapewe mafunzo maalumu ya uokoaji.

Hili ni jambo jema, elimu haijawahi kukosa manufaa, hata hivyo, agizo limezingatia kwamba ajali haina siku wala saa?


Tuangalie ajali yenyewe

Nilipoona picha za video na mnato, ndege ikiwa kwenye maji, kwa haraka nikajua ni ‘ditching’, yaani utuaji wa ndege kwenye maji kwa dharura.

Wataalamu wa usafiri wa anga hutafsiri kuwa hilo ni tendo japokuwa ni la hatari, pia lina manufaa. Ndege ya US Airways 1549 ilitua kwenye Mto Hudson, New York, Julai 15, 2009 na watu 155 waliokuwemo waliokolewa na kufanya ‘muujiza’ (Miracle On The Hudson). Ni miujiza kwa kuwa watu wote kwenye ndege walipona.

Ndege hiyo ilikuwa inatoka Uwanja wa Ndege wa LaGuardia, New York, ikielekea Charlotte na Seattle, injini zote mbili zilifeli rubani akaipeleka mtoni. Abiria na wafanyakazi waliokolewa na majeruhi walikuwa wachache, wenye majeraha kidogo.

Hivyo, hata kama ingekuwa rubani wa Precision aliamua kutua majini kwa dharura na kwa kuzingatia athari zake kitaalamu, haikuwa sawa kupoteza watu 19 kwa umbali ule mdogo kutoka nchi kavu.

Kila uwanja wa ndege unapaswa kuwa na vifaa na wataalamu wa uokoaji. Na hufanya mazoezi mbalimbali ya utayari. Uwanja wa ndege Bukoba walishaendesha mazoezi mengi ya ndege kuzama Ziwa Victoria na kuokoa lakini siku ya tukio hali ikawa tofauti.

Mei 21, 1996 Meli ya MV Bukoba ilizama ikiwa inakaribia Bandari ya Mwanza. Watu takribani 900 walifariki dunia. Malalamiko ni kuwa uwezo wa uokoaji na uamuzi wa kuitoboa meli kwa juu, ni sababu ya kupoteza watu wengi ambao inadhaniwa walikuwa wazima.

Malalamiko ya wengi yalibeba hisia kuwa mahali Mv Bukoba ilipozama, palikuwa karibu na bandari (kilometa 8), ambapo kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kuokoa watu wengi, kama uamuzi na vitendo vya uokoaji. Haikuwezekana wakati huo hata sasa ndege ikiwa mita 100 majini.

Septemba 20, 2018, miaka 20 baadaye, ndani ya ziwa ndani ya mita 100 kutoka ilitokea ajali ya kivuko cha Mv Nyerere huko Ukara, waliookolewa walikuwa wachache, wengi walifariki dunia. Kati ya hao wachache, idadi kubwa iliokolewa na wananchi wa kawaida wasio na vifaa.

Hivyo, katika kuitazama ajali hii ya ndege, nusu ya vipaumbele vinapaswa kuelekezwa kwenye makosa ya uokoaji.

Wataalamu wa uokoaji Uwanja wa Ndege Bukoba na uongozi wake mzima wanapaswa kuwajibika, hawakimbii lawama.

Kama ingekuwa walikuwa macho na wakaenda kwenye maji haraka kutoa msaada vifo vikatokea, ungeweza kuwatetea kwamba walifanya kadiri ya uwezo wao. Tofauti iliyopo hapa ni kwamba hawakuonekana.


Ukaidi wa wataalamu

Ukisikiliza simulizi za walionusurika, unagudua kuwa ndege ya Precision Air, haikutua Ziwa Victoria kwa dharura, bali hali ya hewa ilimpoteza rubani. Kulikuwa na mvua, wingu na ukungu.

Mmoja wa walionusurika, Richard Komba, aliyesafiri na ndege hiyo kutoka Dar es Salaam, alisema walitaarifiwa na rubani kuhusu hali ya hewa kuwa mbaya, hivyo ndege ilizunguka anga ya Bukoba, kungoja patulie watue.

Kwa hali hiyo, rubani aliwaeleza kwamba wangevuta subira kuona mabadiliko, na kama ingeshindikana kutua Bukoba kwa sababu ya hali ya hewa, ingebidi warudi Mwanza. Hivyo ndege ikaendelea kuzunguka maeneo mbalimbali kwenye anga ya Kagera.

Baadaye, rubani aliwatangazia abiria wajiandae kwa kutua. Na kilichofuata wakajikuta wapo kwenye maji. Hizo ni simulizi. Kwa bahati mbaya, rubani na msaidizi wake ni sehemu ya waliofikwa na mauti kwenye ajali hiyo, hivyo, tunashika kinachosimuliwa na walionusurika pekee.

Chukua sentensi mbili zinazodaiwa za rubani; ya kwanza ni kuwa kama ingeshindikana kutua wangerejea Mwanza. Ya pili, ni abiria wajiandae kutua. Utapata tafsiri kuwa rubani aliona hakuna sababu ya kurejea Mwanza, hivyo wangeweza kutua salama.

Sasa, unaweza kupatia ukisema huenda rubani aliona maji akachanganya na uwanja, matokeo yake akatua ziwani. Hapo kuna mambo matatu, ama kulazimisha kutua, mazingira magumu ya uwanja na ukaidi wa ushauri wa wataalamu wa hali ya hewa.

Tunaweza kuistahi dhambi ya rubani kutua wakati mazingira hayakuwa salama. Mungu ameshamchukua. Iwe funzo kwa wengine. Tushike maagizo na ushauri wa wataalamu wa hali hewa.

Mkurugenzi wa Utabiri, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Hamza Kabelwa alisema kuwa walitoa tahadhari siku moja kabla kuhusu hali ya hewa ya Kagera ingekuwa na mvua, mawingu na ukungu.

Katibu Mkuu Uchukuzi, Gabriel Migire alisema kuwa hali ya hewa ilikuwa mbaya, ukungu ulikuwa mzito hivyo rubani aliweza kuona mbele kwa kilometa mbili wakati kwa uhalisia hupaswa aone si chini ya kilometa 10.

Ufafanuzi wa Migire unaonyesha kuwa kilichotabiriwa na TMA ndicho kilitokea. Kwa maana hiyo, kama wahusika wangezingatia ushauri wa kitaalamu, pengine ndege isingepelekwa Bukoba asubuhi Novemba 6 au isingeruhusiwa kutua.

Hili linaigusa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) na Mamla ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA). TCAA kupitia taarifa ya TMA, wangezuia ndege kuingia na kutoka anga ya Kagera mpaka pale hali ingetulia. TAA wangekataza utuaji na upaaji wa ndege Uwanja wa Ndege Bukoba.


Ugumu wa uwanja

Mazingira magumu ya Uwanja wa Ndege Bukoba ni nyuzi nyingine 90. Sasa tunafikisha nyuzi 270. Ukiacha makosa ya kibinadamu, uwanja wenyewe ni tatizo kubwa na wataalamu walishapendekeza ujengwe mwingine.

Uwanja wa Ndege wa Bukoba, una eneo dogo la kutua na kurushia ndege (runway). Hakuna uwezekano wa kuongeza ukubwa wa uwanja kwa sababu upo katikati ya Ziwa Victoria na Kisiwa. Ndiyo maana wataalamu walishauri ujengwe uwanja mwingine ambao ungekuwa salama katika eneo la Omukajunguti

Uwanja huo hauna taa za kuongozea ndege nyakati za usiku, kwenye mvua, wingu kali au kukiwa na ukungu. Hii inaweza kusababisha rubani kuipeleka ndege majini akidhani ni uwanjani. Endapo uwanja mpya ungejengwa na kuwekewa taa, ingekuwa rahisi marubani kuona vizuri njia na kutua salama.

Swali ni kwa nini haukujengwa? Jibu lake lipo kwenye taarifa ya Ikulu ya Novemba 6, 2017. Rais John Magufuli alikataa kujengwa uwanja mpya kwa kile kilichoelezwa ni kuzuia matumizi mabaya ya fedha za Serikali.

Maandalizi yote ya ujenzi wa uwanja mpya yalikuwa yameshafanyika eneo la Omukanjunguti, Bukoba. Wananchi wenye nyumba zao ndani ya eneo lililopangwa kujengwa uwanja, walilipwa karibu Sh9.2 bilioni, hata hivyo, Magufuli alizuia ujenzi wa uwanja huo.

Magufuli hayupo duniani ila madhara ya uamuzi wake yanaonekana. Kagera haiwezi kuendelea kuhudumiwa na Uwanja wa Ndege wa Bukoba ni lazima mwingine ujengwe.

Mazingira magumu ya uwanja ni moja ya sababu ya ajali hii na nyingine. Si vema kukataa ushauri wa wataalamu. Viongozi wahakikishe wanafanya uamuzi mzuri na salama kwa ajili ya wananchi.


Motisha ya waokoaji

Kijana Majaliwa Jackson, peke yake amehusika kuokoa watu 24 walionusurika kwenye ajali. Tena akaumia alipokuwa anapambana kuokoa wengine zaidi akisaidia na wengine wakiwemo wavuvi.

Majaliwa ndiye aliyevunja mlango kwa kutumia kasia, hivyo kuwaokoa abiria waliokuwa ndani ya ndege.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila, alimpa Majaliwa motisha ya Sh1 milioni, kwa niaba ya Waziri Mkuu. Kisha, kijana Majaliwa amepelekwa kwenye mafunzo ili aajiriwe na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan. Pongezi kwa Samia kuona kuwa shujaa huyo anastahili kitu kitakachomkumbusha tukio hilo katika maisha yake.

Lakini, kwa kazi ambayo Majaliwa alifanya kwa kushirikiana na wenzake, motisha iliyotoka ni ndogo. Ikiwa kuna watu wanalipwa mishahara na kutengewa bajeti za uokoaji na kazi hawafanyi, kwa nini uwape mashujaa waliofanya kazi kubwa ya kuokoa maisha ya watu 26, Sh1 milioni tu? Ni changamoto kwa Serikali kuona nini inapaswa kufanya. Bajeti za uokoaji ni kiasi gani? Wanaolipwa mishahara walifanya nini?

Bajeti za uokoaji zilisaidia nini? Hatua zichukuliwe.