Sh40,000 zilivyokatisha ndoto za shujaa Majaliwa

Majaliwa Jackson (20)

Muktasari:

Mama mzazi wa kijana Majaliwa Jackson (20), kijana aliyefanikisha kuokolewa abiria 24 kwenye ajali ya ndeye ya Precision Air, ameeleza maisha ya kijana huyo aliyeshia kidato cha pili kwa kukosa ada ya Sh40,000, kuwa hupenda kusaidia watu tangu utotoni.



Mwanza/Bukoba. Mama mzazi wa kijana Majaliwa Jackson (20), kijana aliyefanikisha kuokolewa abiria 24 kwenye ajali ya ndeye ya Precision Air, ameeleza maisha ya kijana huyo aliyeshia kidato cha pili kwa kukosa ada ya Sh40,000, kuwa hupenda kusaidia watu tangu utotoni.

Arodia Bernado, mama mzazi wa Majaliwa, alisema hayo akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake eneo la Nyamkazi, Manispaa ya Bukoba, jana akiishukuru Serikali kwa kumzawadia mwanaye fedha na kumpatia ajira.

Arodia ambaye Majaliwa ni mtoto wake wa pili kati ya wanne, alisema fursa ya ajira na uhakika wa kipato utamwezesha mwanaye kutimiza ndoto zake kimaisha ikiwamo kurejea darasani kumalizia elimu yake.

“Mtoto wangu alilazimika kuacha shule akiwa kidato cha pili kwa kukosa Sh40, 000 za sare, madaftari na mahitaji mengine ya shule. Naamini atarejea shuleni kwa sababu ndiyo ndoto yake siku zote,” alisema.

Alisema tangu akiwa shule ya msingi na hata alipojiunga sekondari, Majaliwa alikuwa analazimika kwenda mwaloni kufanya uchuuzi wa samaki kupata kitoweo na fedha kwa ajili ya mahitaji ya familia.

“Kuna kipindi hakwenda shuleni muda mrefu hadi walimu wakatishia kufuta jina lake ikabidi niende kumwombea akakubaliwa kurudi darasani baada ya kuadhibiwa,” alisema.

Bila kutaja mwaka, mama huyo alisema hali ya kiuchumi ya familia ilizidi kuwa mbaya Majaliwa akajiunga na kikundi cha vijana cha mwalo wa Nyamkazi kusomba dagaa na kujikuta akitumia muda mwingi huko badala ya kwenda shule.

“Majaliwa alipenda shule lakini alikatisha masomo akiwa kidato cha pili kwa kukosa Sh40, 000 za sare, madaftari na mahitaji mengine,” alisema.

Baadaye, Arodia alisema kijana wake iliacha kabisa na kujikita kwenye uchuuzi na kazi zingine za mkono ikiwemo kulima mashamba ya watu kutafuta fedha na mahitaji mengine ya familia,” alisema.

Alisema hata baada ya kukatisha masomo, mara kwa mara kijana huyo alimsisitizia nia yake ya kurejea darasani baada ya kupata uwezo wa kifedha za kugharamia masomo.

“Kuna siku aliniambia akishindwa kabisa kurudia masomo kupitia madarasa ya watu wazima, ataenda hata Veta (Chuo cha Ufundi Stadi) kusoma kozi ya udereva; naamini fursa ya ajira aliyopata itamfikisha kwenye ndoto zake,”alisisitiza.


Hofu kumpoteza

Akizungumzia siku ya uokoaji uliomfanya mwanaye shujaa, Arodia alisema “nilikuwepo wakati Majaliwa anaokolewa na kukimbizwa hospitali ya mkoa; nilikimbilia huko na kumkuta akiwa amewekewa mashine ya oksijeni huku amezungukwa na madaktari.

“Nilipata hofu ya kumpoteza tegemeo na shujaa wangu kiasi nami nilianza kuishiwa nguvu ikibidi nitolewe nje,” alisema mama huyo.

Alisema alipopata nguvu alirejea kwenye chumba alicholazwa mtoto wake na madaktari wakamtuliza kwa kumhakikishia kwamba atapona, ahadi iliyomrejeshea matumaini huku akiendelea kumwombea mtoto wake na majeruhi wengine.

“Alirejewa fahamu saa 11:00 jioni tangu alipozimia saa 4:00 asubuhi, nikajaribu kumsemesha lakini nikaambiwa, nimwache apumzike. Ilipofika Saa 2:00 usiku niliruhusiwa kumsemesha, nilimwita jina na kumuuliza kama ananifahamu akajibu kwa kuniita mama. Hapo nikajua shujaa wangu amerudi,” alisimulia


Msaada kwa wengine

Mama huyo alisema “tangu akiwa mdogo, Majaliwa amekuwa faraja kwa wengine kutokana na tabia yake ya kujishughulisha na matatizo ya watu; tabia hiyo imempa umaarufu kwenye mwalo wa Nyamkazi na visiwa jirani.

“Ndiyo maana hata anaposifiwa na kuzawadiwa sasa kwa kuokoa watu sisi tunamfahamu tunajua hiyo ndiyo hulka yake,” alisema. Mama huyo alisema Majaliwa hajaanza sasa tabia ya kujitosa majini kuwaokoa watu wanapopatwa na dharura majini kwa kuwa amewahi kufanya hivyo mara kadhaa.