Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kiingereza sawa ila tubaki Waswahili

Hali hii inajitokeza kwenye taasisi za Serikali, maeneo ya huduma za afya, sekta ya elimu, na hata katika maisha ya kila siku. Lugha hii, ambayo kihistoria si sehemu ya utambulisho wa mwananchi wa kawaida, imepewa hadhi ya juu kiasi cha kuwa kigezo cha “maarifa” au “ustaarabu.”

 Kasumba hii imeanza kutafuna msingi wa utambulisho wetu wa lugha na tamaduni, na kama hatutachukua hatua, huenda tukapoteza kabisa uzalendo wa kuenzi lugha yetu ya Kiswahili.

Moja ya maeneo ambayo kasumba hii imejikita kwa kina ni katika sekta ya afya. Katika hospitali nyingi nchini, hususan zile kubwa na zinazotoa huduma za rufaa, maneno ya Kiingereza hutawala kwenye mabango, taarifa na hata mazungumzo ya wahudumu. Tunaona maandishi kama OPD (Out-Patient Department), Laboratory, Pharmacy, Radiology, na mengine mengi. 

Japo maneno haya yanaweza kuwa sehemu ya istilahi za kitaalamu, ukweli ni kwamba sehemu kubwa ya watumiaji wa huduma hizo ni Watanzania wa kawaida ambao wanazungumza Kiswahili tu. 

Je, ni sahihi kwa taasisi zinazohudumia umma kutumia lugha ya kigeni katika kutoa huduma za msingi? Kwa nini tusitumie Kiswahili: “Idara ya Wagonjwa wa Nje,” “Maabara,” “Dawa,” au “Idara ya Mionzi”?

Pia, kasumba hii imepenya katika mfumo wa elimu. Watoto wanakuzwa kuamini kukimanya Kiingereza ni sawa na kuwa na akili sana. 

Wazazi wengi hujisifu watoto wao wakizungumza Kiingereza, hata kama hawajui maarifa mengi yakiwamo yale ya msingi tu maishani.

Katika shule nyingi za msingi na sekondari, hasa za binafsi, Kiswahili kinachukuliwa kama somo la kawaida lisilo na uzito,  wakati ambapo lugha hiyo ndiyo nyenzo kuu ya mawasiliano kwa jamii yetu.

Kasumba ya Kiingereza pia imejikita katika mawasiliano ya taasisi za umma na binafsi. Mabango ya matangazo ya kazi, taarifa kwa umma, au hata mialiko ya mikutano mingi ya kiserikali huandikwa kwa Kiingereza. 

Hii inaathiri uwezo wa wananchi wa kawaida kuelewa taarifa muhimu kuhusu nchi yao. Tunawezaje kujenga taifa lenye mshikamano ikiwa sehemu kubwa ya wananchi wanaachwa nyuma kwa sababu tu hawajui Kiingereza?

Ukiangalia hata katika majukwaa ya mijadala ya kitaifa au kwenye vipindi vya televisheni, mara nyingi mgeni au mtoa mada anazungumza Kiingereza, kisha msimulizi au mtangazaji hatoi tafsiri ya kile kinachozungumzwa. Matokeo yake, sehemu kubwa ya watazamaji wanashindwa kufuatilia mjadala.

 Huu si uzalendo. Ni ubeberu wa kisasa wa kifikra unaojificha nyuma ya mwamvuli wa "utandawazi."

Lugha ni utambulisho. Kiswahili si tu njia ya mawasiliano, bali ni kiini cha utamaduni wetu, historia yetu na mshikamano wetu kama Watanzania.

 Ilikuwa ni dhamira ya Mwalimu Julius Nyerere, kuhimiza matumizi ya Kiswahili kama lugha ya taifa na chombo cha maendeleo. 

Alifahamu kuwa ili kujenga taifa imara, ni lazima tuwe na lugha inayotuletea pamoja – lugha inayotueleweka sote. Alisisitiza kuwa elimu ya kweli ni ile inayotolewa kwa lugha ambayo wanafunzi wanaielewa.

Leo hii, hatuoni aibu kusema “I’m sorry” badala ya “Samahani.” Tunawapongeza watoto wetu kwa kusema “How are you?” lakini hatujali wanaposhindwa kuandika barua ya Kiswahili. 

Tunaita vikao kuwa meetings, hata kama vinahusu wanakijiji mbumbumbu ambao hawajawahi kusikia neno hilo. 

Haya yote si maendeleo; ni dalili ya kupoteza mwelekeo wa utambulisho wa Taifa letu.

Kasumba ya Kiingereza haimaanishi kwamba lugha hiyo haina umuhimu. Ni kweli kuwa Kiingereza ni lugha ya kimataifa na inatufungulia fursa nyingi katika biashara, elimu na teknolojia. 

Hata hivyo, matumizi yake yanapaswa kuwa ya kimuktadha, si kwa gharama ya kuua Kiswahili. 

Tunaweza kufundisha Kiingereza kama somo muhimu kibiashara, kidiplomasia na maeneo mengine, lakini tusisahau kuiendeleza Kiswahili kama lugha ya kufikiri, kubuni, kuongoza, na kuishi kama Watanzania.


Ni wajibu wetu sote, wazazi, walimu, watunga sera, wasomi na wananchi kwa ujumla, kukomesha kasumba hii. Tujifunze Kiingereza kwa manufaa ya kimataifa, lakini tuenzi Kiswahili kwa ajili ya mshikamano na maendeleo ya Taifa. Hospitalini, shuleni, kazini, na hata majumbani, tuonyeshe fahari ya kuwa Watanzania kwa kutumia Kiswahili kikamilifu. 

Tuchukue hatua sasa tuanze na sisi binafsi kwa kuipa heshima lugha yetu ya Kiswahili. Tuseme wazi: Kiswahili kinatosha!


Abeid Poyo ni mhariri wa makala wa Mwananchi. 0754990083