Kesi za madai katika Mahakama Kuu ya Tanzania
Muktasari:
Kiongozi mkuu wa Mahakama Kuu ni Jaji Kiongozi ambaye huteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jaji kiongozi ndiye msaidizi maalumu wa Jaji Mkuu katika utendaji wa kazi katika Mahakama Kuu na mahakama nyinginezo zote za ngazi ya chini yake.
Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni mahakama ya ngazi ya juu baada ya mahakama ya wilaya na mahakama ya hakimu mkazi. Mahakama hii imeanzishwa kwa mujibu wa ibara ya 108 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Kiongozi mkuu wa Mahakama Kuu ni Jaji Kiongozi ambaye huteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jaji kiongozi ndiye msaidizi maalumu wa Jaji Mkuu katika utendaji wa kazi katika Mahakama Kuu na mahakama nyinginezo zote za ngazi ya chini yake.
Pamoja na Jaji Kiongozi, kikatiba wanapaswa kuteuliwa majaji wasiopungua kumi na tano ambao watakuwa ni wa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao huwa wanateuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pamoja na uwapo wa Mahakama kuu pia vipo vitengo mbalimbali za Mahakama Kuu ambazo ni Kitengo cha Kazi, Ardhi na Biashara.
Kitengo cha Ardhi kimepewa jukumu la kusikiliza kesi zote zinazohusiana na masuala ya ardhi na nyumba japokuwa kesi hizi pia husikilizwa na Mahakama Kuu yenyewe.
Kitengo cha Kazi kimeanzishwa kwa lengo la kusikiliza migogoro ya kazi pamoja na kupokea rufaa za migogoro ya kazi ambayo huanzia katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi.
Pia, kuna Kitengo cha Biashara ambacho kimepewa jukumu la kusikiliza kesi zote zinazotokana na maswala mbalimbali ya kibiashara kati ya mtu mmoja na mwingine au taasisi moja na nyingine.
Ni muhimu sana ukatambua aina ya tatizo ulilo nalo na mahakama maalumu iliyopewa mamlaka ya kusikiliza na kushughulikia kesi za aina hiyo. Hii itakusaidia kuepuka usumbufu na gharama unayoweza kuingia bila sababu za msingi.
Kwa sababu ukienda kufungua kesi mahali pasipostahili mahakama hiyo au mpinzani wako atapata kigezo cha kukuwekea pingamizi kwamba mahakama hiyo haina mamlaka au sifa ya kusikiliza kesi hiyo, hivyo utashindwa kesi na kulipa gharama.
Mahakama kuu pia ina mamlaka ya kirufani kwa maana kwamba inapokea kesi za rufaa kutoka katika mahakama za chini, pale na mdaiwa au mdai, anakuwa hajaridhika na uamuzi wa mahakama ya mwanzo, wilaya au mahakama ya hakimu mkazi.
Katika mamlaka ya usimamizi Mahakama Kuu ina uwezo wa kuita na kukagua jalada la kesi la Mahakama Kuu au mahakama ya mwanzo, kutoa maelekezo kwamba mahakama ya wilaya iitishe jalada la mahakama ya mwanzo na kukagua mwenendo wa kesi ili kujiridhisha juu ya usahihi na uhalali wa uamuzi na kama sheria na kanuni zilifuatwa katika kusikiliza na kutoa hukumu ya kesi au la.
Kesi zinazopaswa kufunguliwa Mahakama Kuu ni zile ambazo haziwezi kusikilizwa na Mahakama za chini kimamlaka. Mamlaka ya kifedha ya Mahakama Kuu yanaanzia madai au mali yenye thamani isiyopungua Sh100 milioni.
Kesi za madai zinaendeshwa na mdai mwenyewe au kwa kuwakilishwa na wakili wake. Mdai ndiye mwenye jukumu la kufungua kesi, kuhakikisha kuwa mdai wake anapata taarifa za kesi hiyo, kuleta ushahidi na mashahidi wa kutosha mahakamani ili kuthibitisha madai yake na kuiachia mahakama kutoa maamuzi baada ya mdaiwa kutoa utetezi wake mbele ya mahakama.
Usiporidhika na uamuzi wa Mahakama Kuu bado unayo haki ya kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ndani ya siku 60.