Kero wananchi kukosa vitambulisho ifike mwisho

Jana tuliandika taarifa kuhusu kero aliyokutana nayo Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi kwenye ziara yake ya siku sita katika Mkoa wa Kagera kwenye kila wilaya kuhusu kutopatikana kwa vitambulisho vya Taifa vinavyotengenezwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).
Akiwa Kagera, kero kubwa iliyojitokeza kwenye kila wilaya alipotembelea, ni wananchi kukosa vitambulisho vya Taifa, jambo linalowakwamisha kupata baadhi ya huduma muhimu kama vile kusajili laini za simu.
Wananchi wa Kijiji cha Kumunazi kilichopo Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, walieleza kero ya kutopatiwa vitambulisho vya Taifa vinavyotolewa na Nida, jambo linalowakwamisha kupata baadhi ya huduma muhimu.
Hali hiyo haipo Kagera pekee, kwani changamoto hiyo imekuwa ikijitokeza katika maeneo mengi ya pembezoni.
Hata hivyo, changamoto ya wananchi wengi kukosa vitambulisho hivi imekuwa ikijitokeza kwa muda mrefu, na ni wakati mwafaka sasa kwa Serikali na taasisi husika kuchukua hatua madhubuti ili kumaliza tatizo hili mara moja.
Inafahamika kuwa vitambulisho vya Taifa ni kitambulisho rasmi kinachomthibitisha raia na kumwezesha kupata huduma mbalimbali za msingi, kama vile huduma za afya, benki, mikopo na haki nyingine za kiraia.
Zaidi ya hayo, kitambulisho cha Taifa ni muhimu kwa kuimarisha usalama wa nchi. Kwa kutokuwa na mfumo madhubuti wa utambuzi wa raia, Serikali inakuwa katika nafasi ngumu ya kudhibiti uhalifu, ugaidi na vitendo vingine viovu.
Kutokana na umuhimu wa kitambulisho hicho, ni vema mamlaka zinazohusika kuhakisha wananchi wanaondokana na kadhia hiyo kwa kupatiwa vitambulisho tena kwa wakati.
Tunaamini kukosekana kwa vitambulisho hivi kunafanya iwe vigumu kwa vyombo vya usalama kutekeleza majukumu yao ipasavyo, hali inaweza kuhatarisha usalama wa taifa.
Tunaamini mamlaka zinazohusika zitafanya jitihada mbalimbali kuondoa hali hii, ikiwamo urasimu katika mchakato wa upatikanaji wa vitambulisho, uhaba wa vifaa na rasilimali na ufikaji duni wa huduma katika maeneo ya vijijini.
Ili kumaliza changamoto hii, Serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka na za makusudi. Kwanza, ni muhimu kuwekeza katika teknolojia na miundombinu ya kisasa, ili kurahisisha mchakato wa utambuzi na utoaji wa vitambulisho.
Pia, Serikali inapaswa kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa vitambulisho vya Taifa na mchakato wa kuvipata, ili kuondoa upotoshaji na uvivu wa baadhi ya wananchi.
Ingawa kuna taarifa kuwa baadhi ya vitambulisho bado vipo katika ofisi za Nida, hiyo haiondoi umuhimu wa taasisi hiyo kuwafikia wananchi na kuwapatia vitambulisho.
Ni wazi kuwa vitambulisho vya Taifa vina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya nchi, hivyo changamoto ya wananchi kukosa vitambulisho inapaswa kushughulikiwa kwa haraka na kumalizika, ili kuhakikisha kila raia anapata haki yake ya kimsingi ya kuwa na kitambulisho hicho.
Tunaamini Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali watashirikiana kwa karibu kuhakikisha changamoto hii inafika mwisho na kila mwananchi anapata kitambulisho cha Taifa bila vikwazo.