Kauli za viongozi wa dini zipewe kipaumbele

Viongozi wa dini kwa nyakati tofauto, wamepaza sauti zao wakitaka uchaguzi mkuu uifanyike kwa amani bila kuathiri umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania. Pia, wengine wakashauri wanasiasa na vyama vya siasa kukaa mezani kufanya mariadhiano kama njia ya kudumisha haki, umoja na mshikamano wa Taifa.
Wote tunafahamu kuwa Oktoba, 2025 Tanzania itakuwa inafanya uchaguzi mkuu kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani na tayari joto limeanza miongoni mwa wadau wa uchaguzi.
Tunaungana na viongozi wa dini na makundi mengine ya jamii yanayoitakia mema nchi yetu, kuiomba Serikali, tunayoamini ni sikivu, wanasiasa na wadau wengine kuhakikisha uchaguzi huu unafanyika kwa amani.
Pia, tunazikumbusha mamlaka kusikiliza kilio cha wadau wa uchaguzi kuhusu mifumo ya uchaguzi ili haki itendeke kwa wadau wote.
Tunasema haya tukitambua kuwa, Katiba ya Tanzania inatambua nchi yetu inafuata mfumo wa vyama vingi vya siasa na kwamba wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwao.
Ukisoma Ibara ya 13(1) ya Katiba hiyo ya mwaka 1977 inasema watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria, na hiki ndicho ambacho kila Mtanzania anatamani kukiona.
Ni kutokana na msingi huo wa Katiba, ndio maana viongozi wetu wa dini wa madhehebu yote , Wakristo na Waislamu, wametumia sherehe zao za kidini kupaza sauti zao wakitaka amani, mshikamano na haki itendeke kwenye uchaguzi huo.
Akizungumza Machi 31, 2025 wakati wa Baraza la Idd El Fitri, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Alhaji Nuhu Mruma aliitaka Serikali kufanyia kazi dosari zilizojitokeza uchaguzi wa viongozi wa Serikali za mitaa 2024.
Katika ombi hilo, katibu huyo aliziomba mamlaka za Serikali kuzifanyia kazi dosari zilizoripotiwa katika uchaguzi huo na kusisitiza suala la kutenda haki katika kila hatua ya mchakato wa uchaguzi mkuu kwa kuwa, haki ndio msingi mkuu wa amani.
Mwishoni mwa wiki, tumewasikia viongozi wa madhehebu ya Kikristo wakiwamo maaskofu, mapadri, wachungaji na wainjilisti walipita humo humo wakitaka uchaguzi huo ufanyike kwa amani na haki itendeke.
Viongozi hao wa dini walihubiri “haki haki haki” katika mahubiri yao wakisema amani inapatikana tu katika mazingira ya haki na maeneo ambayo hayaendi sawa basi wadau waridhiane ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani.
Tunafahamu kwa muda mrefu, kilio kikubwa kwa vyama vya upinzani ni kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi, japo Serikali imetimiza matakwa lakini malalamiko yanayoendelea ni dhahiri kuna dosari ambazo zinapaswa kuangaliwa.
Tunapongeza hatua zilizochukuliwa kufanyiwa kwa marekebisho ya baadhi ya Sheria ya Uchaguzi na ile ya Vyama vya Siasa iliyofuta baadhi ya mambo ikiwemo mgombea kupita bila kupingwa.
Hata hivyo, bado kuna yanayolalamikiwa hivyo, Serikali haina budi kuyatolea ufafanuzi kwa wadau wanaohusika ili twende kwenye uchaguzi tukiwa wamoja. Tuaamini bado kuna nafasi kwa Serikali kukaa kitako na wadau wengine na kuzungumza kama ambavyo imekuwa ikifanya mara kadhaa.