Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Viongozi wa Serikali waonya vurugu za uchaguzi

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Watanzania wahimizwa kujitokeza kuwania uongozi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2025

Dar/Mikoani. Viongozi wakuu wa nchi katika ujumbe wao wa Pasaka, wamezungumzia uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, wakiwataka wananchi kujitokeza kushiriki na kuepuka vurugu.

Mbali na hayo, wamewakataka kutafakari kuhusu upendo, haki na wajibu.

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ametoa rai kwa wazazi, hususani kina mama kuwaongoza watoto wao, hasa vijana kuacha tabia ya kushabikia vurugu wakati wa kampeni na uchaguzi mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu.

Dk Mpango ametoa rai hiyo aliposhiriki misa ya Pasaka leo Jumapili Aprili 20, 2025 katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska, Kiwanja cha Ndege jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk Mpango amewasihi Watanzania kushiriki uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu, akisema vurugu si sehemu ya jadi ya Watanzania.

“Mwaka huu ni wa uchaguzi wa kumchagua Rais, wabunge na madiwani niwaombe wananchi tukashiriki uchaguzi, vurugu si sehemu ya jadi ya Mtanzania.

“Kwa wote watakaopewa dhamana ya kusimamia uchaguzi tunawasihi sana wakazingatie sheria na miongozo waliyopewa, wakatende haki kwa wote wakakaojitokeza kugombea uchaguzi,” amesema.

Kwa watakaopata dhamana ya kusimamia uchaguzi, amewataka kuhakikisha wanazingatia sheria na miongozo watakayopewa na kutenda haki kwa wote watakaojitokeza kugombea.

Mbali na hayo, amewasihi watumiaji wa vyombo vya moto kuwa na busara na makini ili kuepusha kupoteza maisha ya watu barabarani.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amewaasa Wakristo kuliombea Taifa amani, utulivu, umoja na mshikamano uendelee kuelekea uchaguzi mkuu.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu imeeleza Dk Biteko amesema jijini Mwanza alikoshiriki ibada ya Pasaka katika Kanisa la African Inland Church (AIC) - Makongoro.

“Mwaka huu ni wa uchaguzi na una michakato mbalimbali ya kujiandikisha, kugombea, kupiga kura na kutangaza matokeo. Kwa niaba ya Serikali napenda kuwaomba waumini wa AICT na wale ambao tunadhani tuna uwezo wa kugombea nafasi mbalimbali tujitokeze kwa wingi tugombee, wale tu wenye nia ya kweli tuhakikishe tunawasaidia watu katika hali zao,” amesema.

Pia, amewahimiza waumini kuliombea Taifa kuelekea, wakati na baada ya uchaguzi.

“Tujitokeze ili tuweze kugombea kwa ajili ya kuhudumia nchi yetu na wakati wa kampeni utakapofika naomba tuendelee kuliombea Taifa,” amesema.


Ujumbe wa Rais Samia

Rais Samia Suluhu Hassan, amewatakia kheri Wakristo na jamii kwa jumla katika kuadhimisha sikukuu ya Pasaka akiwataka kutafakari kuhusu upendo, haki na wajibu.

Kupitia mitandao yake ya kijamii jana, Rais Samia amesema: “Siku hii njema ikawe pia ya tafakari kwetu sote juu ya upendo wetu kwa muumba wetu na wenzetu; juu ya kujitoa kwa bidii na weledi katika utekelezaji wa majukumu yetu popote pale tulipo.

“Juu ya kuendelea kujenga jamii inayoishi katika kweli na juu ya haki ambazo daima huambatana na wajibu kwetu sote.

 “Kwa pamoja tuendelee kuliombea Taifa letu kheri, huku tukiishi na kutenda yale yanayoiwezesha nchi yetu kuendelea kubaki kuwa moja, imara, yenye amani na utulivu.”

Akizungumza katika Usharika wa Moshi Mjini wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava amesema uongozi ni utumishi na utumishi ni kwa ajili ya watu, akiwataka Watanzania wote katika eneo lolote walilopo kujitoa kwa ajili ya wengine.

"Kuteswa kwa Bwana wetu Yesu Kristo na kufa kwake ni kwamba maisha yetu wakati mwingine yanapaswa yawe kwa faida ya wengine na kutanguliza wengine bila kutazama nafsi zetu sisi wenyewe na mambo yetu sisi wenyewe.

"Ikiwa ni katika eneo lolote lile, kwenye utumishi wa umma, utumishi kwenye sekta binafsi, kwenye familia, popote pale ulipo, wakati mwingine ni bora kuwasaidia wengine bila kujitanguliza wewe na ndivyo bwana wetu Yesu Kristo alifanya kwa gharama ya kutoa hata nafsi yake na uhai wake kwa ajili ya kutukomboa sisi sote. Hivyo tunapoendelea kutafakari ukuu wa Yesu Kristo nasi pia tuende kwa mtazamo huo," amesema.