Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Inashangaza walimu kuwabebesha mimba wanafunzi

Muktasari:

Geni zaidi hasa kwa siku za karibuni ni taarifa kuwa baadhi ya walimu ndio vyanzo vya hali hiyo ambayo mwishowe husababisha wanafunzi kuachishwa shule.

Si jambo geni kusoma au kusikia taarifa kupitia vyombo vya habari kuhusu matukio ya wanafunzi wa kike kupata ujauzito masomoni.

Geni zaidi hasa kwa siku za karibuni ni taarifa kuwa baadhi ya walimu ndio vyanzo vya hali hiyo ambayo mwishowe husababisha wanafunzi kuachishwa shule.

Ile kauli ya mtoto wa mwenzako ni wako kwa sasa ipo chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu kwani miongoni mwetu kumeibuka wanaume wakware wakiwamo walimu wanaowaharibu watoto wa kike.

Hivi karibuni huko wilayani Rombo Mkoa wa Kilimanjaro wanafunzi 34 wa shule za sekondari walikatisha masomo yao baada ya kupata mimba. Tatizo lililoripotiwa kujikita zaidi katika Tarafa ya Tarakea, ambayo inaundwa na kata za Motamburu, Kitendeni, Tarakea Motamburu, Reha na Nanjara. Kuweka kumbukumbu sawa, Rombo ni miongoni mwa wilaya zilizoripotiwa kuwa na matukio ya mimba nyingi za utotoni.

Kwa mujibu wa Kaimu ofisa elimu sekondari, Viane Mgoma, mwaka 2015 zaidi ya kesi 27 za mimba kwa wanafunzi ziliripotiwa wilayani hapo.

Tukio jingine la aibu ni la mwalimu wa Shule ya Msingi Simbo wilayani Igunga Mkoa wa Tabora kushikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumtia mimba mwanafunzi wake wa kidato cha kwanza mwenye umri wa miaka 15, binti aliyebainika baada ya babu yake kubaini kuwa ameacha ghafla kuhudhuria masomo.

Kama hiyo haitoshi miezi kadhaa iliyopita walimu watano wa Shule ya Sekondari Mihama, Kata ya Kitangili, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, walisimamishwa kazi na kushikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufanya mapenzi na wanafunzi wao.

Kwa matukio hayo machache yaliyoripotiwa yanaonyesha picha mbaya kwa walimu, watu wanaoaminika katika jamii kuwa walezi bora wa watoto wawapo shuleni.

Matukio haya yanaichafua taaluma ya ualimu ambayo ilijijengea heshima kubwa tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere kwani walimu waliitwa viongozi kila walipokuwapo.

Swali kwa walimu na wanaume wakware wengine wanaowatolea mate watoto wa kike; mnajisikiaje kuwa sehemu ya matatizo na mkwamo wa elimu kwa mabinti hawa?

Hamuwazi kuwa hawa nao wanahitaji kufikia angalau mlipofikia nyie? Nini kimewakumba mpaka nanyi mnasahau maadili ya kazi na kufanya mapenzi na watoto wenu? Na pia, utajisikiaje ikiwa binti yako akipewa mimba na kukatisha masomo?

Ukijiuliza haya na kupata ghadhabu ujue matendo haya ni aibu na hayapaswi kuendelea kutokea. Nilipata bahati ya kutembelea baadhi ya shule katika mikoa ya Mbeya na Katavi na kufanya mahojiano na baadhi ya walimu.

Wengi wanasema ni walimu wachache wasio na wito na maadili, wanaoweza kujihusisha na matendo ya aibu kwa wanafunzi wao na hawa wanapaswa kuhojiwa kuhusu wito wao katika kazi hii adhimu.

Ikumbukwe kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi za Kiafrika zilizoadhimisha siku ya mtoto wa Afrika Juni 16. Siku hiyo ina lengo la kutambua thamani, utu na umuhimu wa mtoto duniani. Elimu kwa watoto ndio imekuwa mada kuu kwa nchi nyingi katika kumuinua mtoto wa Afrika.

Tanzania mwaka huu iliadhimisha kwa kaulimbiu isemayo; “ubakaji na ulawiti kwa watoto vinaepukika: chukua hatua kumlinda mtoto”.

Kwa kupitia kaulimbiu hii walimu wakware waliotajwa katika ripoti mbalimbali wajitathmini upya kwa nini waliingia katika ualimu na namna bora ya kujisahihisha kabla rungu la dola halijawaangukia.

Ni kweli wapo walimu wengi bora ambao siku zote licha ya changamoto za kuwahudumia watoto, hawajawahi kutamani kufanya ufuska na wanafunzi wao kwa kuwa wanaheshimu maadili na miiko ya taaluma yao ya ualimu na wanatambua thamani ya muda wa mtoto wa kike akiwa masomoni.

Ni vyema tukaiga jitihada kama za kule wilayani Ulanga. Mwaka huu wameanzisha kampeni ya “Magauni Manne” kauli iliyofafanuliwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Christina Mndeme kuwa kuna sare nne muhimu kwa mtoto wa kike. Hizi ni sare ya shule, joho la mahafali, gauni la harusi na nguo ya mjamzito ambazo ni hatua za mwanafunzi wa kike anazopaswa kuzizingatia bila kuruka hatua yoyote.

Nawasihi walimu wa kiume waepukane na fedheha na tamaa kwa wanafunzi. Ninyi ni tegemeo na nguzo kwa taifa na ndio maana viongozi wengi waliofanya vizuri walianza kuwa walimu. Lindeni heshima yenu ili hadhi yenu na taaluma ya ualimu kwa jumla, iendelee kuwa juu na jamii na Serikali nayo itaungana nanyi katika kuleta elimu bora Tanzania inayozingatia usawa.

Dennis Mwasalanga ni ofisa program, idara ya habari na utetezi HakiElimu. [email protected]

Kwa taarifa zaidi nunua gazeti lako la Mwananchi au soma mtandaoni kupitia www.epaper.mcl.co.tz