Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hiki ndicho kinacholiponza Jeshi la Polisi

Nimemsikia Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Camilius Wambura akijiweka kando na shutuma za utekaji, lakini kiuhalisia kinachowaponza hadi wanyooshewe kidole ni kukiuka sheria zilizopo katika ukamataji wa washukiwa na upelelezi.

Ukamataji wa washukiwa usiozingatia Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) ya mwaka 2022 na Kanuni za Miongozo ya Jeshi la Polisi (PGO), kunafanya raia wema washindwe kutofautisha ukamataji wao na wa watu wasiojulikana.

Mbali na kukiukwa waziwazi kwa sheria, hata mwongozo namba moja wa Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) wa 2023, Polisi wetu hawaonyeshi chembe ya mabadiliko ya kifikra, weledi na maadili katika utendaji kazi wao.

Polisi wanakamata watu ‘kininja’, bila kujitambulisha wala kuwaeleza kosa linalowafanya wawekwe chini ya ulinzi, wanakaa na watuhumiwa kwa zaidi ya saa 24 bila kuwafikisha kortini na ndugu wanapowaulizia wanakana kuwashikilia.

Mfano mzuri ni wa kada wa Chadema, wilayani Handeni mkoani Tanga, Kombo Mbwana, ambaye alichukuliwa na watu wasiojulikana na kutoonekana siku 29 na Polisi wakatoa RB ya kumtafuta, lakini baada ya siku 29 wanakiri kumshikilia.

Hali hii ikiendelea, ipo hatari ya wananchi kuanza kuwashambulia makachero wa Polisi na pengine hata kusababisha mauaji kwa kisingizio cha kukabiliana na magenge ya wahalifu wanaoteka watu kwa mwavuli wa Jeshi la Polisi.

Sasa tumemsikia IGP Wambura akisema Jeshi hilo halihusiki na shughuli za utekaji wa watu au kupotea kwa watu kunakofanywa na watu wasiojulikana, akisisitiza wajibu wao Jeshi la Polisi ni kulinda usalama wa raia wema na mali zao.

IGP akaenda mbali na kusema wale wanaolituhumu Jeshi hilo kwa vitendo hivyo vya utekaji wa watu wanalikosea adabu na kutolea mfano wa matukio ya watoto walitekwa na watekaji kuomba fedha, na kuhoji kama hao nao ni Polisi.

Kauli hii ya IGP ukiifanyia uchambuzi (analysis) utagundua kuna kitu anataka kukisema hataki kukisema, kwa sababu Kombo ni mfano halisi wa Polisi kuteka kwa sababu ukamataji wao haukuzingatia sheria, haki za binadamu wala weledi.

IGP tungemwelewa kama angezungumzia kutekwa kwa mwanamtandao Edga Mwakalebela maarufu kama ‘Sativa’, na kwenda kutupwa Hifadhi ya Taifa ya Katavi, lakini kabla ya kupelekwa huko anadai alilala karakana kituo cha Polisi Oysterbay.

Hakuna maelezo ya kutosha nani walimpeleka Sativa Oysterbay Polisi, na kuchukuliwa kwenda kupigwa risasi huko Katavi, lakini katikati ya kelele za wananchi juu ya ndugu zao kutekwa, IGP anakuja na kauli nyepesi sana.

Nasema ni kauli nyepesi ambayo haijibu kilio cha waliopotelewa na ndugu zao kwa staili ya kutekwa, kwa sababu kuna orodha ndefu ya watu hawajulikani walipo na hili lilijitokeza sana hata katika mikutano ya Paul Makonda akiwa Katibu wa Itikadi.

Sasa ili tuliamini Jeshi la Polisi kuwa hawahusiki na matukio hayo na hapa sizungumzii wale walioteka watoto au kujiteka na kuomba fedha (ransom), ni lazima Jeshi la Polisi litekeleze majukumu yao ndani ya sheria na si vinginevyo.

Nasema hivyo kwa sababu hata kifungu cha 32 (1) cha CPA kinataka mshukiwa aliyeko mahabusu (ukiondoa makosa yasiyo na dhamana) afikishwe kortini ndani ya saa 24 na kama wanaona hawawezi basi adhaminiwe au ajidhamini.

Sasa tujiulize, polisi wetu wanafanya haya? Tuchukulie tu mfano wa makosa aliyoshitakiwa nayo Kombo, yana dhamana au hayana? Kwa nini Polisi walimshikilia kwa siku 29 bila uhalali wowote kisheria, tena awali wakikana kumshikilia.

Katiba ya Tanzania Ibara ya 13(5)(b) inasema ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika anayo hatia ya kutenda kosa hilo, sasa vipigo vya washukiwa polisi vya nini?

Wiki iliyopita tu, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imelinyooshea kidole Jeshi la Polisi kwa wananchi kupigwa, kufanyiwa ukatili na mateso wanapokuwa mikononi mwa polisi na washukiwa kutopewa dhamana.

Tunafahamu suala la ukamataji kininja lilibainishwa na Tume ya Haki Jinai, ikisema uwepo wa vyombo vingi vya ukamataji na vyenye mahabusu ni sababu mojawapo ya watu waliokamatwa kupotea mikononi mwa vyombo vya dola hapa Tanzania.

Hata hivyo, hili la Tume ya Haki Jinai kamwe haliwezi kuwabeba polisi kwa sasa, kwani vidole ambavyo Jeshi la Polisi linanyooshewa ni vingi, hivyo ni wajibu wa IGP kuacha blaablaa na kulisimamia Jeshi lake litimize wajibu wake kwa weledi.

Kamateni watu kwa mujibu wa sheria, ili wakija watu wasiojulikana basi nguvu ya umma itumike kuwakabili, kwani itakuwa rahisi kutofautisha polisi na watu hao.


0656600900