Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Gamondi atumie FIFA Series kama daraja

Kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' Miguel Gamondi. Picha na Mtandao

Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ipo kwenye hatua muhimu ya maandalizi kuelekea Fainali za Kombe la Mataifa Afrika 2027 (AFCON 2027), ambazo Tanzania itakuwa mwenyeji pamoja na Kenya na Uganda.

Kabla ya mashindano hayo makubwa, Stars itashiriki michuano ya FIFA Series itakayofanyika nchini Rwanda baadaye mwezi huu, ambapo itamenyana na mataifa ya Aruba, Macau na Liechtenstein chini ya kocha mpya, Miguel Gamondi.

Hii ni mara ya pili Stars inashiriki michuano hiyo ambapo mara ya kwanza ilikutana na Bulgaria na Mongolia.

Michuano hiyo ni fursa kwa Stars kujijenga upya, kuimarisha kikosi na kuweka misingi imara ya mafanikio ya baadaye baada ya kufanya vizuri kwenye michuano ya Afcon iliyopita pamoja na ile ya CHAN.

Kushiriki FIFA Series, kunatoa nafasi ya kujenga muunganiko wa kikosi lakini pia kumsaidia kocha wa timu hiyo kupata kikosi imara kwa ajili ya mashindano makubwa yajayo.

Kwa kuwa Gamondi ni kocha mpya baada ya kutangazwa rasmi hivi karibuni, mashindano haya yatampa muda wa kuwafahamu wachezaji wake zaidi, kuelewa uwezo wao na kuanzisha falsafa yake ya soka akiwa kocha mkuu rasmi kwa kipindi cha miaka miwili.

Tunaelewa kuwa alienda na Stars AFCON 2025 nchini Morocco, lakini ni ngumu kuamini kuwa ule ndiyo ulikuwa uwezo wake wa mwisho kwa kuwa hakuwa na muda mrefu wa maandalizi kabla ya kwenda kwenye fainali husika. Mechi dhidi ya mataifa yenye mitindo tofauti ya uchezaji na mabara tofauti zitawasaidia wachezaji kuzoea mbinu mbalimbali, jambo litakalokuwa muhimu sana kwenye AFCON ambako hukutana na wapinzani wa aina tofauti.

Lakini michuano hiyo ni jukwaa la kuwapa nafasi wachezaji chipukizi kwa kuwa si mashindano yenye presha kubwa kama AFCON, Gamondi anaweza kuwajaribu vijana wapya bila hofu ya matokeo kuathiri hadhi ya timu. Hatua hii itasaidia kupanua wigo wa kikosi na kujenga ushindani wa ndani timu yenye ushindani wa ndani huwa na morali ya juu na wachezaji wake hujituma zaidi.

Pia mechi hizo zitasaidia kuongeza kujiamini ushindi dhidi ya mataifa hayo unaweza kuongeza morali ya kikosi na kuimarisha imani ya mashabiki kwa timu yao. Kujiamini ni silaha kubwa kwenye mashindano makubwa kama AFCON, hasa kwa kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji na matarajio yatakuwa makubwa, historia inaonyesha kuwa timu mwenyeji hupata nafasi kubwa kutoka kwa mashabiki, lakini pia hukumbwa na presha, hivyo kujiamini mapema ni jambo la msingi.

Hata hivyo, ili Stars ifanye vizuri kwenye AFCON 2027 ikiwa ni mara yao ya tano kushiriki kocha Gamondi anapaswa kuzingatia mambo kadhaa muhimu.

Kwanza, ajenge utambulisho wa timu hadi sasa kumekuwa na maswali mengi kuhusu jinsi ambavyo Stars inacheza kwa kuwa kila siku imekuwa na mtindo mpya,  ni vyema miaka miwili ya Gamondi akaonyesha kuwa timu yake inataka kuchezaje, kushambulia sana, kulinda sana au vyote kwa pamoja.

Kwa ujumla, FIFA Series ni hatua muhimu ya maandalizi kwa Taifa Stars kuelekea AFCON 2027. Ni jukwaa la kujenga kikosi, kujaribu mbinu na kuimarisha hali ya kujiamini ikiwa kocha Gamondi atatumia fursa hii vyema kwa kujenga timu yenye nidhamu, mshikamano na utambulisho wa kiuchezaji, Tanzania inaweza kuandika historia mpya kwenye michuano hiyo ya AFCON 2027.