Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bila elimu sahihi ya fedha kausha damu itatumaliza

Hivi karibuni nimemsikia Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) Tuse Joune akizitaka taasisi za fedha zikiwemo benki kuweka nguvu kwenye utoaji wa elimu ya fedha kwa wananchi.

Kwa mujibu wa mtendaji huyu, malalamiko ya wananchi wengi yanatokana na kukosa elimu ya klifedha hivyo ni muhimu kuwasaidia kabla ya kuingia kwenye mikopo ambayo itageuka kuwa mzigo kwao.

Nikimnukuu alisema, “Tumegundua kwamba huduma zinatolewa lakini inawezekana kila tunachokitoa hakitimizi malengo ya mlengwa, tumeona kuna mfumuko wa taasisi zinazotoa mikopo inayoumiza watu na si kwamba benki hazipo bali wanazikwepa kwa sababu hawana elimu ya fedha”.

Nimeona leo kuna haja ya kuzungumzia suala hili hapa uwanjani ikizingatiwa kwamba wanawake ndiyo waathirika wakubwa wa hii mikopo umiza. Ukisikia hiyo mikopo ya kausha damu waliokaushwa zaidi ni wanawake na ukifuatilia chanzo ni kukosa elimu ya fedha.

Iko hivi wengi wetu huwa tunataka fedha za haraka, sababu hii inakufanya usipate muda wa kufikiria wala kutafakari yanayoweza kutokea baada ya kuchukua huo mkopo ambao umeshawishiwa na taasisi inayokopesha.

Bahati mbaya ni wakati mwingine hao wakopeshaji wanafanya kusudi kabisa kutomueleza mtu aliyekopa hatari iliyopo mbele yake na wanafanya hivyo kukamilisha lengo lao la kukopesha wapate faida.

Na vile wanawake huwa tunaongozwa kwa hisia tunakimbilia kukopa bila kuangalia ya mbeleni, matokeo yake tunaishia kuuza vitu vya ndani ili kuweza kuendana na masharti ya mkopo.

Wenye bahati ni wale wenye hivyo vitu vya kuuza, kuna wenzangu na mimi wanaishia kudhalilika na kunyang’anywa hata hivyo vidogo wanavyomiliki wanajikuta wakiangukia kwenye aibu na kuathiri familia zao.

Niliwahi kukutana na binti mmoja mwanafunzi wa kidato cha tano, anasema mama yake alitoweka nyumbani katika mazingira yasiyoelezeka chanzo kikubwa kikiwa ni mikopo.

Binti yule anasema alikuwa akishuhudia mara kwa mara watu kutoka taasisi za fedha zinazokopesha mitaani wakimfuata mama yake kumdai, baada ya kusongwa sana akaamua kutoroka nyumbani ni zaidi ya mwaka mmoja sasa.

Hapo ndiyo narudi kwenye kauli ya Mkurugenzi Mtendaji wa TBA kwamba kuna ombwe kubwa la elimu ya fedha kwa wananchi, wengi wanakimbilia kupata mikopo ya haraka bila kuangalia faida na hasara zake.

Inawezekana benki zina masharti au milolongo inayowafanya wengin wakwepe kuzifuata taasisi hizo lakini ukweli unabaki pale pale angalau upande huo una usalama kuliko hizi kausha damu zinazotufuata hadi majumbani kutukopesha.

Kukabiliana na hilo nisisitize hapo kwenye elimu, ifike pahala benki zishuke kwa wananchi zikatoe elimu ya fedha. Hii itasaidia watu kuwa na maamuzi sahihi wanapofikia uamuzi wa kuchukua mikopo na kwenda kwenye taasisi zinazoheshimu haki na kulinda utu wa wakopaji.

Nikiweka msisitizo kwa benki ni muhimu kwenu mkatambua kwamba kuna uhitaji mkubwa wa mikopo hivyo zinahitajika programu za elimu ya fedha kwa makundi muhimu kwenye jamii hasa wanawake na vijana.

Wito wangu kwa wakopaji hasa wanawake ni muhimu tukajiridhisha kwanza kabla ya kuingia kwenye mikopo.

Ni kweli tumetingwa na mambo mengi ila muhimu kuitafuta elimu ya fedha hata kama hauna mpango wa kukopa huenda ikakusaidia siku za usoni ukiwa na uhitaji huo.