Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Afcon U20 lengo lisiwe kufuzu tu

Mashindano ya kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa umri chini ya miaka 20 (Afcon U20) kwa ukanda wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) yalianza jana hapa Dar es Salaam, Tanzania.

Kinyang'anyiro cha kuwania tiketi ya Afcon U20 kilianza kwa mechi iliyokutanisha mwenyeji Tanzania 'Ngorongoro Heroes' dhidi ya Kenya na baada ya hapo Sudan ikaikabili Djibouti.

Idadi ya timu tisa kutoka nchi wanachama wa Cecafa zitakuwa zikiwania nafasi mbili za kuwakilisha ukanda huu kwenye fainali za Afcon U20 ambazo zitafanyika mwakani katika muda na eneo ambalo zitapangwa.

Timu hizo tisa ambazo zitatumia viwanja vya KMC Complex na Azam Complex vilivyopo hapa Dar es Salaam  ni Tanzania, Kenya, Sudan, Djibouti na Rwanda ambazo zimepangwa katika kundi A na kundi B lina Uganda, Sudan Kusini, Ethiiopia na Burundi.

Uganda ndio bingwa mtetezi wa mashindano hayo ya kuwania kufuzu Afcon U20 kwa kanda ya Cecafa ikiwa imelitwaa mara mbili mfululizo zilizopita ambazo ni 2020 na 2022 na kabla ya hapo bingwa ilikuwa ni Tanzania.

Baada ya kukosa taji kwa awamu mbili mfululizo zilizopita, hapana shaka Ngorongoro Heroes itaitoa kimasomaso Tanzania kwa kutwaa ubingwa wa mashindano hayo na kujihakikishia tiketi ya kufuzu Afcon U20.

Hata hivyo wachezaji na benchi la ufundi la Ngorongoro Heroes hawapaswi kufikiria kufuzu fainali hizo pekee bali wanatakiwa wawe na ndoto kubwa zaidi za mafanikio kupitia mashindano hayo ambayo yamekuwa yakiongezeka thamani siku hadi siku ndani na nje ya bara hili.

Kuamini kwamba kufuzu tu Afcon U20 kunatosha kuwa mafanikio kwa maofisa wa benchi la ufundi na wachezaji sio jambo sahihi na ni mawazo ya kujirudisha nyuma kwa nchi kiujumla na mtu mmoja mmoja.

Kushiriki Afcon U20 kunapaswa kuwa lengo dogo zaidi miongoni mwa yale ambayo timu inapaswa kuweka ikiwa inafanikiwa kukata tiketi ya kushiriki mashindano hayo.

Lengo mojawapo kubwa linapaswa kuwa ni wachezaji na makocha kujiweka sokoni na hili hilo litimie iko haja ya timu na mchezaji mmoja mmoja kucheza vizuri katika mechi zote ambazo zitaikabili timu katika mashindano hayo.

Ni fainali ambazo zinafuatiliwa na kundi kubwa la maskauti, mawakala na makocha wa soka kutoka pande tofauti duniani ambao hukusanyika mahali zinakofanyikia ili kusaka vipaji ambavyo wanaamini vitanufaisha timu zao nje na ndani ya uwanja siku za usoni.

Wanajazana kuvisaka hivyo vipaji kwa vile wanaamini wanapata wachezaji wazuri wakiwa katika umri mdogo hivyo timu hazitotumia gharama kubwa katika usajili wao ingawa baadaye zinaweza kuwauza na zikaingiza fungu la fedha.

Hii sio kwa wachezaji tu bali makocha nao ni sehemu ambayo wanaweza kuitumia kutengeneza wasifu wao na hivyo kujiweka katika uwezekano mkubwa wa kupata malisho ya kijani zaidi kutoka timu mbalimbali baada ya hapo.


Iko mifano mingi ya wachezaji na makocha ambao walinufaika kupitia fainali za A\fcon U20 na sasa wamepiga hatua kubwa zaidi ya pale walipokuwa mwanzoni.

Katika fainali zilizopita za Afcon U20, beki Omar Fayed aliitumikia timu ya taifa ya Misri akiwa mchezaji wa klabu ya Al Mokawloon Al Arab lakini baada ya hapo akapata fursa ya kusajiliwa na Fenerbahce inayoshiriki Ligi Kuu ya Uturuki.

Mfano mwingine ni mshambuliaji wa Senegal, Ibou Sané ambaye baada ya fainali zilizopita za vijana wa umri huo, alipata fursa ya kujiunga na Metz ya Ufaransa akitokea Generation Foot ya kwao Senegal.

Aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya Nigeria U20,  Paul Aigbogun baada ya kuiongoza timu hiyo katika fainali za Afcon U20 za 2019, ali[pata fursa ya kuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya nchi hiyo.

Ukiondoa hilo, tunategemea vijana waliopo katika kikosi cha Ngorongoro Heroes kwa sasa ndio waje kuunda timu ya taifa ya wakubwa 'Taifa Stars' hapo baaadaye.

Taifa Stars mwaka 2027 itashiriki fainali za Afcon ambazo Tanzania itakuwa mwenyeji pamoja na Kenya na Uganda.

Tegemeo kubwa ambalo wengi wanaamini litakuwa la wachezaji wa Taifa Stars ni hawa vijana ambao sasa wapo katika kikosi cha Mgorongoro Heroes.

Wapambane na kuhakikisha wanafuzu kushiriki Afcon U20 mwakani ili iwe jukwaa zuri kwao la kupatia uzoefu na ubora zaidi ambao utakuja kuinufaisha nchi katika Afcon 2027.

Litakuwa ni jambo la kushangaza ikiwa Ngorongoro Heroes itashindwa kufuzu Afcon U20 kupitia Cecafa na sidhani kama itakuwa na la kujitetea.

Kwanza inaundwa na kikosi cha idadi kubwa ya wachezaji ambao wana uzoefu wa mechi za ushindani kwa vile wanapata nafasi ya kutosha ya kucheza katika klabu zao na wengi ni tegemeo la makocha wa timu zao.

Lakini pili mashindano yanafanyikia nyumbani na wenyewe watapata sapoti kubwa ya mashabiki kulinganisha na timu nyingine shiriki.

Na ukiongezea na maandalizi ambayo wamepata, tunaamini kwamba wataipa heshima nchi kwa kubakisha kombe nyumbani na kufuzu Afcon U20.