Prime
HADITHI: Mwiba mdogo-2

ILIPOISHIA JANA...
Aliingia kwenye gari baada ya kufunguliwa mlango na dereva wake, wakati anafunga mkanda ili gari liondoke warudi ofisini, simu yake ya mkononi iliita.
Endelea...
Aliitoa mfukoni na kuitazama namba inayompigia ilikuwa ngeni, alijikuta akitaka kuacha kupokea lakini aliamua kuipokea.
“Haloo mzee Shila.”
“Ndiyo unasemaje?” aliuliza kwa ukali baada ya kusikia sauti ya mtoa taarifa.
“Mnaondokaje bila mwili wa marehemu?”
“Hakuna aliyekufa acha kuchezea jeshi la usalama.”
“Nilikueleza kuwa kifo cha mchungaji nakijua mimi peke yangu na wewe utakuwa mtu wa pili, sasa unakwenda wapi. Hata huyo sekretari hajui kinachoendelea ofisini kwa bosi wake. Rudini muondoke na mwili la sivyo mtarudi mara ya pili na kuukuta umeharibika vibaya. Huoni kama matumizi mabaya ya mali za uma kuchoma mafuta mara mbili?”
“Sawa nimekuelewa,” Shila alijikuta njiapanda akijiuliza mpigaji wa simu huenda anachokisema ni kweli.
Alimweleza dereva azime gari na kurudi hadi kwa sekretari ambaye alipowaona alishtuka.
“Vipi tena mkuu mbona mmerudi?”
“Nenda ofisini kwa bosi wako kama bado yupo kwenye maombi tutaondoka.”
“Sawa.”
Yule binti mrembo alinyanyuka kwa shingo upande hadi kwenye mlango wa mkuu wake, alijiuliza agonge au aingie. Aligonga taratibu lakini ndani hakukuwa na majibu yoyote.
Alizungusha kitasa taratibu mlango ulitii amri, aliusukuma kwa unyenyekevu kama baba Mchungaji yupo kwenye maombi asimsumbue.
Mlango ulifunguka taratibu na kumfanya binti kuingiza kichwa kuchungulia ndani ili ajue Mchungaji anafanya nini kwa vile siku ile haikuwa ya maombi.
Alishangaa kumkuta baba Mchungaji akiwa amejilaza juu ya meza. Mlalo ule ulimshtua kwa vile tangu amjue Mchungaji Samwel hakuwahi kumuona akijilaza juu ya meza.
Aliingia ndani na kusogea karibu yake, alishtuka kumuona mchungaji akitokwa na damu machoni, puani na maskioni, ulimi na macho vimemtoka pima, lilikuwa tukio la kutisha sana.
“Maaaaamaaaa!” Sekretari alipiga kelele.
Kwa vile mlango wa ofisi ulikuwa wazi, zile kelele zilimshtua Shila na vijana wake na kujikuta akisema kwa sauti ya chini:
“Kumekucha.”
Kwa haraka alichomoa bastola na kuingia ofisini kwa tahadhari kubwa, juu ya meza alikuwa amelala mchungaji Samwel akiwa anatoka damu sehemu zote zenye tundu za kichwa, macho na ulimi vilikuwa vimemtoka pima.
Kwake lilikuwa tukio la kwanza la kutisha la mtu kutokwa na ulimi nje na macho kuvimba, damu nyeusi zilitoka puani, mdomoni na masikioni.
“Mmh! Kazi ipo,” alisema huku akivaa glovu na kuugeuza mwili ule ambao hakuwa na uhai.
Wakati huo binti mrembo alikuwa ameanguka chini na kuzirai baada ya kuona tukio lile la kutisha.
Ili kupata mwanga wa tukio lile walimpatia huduma ya kwanza binti yule ili wajue kipi kimesababisha kutokea kitu kile.
“Pole binti,” Mkuu Shila alimsemesha kwa saui ya upole baada ya kuzinduka.
“Aa..aa..sante,” alijibu kwa sauti ya kilio.
Kabla ya kuendelea kumuhoji aliagiza aletewe glasi ya maji baridi ili kupunguza presha. Mpelelezi Shila aliendelea kumhoji.
“Unaitwa nani?” Shila alimuuliza kwa sauti ya upole.
“Siwezi kuongea inauma sana inauma,” yule binti alishindwa kuongea na kuangua kilio cha sauti kilichowavuta watumishi wa kanisa lile ambao mpaka muda ule hawakujua kumetokea kitu gani.
Baada ya kusikia kilichomkuta Mchungaji wao, nao waliangua vilio na kufanya sauti kuwa kubwa na kuwavuta wapita njia ambao walisogea kutaka kujua kulikoni vilio vile vya kanisa zima.
“Sikiliza binti lazima uzungumze, la sivyo kesi ya mauaji itakuwa kwako,” mkuu alimtisha ili aache kulia na kujibu maswali yake.
“Mimi?” aliuliza macho ameyatoa pima.
“Ndiyo, ulikuwa unatukataza kuingia kumbe umeshamuua mchungaji wako.”
“Jamaniii, mimi nimuue ili iweje?”
“Ndiyo maana tunataka maelezo yako ili tujue pa kuanzia.”
“Sa..sa..sawa ni..ni ta..ta,” binti alikuwa kwenye wakati mgumu.
Kabla ya kumuuliza maswali walimpa glasi nyingine ya maji kushusha presha ndipo walipoanza kumhoji.
Wakati huo watumishi wa kanisa walielezwa watulie mpaka taarifa ya kidaktari kama amekufa au yupo hai.
“Haya binti niambie unaitwa nani una muda gani hapa kanisani pia nipe ratiba yako ya jana na leo pia ratiba ya mchungaji wako.”
“Naitwa Sarah Mwilu, hapa kanisani nina miaka miwili kasoro, ratiba yangu ya kila siku nifikapo asubuhi hufanya usafi wa ofisi ya bosi ikiwa pamoja kuvipanga vitu vyake kwenye mpangilio mzuri, kisha ofisi yangu na kuandaa taarifa zote za kiofisi ambazo humkabidhi Mchungaji baada ya kuingia.”
“M’hu, niambie ratiba ya leo.”
“Baada ya kufika nilifanya majukumu yangu kama kawaida, leo mchungaji alichelewa kidogo baada ya jana kukesha kwenye misa ya maombi.
Baada ya kuingia ofisini nilimpelekea kifungua kinywa.”
“Kifungua kinywa gani?”
“Maziwa, mayai na juisi.”
“Ehe, endelea.”
“Basi baada ya muda alinijulisha amemaliza kufungua kinywa na mimi kwenda kutoa vyombo kisha nilirudi kuendelea na majukumu yangu ya kila siku. Nikiwa naendelea na majukumu yangu Mchungaji alinijulisha kuna mgeni atakuja hivyo baada ya kuzungumza atakuwa na mtoko wa kwenda Yombo ambako kuna sherehe la kusimikwa kiongozi wa kanisa la Mungu tawi la Yombo.”
Sarah alinyamaza kidogo kufuta kamasi nyembamba na kitambaa kisha aliendelea kuzungumza.
“Baada ya dakika kumi aliingia mwanamke aliyevalia vazi la kuficha macho.
“Hukushangaa mtu anayevaa mavazi hayo kuja kanisani?”
“Sikushangaa kwa vile huduma zetu hazikulenga imani ya dini moja, mtu anayevaa hivyo kuja pale hakuwa wa kwanza wapo hata waliotoa ushuhuda baada ya kufanyiwa muujiza na Bwana Yesu.”
“Ehe.”
“Basi yule mwanamke aliyevalia vazi la kubakiza macho alinisalimia na kujitambulisha anaitwa mtoto wa marehemu.”
“Nani?” Shila alishtuka baada ya jina lile kufanana na aliyetoa taarifa ya kifo cha mchungaji.
“Mtoto wa marehemu.”
“Mmh! Sawa, endelea.”
“Kwa vile taarifa zake nilikuwa nazo nilimruhusu aingie, alikaa ndani kwa zaidi ya saa moja na nusu kisha alitoka na kunieleza kuwa Mchungaji kwa muda ule hataki mtu mpaka aniite. Basi nami nilitii maagizo kwa vile haikuwa kauli mpya ya baba mchungaji.
Mchungaji anapokuwa na mambo yake. Nami niliendelea na majukumu yangu mpaka ninyi mlipofika.”
Kwa taarifa ile aliamini kabisa sekretari hajui chochote, hivyo angekuwa anapoteza muda bure. Aliamini yule mwanamke aliyekuja amevaa nguo ya kuficha macho ndiye muuaji, aliwaza kimoyomoyo kuwa lazima kuna siri nzito nyuma ya kanisa.
Wakati akijiandaa kurudi ofisini, kijana wake mmoja aliona kikaratasi chenye wino mwekundu. Alikichukua na kumpa bosi wake.
“Mkuu kuna ujumbe huu.”
Shila aliuchukua bila kuusoma na kutoka nje, wakati huo gari la wagonjwa lilikuwa limeshafika kuuchukua mwili wa Mchungaji Samwel na kuupeleka hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya kuufanyia uchunguzi na kuuhifadhi chumba cha maiti.
Akiwa ndani ya gari aliusoma ujumbe wa kwenye kalatasi uliokuwa umeandikwa.
“Huyu ni mmoja kati ya watano wa kufa, bado wanne, sipendi nikusumbue kunitafuta kwa vile hutanipata mpaka nikamilishe hesabu yangu, hapo ndipo nitajisalimisha mwenyewe.
“Mimi mtoto wa Marehemu.”
“Mmh kazi ipo.”
“Mkuu ujumbe unasemaje?” msaidizi wake alihoji baada ya kumuona mkuu wake baada ya kuusoma ujumbe kakunja uso.
“Eti huyu wa kwanza bado wanne.”
“Amesema sababu ya kuwaua?”
“Amesema atasema sababu akimuua mtu wa mwisho.”
“Yaani tusubiri awamalize wote tupo tu tunamsubiri?” Sele dereva wa Shila alihoji.
“Hapo ndipo kwenye mtihani mzito, hatuwajui kina nani na kwa nini anawaua.”
“Huenda ameuliwa baba yake,” mmoja alitoa wazo.
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Ni wazi walishirikiana kumuua baba yake hivyo analipa kisasi.”
“Maneno yako yanakaribiana na ukweli, tukiwajua watu wao wa karibu tutaujua ukweli.”
Itaendelea